Sheria za makosa ya unyanyasaji wa kijinsia kupitiwa

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni leo Alhamisi, Aprili 18, 2024.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema ipo haja ya kuzipitia sheria ili kuhakikisha jamii inakuwa salama

Dodoma. Serikali ya Tanzania imesema itafanya mapitio ya sheria na kanuni zinazohusiana adhabu dhidi ya makosa ya unyanyasaji wa kijinsia, lengo likiwa ni kukomesha vitendo hivyo nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa leo Alhamisi Aprili 18, 2024 wakati akijibu swali la papo kwa hapo la Mbunge wa viti maalumu, Tunza Malapo.

Malapo amesema matukio ya unyanyasaji wa kijinsia kwa watoto, wanawake na makundi mengine yamekithiri sana.

“Watu wanafanya na adhabu zinatolewa lakini matukio hayo yamekuwa yakiendelea. Na sasa hivi hali imekuwa mbaya, watu wanalawiti hadi wanyama,” amesema Malapo.

Amehoji iwapo Serikali haioni kuwa ni wakati muafaka wa kupeleka muswada bungeni ili kuongeza adhabu ama kubadili adhabu.

Malapo ametaka adhabu zitakazotolewa zikidhi haja na kukomesha matukio hayo yanayowaathiri watu mbalimbali wakiwamo watoto na wanawake.

Akijibu swali hilo, Majaliwa amesema matukio ya unyanyasaji wa kijinsia yapo nchini na Serikali imekuwa ikichukua hatua kali kwa wale wanaokutwa wakitenda matukio hayo.

Hata hivyo, amesema jamii inatakiwa kuwa mstari wa mbele kukemea na kuchukua hatua kwa kuwafikisha katika vyombo vya sheria wale wanaobainika kufanya matukio hayo.

Amesema matukio hayo yamekuwa yakitokana na sababu mbalimbali ikiwamo ulevi wa vilevi holela vinavyopunguza uwezo wa mtu kufikiri na kutafakari matendo pamoja na malezi ya watoto katika ngazi ya jamii na namna wazazi wanavyowajibika katika kuwalea watoto.

Ametaja sababu nyingine ni imani katika jamii, wapo wanaoamini wakitenda jambo fulani la unyanyasaji wa kijinsia wanapata mafao na utajiri.

“Haya yanasukuma watu kufanya ukatili wa kijinsia lakini pia kuna mila kandamizi za baadhi ya makabila. Haya machache niliyoyataja yanachangia sana katika matukio ya unyanyasaji wa kijinsia,”amesema Majaliwa.

Amesema yanawezekana matukio hayo yanajirudia kwa sababu baadhi ya maeneo sheria zake bado si kali sana.

Majaliwa amesema jambo hilo ni mtambuka na linagusa wizara nyingi, hivyo kila wizara inaweka sheria zake katika kujikinga jambo hilo.

“Napokea ushauri wa kufanya mapitio kwenye sheria hizi, malengo yetu ni kuhakikisha jamii inabaki kuwa salama na wale wote wanaotenda matendo haya ya unyanyasaji wa kijinsia wanachukuliwa hatua kali zaidi. Tunatamani kuona kuwa jambo hili likikoma katika jamii yetu,”amesema Majaliwa.

Amesema Serikali itaendelea kufanya mapitio ya sheria zinazohusu suala hilo na pale kutapohitaji mabadiliko ya sheria na kanuni watapeleka bungeni kwa ajili ya kufanya marekebisho zaidi.

Majaliwa ameiasa jamii kuzingatia mila, desturi na tamaduni ili wasiingie katika matendo ya unyanyasaji wa kijinsia kwa sababu kila mmoja anahaki ya kuishi.

Pia, ameiasa jamii kupunguza ulevi holela unaoweza kuwasababishia kutenda vitendo hivyo.

Katika ripoti ya Mthibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/22, inaonyesha katika kipindi cha miaka mitano matukio hayo yaliongezeka kwa asilimia 80 huku Mkoa wa Dar es Salaam ukiwa kinara.

Katika ripoti hiyo ya ufanisi katika usimamizi wa hatua za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini, inaonyesha kuwa mwaka 2022 Dar es Salaam yaliripotiwa matukio 1,656 kutoka matukio 326 ya mwaka 2018.