Warioba ataja sababu ya wapigakura wachache

Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba.

Muktasari:

  • Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba amesema hali ya idadi ndogo ya wapiga kura wanaojitokeza kwenye uchaguzi inatokana na wananchi kupelekewa wagombea ambao wanajua kuwa si viongozi wanaowahitaji.

Dodoma. Waziri Mkuu mstaafu Jaji Joseph Warioba ametaja mambo ambayo yakifanyiwa kazi mapema yatawezesha wananchi wengi kushiriki uchaguzi na kuwapata viongozi wanaowataka kuwawakilisha kwenye vyombo vya maamuzi.

Jaji Warioba ametoa kauli hiyo leo Jumanne Aprili 30, 2024 kwenye kongamano la wadau wa habari na uchaguzi Tanzania lililoandaliwa na baraza la habari nchini (MCT) Jijini Dodoma.

Jaji Warioba amesema yapo mambo mengi yanayochangia wananchi kususia uchaguzi hivyo idadi ndogo kujitokeza kupiga kura ikiwemo nafasi za uteuzi ndani ya vyama ambayo huteua watu ambao wananchi wanawafahamu kuwa si viongozi.

"Zamani mkutano mkuu wa wilaya ulikuwa unahusika kwenye uteuzi wa mgombea wao lakini rushwa ikaingia wakaamua kushusha, hadi ngazi ya kata  ambako ndipo wananchi walipo napo hapakufaa wakaruhusu wanachama wote kwenye jimbo wapewe nafasi ya kuteua kwa kudhani kuwa hawataweza kuwahonga lakini pia huko nako rushwa imeingia," amesema Jaji Warioba.

Amesema wananchi wasipopatiwa mgombea ambaye wanamjua wao kuwa ni kiongozi anayewafaa huwa wana njia zao za kutumia ikiwamo kutoshiriki uchaguzi na ndiyo maana miaka ya hivi karibuni pameshuhudiwa idadi ndogo ya wapigakura kwa sababu viongozi waliopelekewa hawana sifa za kuwa kiongozi.

Amesema katika dunia ya sasa ambayo viongozi hawawaangalii wananchi wa ngazi ya chini katika kufanya maamuzi ndiyo unasababisha wananchi kuishi kwa kufuata utaratibu wao wenyewe ikiwemo ya kususia uchaguzi.

"Nilikuwa nafuatilia uchaguzi mdogo wa madiwani kuna kata moja nahisi iko Mara, waliojiandikisha kupigakura walikuwa ni 6,000  lakini waliojitokeza kupiga kura na kuchagua kiongozi walikuwa ni 1,000  tu sasa hii ni hatari kwa sababu wananchi wameshachoka," amesema Warioba

Amesema hata mchakato mzima wa kuwaandaa wapiga kura usipokaa vizuri kuanzia uandikishwaji wa wapiga kura kwenye daftari la kudumu, mpangilio wa vituo vya kupigiakura, idadi ya wapiga kura kwenye kila kituo, upigaji wa kura na uhesabuji wa kura ni chanzo cha wananchi kususia uchaguzi.

"Unakuta kituo kimoja kina wapiga kura wengi, halafu karatasi zinazopelekwa ni chache na wasimamizi wa kituo wanachelewa kuja kufungua hilo peke yake linaweza kusababisha watu wengi wasipige kura aidha kwa kukosa karatasi, kukosa uvumilivu wa kusubiri  mistari mirefu ya kupigia kura au sababu wasimamizi wamechelewa kufungua vituo hivyo wananchi wanaamua kuondoka," amesema.

Amesema vyombo vya habari vina mchango mkubwa wa kuhakikisha suala la uchaguzi linakwenda kwa haki kama vitaanza kufuatilia hatua zote muhimu za uchaguzi huo badala ya kusubiri mambo yaharibike ndipo vianze kuripoti.

"Sijui kama mnafuatilia uboreshaji wa daftari la kudumu la wapigakura unaoendelea nchini au mnasubiri mpaka wananchi waanze kulalamika kuwa hawajaandikishwa ndipo muanze kuandika, sasa unapotuambia huyu amesahauliwa kuandikishwa na wakati zoezi la uandikishaji limeshafungwa inatusaidia nini sisi, mnatakiwa kufuatilia kuanzia sasa," amesema Warioba.

Mwandishi mkongwe nchini Jenerali Ulimwengu amevitaka vyombo vya habari na wanasiasa kuacha udalali wa uchaguzi kwani hauna afya kwa Taifa.

Amesema wakati wa uchaguzi kama vyombo vya habari havitasimamia maadili na misingi ya taaluma yao vitanunuliwa na wanasiasa na mwisho wa siku vitasababisha machafuko.

Mwandishi mkongwe Edda Sanga ametaka elimu itolewe kwa wanahabari jinsi ya kuripoti uchaguzi mkuu badala ya kutumiwa na wanasiasa ambao mwisho wa siku wataharibu tasnia yote kwa jumla.

Aliyekuwa kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe amesema vyombo vya habari vinachangia kwa kiasi kikubwa kushinda au kushindwa kwa vyama vya siasa kwenye chaguzi zinazoendelea nchini.

Amesema kwa utafiti alioufanya kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 ulionyesha magazeti yanayomilikiwa na Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd (MCL)yalitoa nafasi sawa kwa vyama vyote vya siasa nchini.

Amesema gazeti la Mwananchi liliripoti matukio ya vyama vya upinzani kwa asilimia 27 na chama tawala kwa asilimia 27 huku kwenye uchaguzi wa mwaka 2010 ilituma waandishi wa habari kwenye vituo vyote vya uchaguzi nchini nakupata matokeo ambayo yalikaribiana na yale yaliyotangazwa na tume ya Taifa ya uchaguzi.

"Kwa hiyo vyombo vya habari vina mchango mkubwa kwa vyama vya siasa katika uchaguzi japo wamejikita zaidi kuripoti matukio badala ya kutoa elimu kwa wananchi," amesema Zitto.