'Wengi wana ugonjwa wa akili bila kujitambua'

Muktasari:

  • Imeelezwa kuwa, sehemu ya kazi inaweza kuwa chanzo cha matatizo ya akili kwa mfanyakazi kutokana na mwingiliano wa majukumu, huku wengine wakitajwa kupata tatizo hilo bila wao kujitambua.

Dar es Salaam. Imeelezwa kuwa, sehemu ya kazi inaweza kuwa chanzo cha matatizo ya akili kwa mfanyakazi kutokana na mwingiliano wa majukumu, huku wengine wakitajwa kupata tatizo hilo bila wao kujitambua.

 Hayo yameelezwa na mtaalamu wa saikolojia kutoka kampuni ya bima ya Jubilee (JJ Insurance), Charles Kalungu leo Oktoba 17, 2023 wakati akitoa elimu kwa wafanyakazi wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), jijini hapa.

Amesema viwango vya changamoto za afya ya akili vimeongezeka kwa kiasi kikubwa kutokana na sababu za kiafya, mfadhaiko unaohusiana na kazi pamoja na masuala mengine binafsi.

Kalungu amesema watu wengi ikiwepo wafanyakazi wamekuwa na tatizo la afya ya akili kutokana na mazingira ya kazi waliyopo, kwani wengine hupata hilo tatizo bila wao kujitambua.

"Changamoto ya akili inaletwa na mambo mengi ikiwepo mhusika mwenyewe, watu wanaomzunguka na mazingira aliyopo na hii watu wengi wanakumbana nayo na hawajui namna ya kujitibu," amesema.

Amesema wengi hawajui kama wana tatizo la akili kutokana na kujiona wapo sahihi kwenye mambo wanayoyafanya hadi pale watakapoelezwa na watu wanaowatazama.

Kalungu amesema magonjwa ya afya ya akili yanaweza kuletwa na sababu za ama kibaolojia au kisaikolojia, ambazo zinaweza kuwa hasi ama chanya na kwamba kila mmoja amekuwa akitazama jambo hilo kwa namna yake bila kufahamu chanzo.

"Kuna watu wapo ofisini lakini hawajui kama wana tatizo akili, mtu wa namna hii unaweza kumgunda kwa matendo yake ambayo si ya kawaida anapokuwepo ofisini," amesema Kalungu.

Amesema ili kutibu tatizo la afya ya akili kuna haja ya kuonana na wataalamu wa saikolojia ili kujitambua alipo, anapotakiwa kuwa na kuamua kufanya mabadiliko kwa kutegemea uwezo wake mwenyewe.

Pia, amesema kutoa elimu kuhusu magonjwa ya afya ya akili ni kitu cha muhimu katika kuzuia kujirudia au kupata ugonjwa wa akili juu ya matibabu na msaada anaohitaji mgonjwa ili kuendelea na maisha yake ya kila siku.

Maadhimisho ya siku ya afya ya akili duniani hufanyika kila ifikapo Oktoba 10 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu Tanzania yaliadhimishwa jijini Dodoma.

Awali, Meneja Rasilimali watu na Utawala wa MCL, Paul Hamidu amesema kuna haja ya kuwa na mazungumzo hayo kwa wafanyakazi kila baada ya muda mfupi ili kuimarisha utendaji kazi na afya zao za akili.