Polisi yawashikilia Meya wa zamani Jacob, Malisa, kwenda kupekuliwa Dar, Moshi

Muktasari:

  • Boniface na Malisa wameshikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam wakishukiwa kwa tuhuma ya kufanya uchochezi wa kudai Polisi wanaua na kusababisha taharuki na chuki dhidi ya jeshi hilo na jamii.

Dar es Salaam. Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia Meya wa zamani wa Ubungo, Jacob Boniface na Mwanaharakati Godlisen Malisa kwa tuhuma za uchochezi, baada ya wawili hao kuitikia wito wa polisi.

Polisi wamedai hatua hiyo ni kinyume na kifungu 16 cha sheria ya mwenendo wa makosa mtandao.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Aprili 25, 2024 na Hekima Mwasipu, wakili wa watuhumiwa hao, katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

Mwasipu amesema kosa hilo la kimtandao linahusu pia kifungu namba 55 cha sheria ya makosa ya jinai, tuhuma hizo zinahusu uchochezi na kusababisha taharuki kwa jamii.

"Polisi wanasema Boniface na Malisa walichapisha kwenye mitandao ya kijamii tuhuma kwamba Jeshi la Polisi linaua raia, na tuhuma hizo kwa mujibu wa Polisi zinachochea chuki ya jamii dhidi ya Jeshi la Polisi," amesema Mwasipu.

Wakili Mwasipa amesema kutokana na tuhuma hizo Jeshi hilo limewataka wawili hao kupeleka simu zao lakini kwa bahati mbaya wateja wake wakati wanakuja kuripoti kwenye kituo hicho hawazikubeba na zipo maeneo tofauti.

"Simu ya Malisa iko Moshi (mkoani Kilimanjaro) na simu ya Boniface iko nyumbani kwa kwe Msakuzi Dar es Salaam, sasa Jeshi limesema linasafiri na Malisa kwenda Moshi na timu nyingine inaenda kupekua nyumbani kwa Boniface wapate hizo simu walizotumia kuchapisha taarifa hizo," amesema.

Wakili Mwasipa amesema kwa sasa Jeshi hilo litaendelea kuwashikilia hadi hapo simu hizo zitakapopatikana ndipo wataanza kuhojiwa.

"Kwa sasa Wataendelea kubaki chini ya Jeshi la Polisi hadi hapo simu walizotumia kuchapisha taarifa hizo zipatikane halafu Jeshi litaanza kuwahoji sasa," amesema.

Wakili huyo amesema simu hizo zitakwenda kuchukuliwa kwa mfumo wa upekuaji, wakiwa wameambatana na watuhumiwa hao.

"Atahusika mjumbe wa serikali za mitaa pamoja na mashahidi wengine ambao Polisi wataona wanafaa kuwepo katika shughuli hiyo," amesema.

"Kwa hiyo wanaondoka usiku huu wataenda Moshi ili wakachukue simu ya Malisa vilevile waende kwa Boniface wakachukue halafu baada ya hapo watarudishwa waweze kuchukuliwa maelezo mengine," amesema.

Hadi Mwananchi Digital linaondoka Kituo Kikuu cha Polisi 12:30 jioni, Boniface alikuwa amepandihswa kwenye gari kwenda nyumbani kwakwe Msakuzi.

Leo Alhamisi asubuhi, washukiwa hao walianza kuripoti kwenye Kituo cha Polisi Oysterbay wakiwa wameambatana na ndugu zao wengine watano kabla ya utaratibu kubadilishwa kutakiwa kwenda Ofisi za Kanda Maalum ya Dar es Salaam.

Mbali na Wakili Mwasipu wengine waliokuwa katika msafara huo ni Martin Masese, Hoops Kamanga, Noel Shao pamoja na Nasir Balozi.

Boniface na mwenzake waliingia katika ofisi hizo saa 8:42 mchana wakitumia muda mrefu kumsubiri Kamanda wa Upelezi wa Kanda hiyo ambaye awali ilitolewa taarifa alikuwa ametoka kwa shughuli zingine za kiofisi.

Mwananchi Digital lilipomtafuta Kamanda wa Kanda hiyo, Jumanne Muliro kutaka kujua hatma ya dhamana ya washukiwa hao amesema itajulikana baada ya mambo ya msingi ya mahojiano kukamilika.

"Mahojiano yakikamilika suala la dhamana litazingatiwa kwa mujibu wa sheria, hadi yakamilike mambo ya msingi wanayohojiana na wachunguzi wa jambo hili," amesema Muliro.

Sakata la Boniface na Malisa kutiwa mbaroni chanzo chake taarifa za kifo kilichozusha utata cha Robert Mushi aliyezikwa leo Alhamisi, Shirimatunda huko Moshi Mjini, Mkoa wa Kilimanjaro ambapo wawili hao walichapisha taarifa kuhusu kupotea kwake na baadaye mwili wake kupatikana katika Mochwari ya hospitali ya Polisi Kilwa Road.

Taarifa ya Polisi ilielezwa kuwa Mushi alifariki dunia kutokana na ajali.