Wananchi watakiwa kuchangamkia uchaguzi wa Serikali za mitaa

Muktasari:

Mkuu wa Wilayani ya Siha mkoani Kilimanjaro, Christopher Timbuka amewataka wananchi wale wanaotaka kuboresha au kuhuisha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura wajitokeze katika uboreshaji utakapoanza

Siha. Mkuu wa Wilaya ya Siha mkoani Kilimanjaro, Christopher Timbuka amewataka wananchi kushiriki kikamilifu kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika mwaka huu.

Pia, amewataka wananchi wale wanaotaka kuboresha au kuhuisha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapigakura wajitokeze katika uboreshaji utakapoanza.

Akizungumza na viongozi wa dini na watumishi wa halmshauri hiyo na wananchi wengine wakati wa maombi maalumu kwa Taifa yaliyofanyika katika Soko la Sanya Juu, Timbuka amewataka wananchi  kujitokeza kugombea uongozi katika uchaguzi huo.

"Mwaka huu kuna uchaguzi wa Serikali za mitaa ombi langu kwenu wenye sifa, mjitokeze kugombea nafasi hizi na wananchi mchague kiongozi wenye sifa ya kuwa kiongozi ambaye munaona wenyewe atawaletea maendeleao," amesema Timbuka.

“Tujitokeze kuhuisha taarifa zetu katika Daftari la Kudumu la Wapigakura ili kuwa na sifa kushiriki kwenye uchaguzi huo wa Serikali za mitaa unaokuja na baadaye uchaguzi Mkuu wa mwakani 2025,” amesema.

Aidha, amesema Serikali imerejesha mikopo ya asilimia 10 kwa vijana wanawake na watu wenye ulemavu ya mapato ya halmshauri, hivyo wananachi wachangamkie.

“Halmshauri hii ni miongoni mwa halmshauri 10 zilizowekwa kwenye mpango wa majaribio ya utoaji mpya wa mikopo.

“Wananchi tuchangamkie fursa hii, vikundi viwe na wanachama hai ifikopo Julai mwaka huu, wawe na sifa ya kupata mikopa, hivyo ni vizuri mkafanya maandalizi mapema,” amesema.

Pia, amewataka wananchi kipindi hiki cha mvua za masika kuchukua tahadhari ya magonjwa ya mlipuko kutoka kwenye maji ya mvua ambayo huchanganyika na uchafu.

Diwani wa Sanya Juu, Juma Jani akizungumzia miaka 60 ya maadhimisho ya Muugano kati ya Tanganyika na Zanzibar amesema unatakiwa kulindwa kwa gharama zozote.

“Zipo changamoto lakini hata kwenye familia changamoto zipo na maeneo mengi duniani, hivyo lazima tukabiliane nazo kuhakikisaha tunadumisha muungano,” amesema.

Ofisa Maendeleo wa wilaya hiyo, Mark Masue amesema katika maadhimisho ya miaka 60 ya Muungano, wamefanya usafi Soko la Sanya juu, kupanda miti katika Shule ya Sekondari Ormelili.