Rais Samia aagiza bei ya gesi kupungua

Rais Samia Suluhu Hassan akihutubia viongozi, wananchi pamoja na wageni mbalimbali kabla ya kuzindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam leo Mei 8, 2024.

Muktasari:

  •  Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amezindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia huku akiagiza Wizara ya Nishati kukaa na sekta binafsi kuona jinsi ya kupunguza nishati safi.

Dar es Salaam. Huenda bei ya gesi ya kupikia ikapungua kutoka ile inayouzwa sasa, baada ya Serikali kuanza utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia.

Dalili ya kupungua bei ya nishati hiyo, imetokana na kauli ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuitaka Wizara ya Nishati ishirikiane na sekta binafsi kuona namna ya kuifanya bei ya gesi iwe himilivu.

Pamoja na hatua hiyo itakayoshinikiza matumizi ya nishati safi, mkuu huyo wa nchi ametoa marufuku ya matumizi ya kuni na mkaa kupikia kwa taasisi za umma na binafsi zinazohudumia watu zaidi ya 100.

Hatua hizo zote zinalenga kuweka msisitizo wa utekelezaji wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, unaotaka kufikia mwaka 2034, asilimia 80 ya Watanzania watumie nishati safi.

Mkakati huo unakuja katika kipindi ambacho, takwimu zinaonyesha asilimia 90 za kaya zote nchini zinatumia nishati ya kuni na mkaa. Hiyo ni sawa na kusema kati ya kaya 10, tisa zinatumia nishati isiyo safi kupikia.

Hali hiyo inatajwa kusababisha athari zikiwemo za magonjwa ya upumuaji yanayotokana na uvutaji moshi na kupoteza uhai wa takriban watu 33,000 kwa mwaka.

Hayo yalielezwa jijini Dar es Salaam leo Jumatano, Mei 8, 2024 na Rais Samia alipohutubia hafla ya uzinduzi wa mkakati wa matumizi ya nishati safi ya kupikia wa mwaka 2024/2034.


Bei ya gesi

Katika hotuba yake, mkuu huyo wa nchi aliielekea Wizara ya Nishati ikae na wadau ndani ya Serikali na sekta binafsi ili kubaini maeneo ya kufanyiwa kazi na kuongeza haraka upatikanaji wa nishati safi ya kupikia kwa gharama himilivu.

“Kaeni na wizara muone wapi tubane, wapi tuongeze na wapi tupunguze ili tuweke bei himilivu na wananchi wengi zaidi watumie (Nishati safi)," amesema Rais Samia.

Rais  Samia Suluhu Hassan akizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwenye hafla iliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNICC), Jijini Dar es Salaam leo Mei 8, 2024.

Dalili za kupungua kwa bei ya nishati hiyo na nyingine za kupikia pia imedhihirika katika kauli ya Rais Samia iliyotaka kuwekwa mazingira wezeshi ya upatikanaji wake, kwa kupunguza bei na kuongeza wingi madukani.

Katika msisitizo wake wa kupunguza bei ya nishati hiyo na nyingine safi za kupikia, aliibebesha Wizara ya Nishati jukumu hilo, huku Serikali kuu akisema itabeba jukumu la utoaji elimu na kutunga sera wezeshi.

“Jukumu la Serikali ni kutunga sera wezeshi kufikia malengo ya mkakati na kutoa elimu kwa wananchi, huku Wizara ya Nishati ikiwa na jukumu la kuhakikisha nishati safi inapatikana kwa uhakika na bei himilivu,” amesema Rais Samia.


Ombi la wadau

Ili kurahisisha upatikanaji wa nishati safi na kuwezesha bei himilivu, Meneja wa Masoko wa Kampuni ya Gesi ya Oryx, Peter Ndomba akizungumza na gazeti hili amesema ni muhimu kuondoa kodi katika jiko na viunganishi vyake.

“Katika kukaa kwetu na Serikali tutaanzia hapo kwa sababu majiko haya yatashuka bei na watu wote watamudu gharama,” alisema.

Pamoja na hilo, alisema Serikali inapaswa kutoa ruzuku kwenye gesi ili kurahisisha kama inavyofanywa katika baadhi ya mataifa.

Mkazi wa Same mkoani Kilimanjaro, Stella Mramba amesema mkakati huo umekuja wakati mwafaka kwa kuwa wananchi wanahitaji matumizi ya kuni lakini hazipatikani kutokana na uchache wa misitu na ongezeko la watu.

"Tunaishukuru Serikali tunapata shida sana na matumizi ya kuni ambazo hivi sasa kuzipata ni nadra katika eneo tunaloishi,lakini wakati huohuo tunaambiwa tulinde mazingira.Sasa uamuzi huu tunaona mabadiliko makubwa katika safari ya wananchi kutumia nishati safi ya kupikia," amesema.


Marufuku ya kuni, mkaa

Mkuu huyo wa nchi, amemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Dk Seleman Jafo kutangaza marufuku kwa taasisi za umma na binafsi zinazohudumia watu zaidi ya 100, kutumia kuni na mkaa kupikia.

Rais Samia alimtaka waziri huyo kuhakikisha katazo hilo linaanza Agosti mwaka huu, akilenga kile alichoeleza, kuzishinikiza taasisi hizo zihamie kwenye matumizi ya nishati safi.

Hata hivyo, marufuku ya Rais Samia inakuja katika kipindi ambacho kati ya magereza 126 zilizopo nchini, 76 zinatumia nishatisafi ya kupikia.

Sambamba na magereza, kati ya vyuo vya elimu 35 vilivyopo 30 zinatumia nishati safi kwa ajili ya kupikia.

Kutokana na hatua iliyofikiwa na taasisi hizo, Rais Samia amesema: “(Dk Jafo) andaa katazo taasisi zote zinazohudumia watu zaidi ya 100 ni marufuku kutumia kuni na mkaa, ukipiga katazo wataingia.”

Ili kutekeleza mkakati huo, ametaka wadau wote muhimu wafikishiwe kwa njia rasmi, uwekwe kwenye tovuti ya wizara ya nishati na utafsiriwe kwa lugha ya Kiswahili na Kiingereza.


Mfuko wa nishati safi

Rais Samia ametaka kutungwa sheria itakayounda mfuko wa kuendeleza nishati safi ya kupikia kufikia mwaka 2025, akisisitiza Serikali itatafuta namna ya kuujazia.

Katika kuujaza mfuko huo, aliahidi kuendelea kutumia majukwaa mbalimbali ya kimataifa ili kuzishawishi nchi zilizoendelea zitekeleze ahadi ya kutoa fedha kwa nchi zinazoendelea kwa ajili ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Ameeleza fedha hizo zitakazotolewa, pamoja na mambo mengine zitatumika katika utekelezaji wa mkakati huo.

Katika hotuba yake hiyo, ametaka wakuu wa mikoa waongezewe kipengele cha matumizi ya nishati safi kama mmoja ya vigezo vya kupima utendaji wao.

Lakini aliwataka wakuu wa mikoa kuwafikia wadau na kuwatambua ili wafikishe nishati hizo katika maeneo ambayo bado hayajafikiwa.

Kwa mujibu wa Rais Samia, kuna haja ya nishati safi kuingizwa katika dira ya maendeleo ya taifa ya mwaka 2050, huku Wakala wa Nishati Vijijini (Rea) ikitakiwa kujipanga ili kutekeleza majukumu yake yaliyopo katika mkakati huo.

Katika hotuba yake hiyo, alimpongeza January Makamba, akisema alipokuwa Waziri wa Nishati ndiye aliyekuja na ajenda hiyo kwa kasi.

Kwa mujibu wa Rais Samia hekta 469,000 za misitu zinakatwa kila mwaka na nishati za kuni na mkaa ni moja ya chanzo kikuu cha hayo.

Kwa kadri misitu inavyopotea, amesema utafika wakati hata upatikanaji wa nishati ya kuni na mkaa utakuwa mgumu na hivyo kuwafanya wananchi watumie muda mwingi kutafuta nishati kuliko chakula.

“Yaani kutafuta chakula ni rahisi kuliko kwenda kutafuta chakula chenyewe,” amesema.

Katika utekelezaji wa nishati safi ya kupikia, ametaka sekta binafsi ije na mbinu kuleta teknolojia rahisi ya matumizi ya nishati akitolea mfano wa kulipia kwa kadri utakavyotumia.


Alichokisema Majaliwa

Awali, akizungumzia mkakati huo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema kazi ya maandalizi yake ilitekelezwa na kamati ya kitaifa inayojumuisha wizara, idara, wakala na wataalamu kutoka taasisi za elimu, washirika wa maendeleo, asasi za kiraia na sekta binafsi.

Amesema uundaji wa kamati hiyo ulizingatia kuhakikisha ushiriki wa wadau wote muhimu katika utayarishaji wake wanashirikishwa.

Kwa mujibu wa Majaliwa, kamati hiyo pia inajumuisha pande mbili za muungano yaani Bara na Zanzibar.

Majaliwa amesema mkakati huo umezingatia masuala ya kisera, miongozo na kanuni zinazosimamia utendaji yatakayosaidia kupunguza matumizi ya nishati ya kuni na mkaa.

Mambo mengine amesema ni kuondoa vikwazo vya uendelezaji nishati safi ya kupikia na uratibu wa namna bora ya kushirikisha wadau katika mnyororo wa thamani wa nishati safi ya kupikia.

Ameeleza mkakati huo dhima yake ni kuhakikisha upatikanaji wa nishati safi na nafuu

Amesema wanaoanisha sera, sheria, kanuni na miongozo ili iwe wezeshi kwa wote wanaoanza kutoa huduma ya nishati safi ili iwe rahisi kwa kila mmoja kuipata.

Dira yake ni kila Mtanzania atumie nishati safi ya kupikia ili kulinda afya zao.

Kwa mujibu wa Majaliwa, mkakati huo utagharimu Sh4.6 trilioni na kwamba utekelezwaji wake utahusisha wadau wote.

Kwa upande wa, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema atahakikisha mkakati unaozinduliwa hauishii kuonekana kwa kupigwa picha, badala yake unazaa matunda tarajiwa.