Wenye kifafa, wanaouguza waeleza madhila wanayopitia

Mweyekiti wa Uwakita, Dk Saidi Kuganda akizungumza  leo Mei 9, 2024 kwenye kikao cha Jumuiya hiyo kilichofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Muktasari:

  • Jamii yaaswa kuacha unyanyapaa, kuwatenga wenye kifafa

Dar es Salaam. Yapo maradhi yenye kuleta changamoto si tu kimwili kwa mgonjwa bali hata kijamii, ikiwemo kutengwa, kunyanyapaliwa na kukosa haki za msingi, ikiwemo elimu.

Ugonjwa wa kifafa ni miongoni mwa hayo, baadhi ya wagonjwa wameeleza kupitia  changamoto, ikiwemo kutengwa na watu wao wa karibu, wakiwamo ndugu.

Maradhi hayo yanasababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa umeme wa ubongo kutokana na sababu kama vile ajali, minyoo inayopatikana kwenye nyama isiyoiva vizuri, kiharusi, na malaria kali.

Monica Mjwahuzi, mzazi wa mtoto anayeugua kifafa akizungumza na Mwananchi Digital leo Mei 9, 2024 amesema ni changamoto kubwa kumuuguza mtu wa namna hiyo kwani baadhi ya watu humuogopa anapoanguka.

"Mwanangu alipata kifafa akiwa na umri wa miezi saba, alipofika darasa la tatu ikabidi aache shule kutokana. Sasa ana miaka 22 hana elimu na jamii inamtenga," amesema.

Amesema awali alimtibu kwa dawa za miti shamba lakini baadaye mambo yalibadilika.

Monica amesema hata familia ilimtenga yeye na mwanaye, ambaye alinyimwa hata sahani za kulia chakula.

"Nashauri upendo kwa watu hawa kwani ni watu kama wengine na wana haki ya kuishi, tuwapende na tusiwanyanyapae," amesema.

Fides Uiso, mzazi mwenye mtoto wa miaka minane anayeugua maradhi hayo amesema, "Mwanangu ana kifafa kwa siku dawa zinatumika za Sh10,000, hadi uchumi unashuka."

Amesema amejitahidi kuwaelimisha majirani na ndugu kuhusu hali hiyo ili wasinyanyapae.

Fides amesema changamoto kubwa zaidi ukigundulika kuwa na ugonjwa huo ukiwa umeolewa basi kinachofuata ni kuachika.

Mary Kipingili, mgonjwa wa kifafa amesema kuna changamoto ya kutelekezwa na watu wa karibu pindi mgonjwa akianguka.

"Shuleni ikitokea umeanguka basi marafiki wanatimua mbio, pia kingine nataka elimu iwafikie wanafunzi, walimu na hata watu wote waelewe juu ya maradhi haya," amesema.

Wameeleza hayo leo Mei 9, 2024 walipohudhuria kikao cha jumuiya ya wazazi na watu wanaoishi na hali ya kifafa (Uwakita) kilichofanyika katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.

Lengo la kikao hicho ni kuanzisha kampeni ya kuelimisha jamii kuhusu kifafa na kuondoa unyanyapaa kwa watu wanaoishi na hali hiyo.

Takwimu nchini zinaeleza wapo zaidi ya milioni moja wanaoishi na kifafa.

Mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Dk Saidi Kuganda amesema jamii inapaswa kutambua mwenye hali ya kifafa ana haki za kuishi kama watu wengine.

Amesema mtu mwenye kifafa anapaswa kuwahishwa kwenye matibabu, akiwataka wazazi wanaowafungia watoto ndani wakiogopa kutengwa shuleni waache kwa kuwa wana uwezo wa kusoma.

Dk Kuganda ambaye ni bingwa katika maradhi hayo amesema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kuna watu milioni 50 wanasumbuliwa na kifafa, Afrika wakiwapo milioni 10.

"Watu milioni sita hubainika kila mwaka lakini kwa bahati mbaya uelewa wa jamii juu ya hali hii bado ni mdogo, hivyo kumekuwapo vitendo vya unyanyapaa na kubaguliwa na watu wa karibu,” amesema.

"Hali hii huleta msongo wa mawazo kwa watu hawa na inakadiriwa takribani watu watano kati ya 10 wanaoishi na hali hii wanapata maradhi ya wasiwasi au sonona, wapo kwenye hatari ya kufariki mapema mara tatu zaidi ya wasiougua kifafa," amesema.

Amesema Uwakita wanaungana na Serikali, taasisi zote za kijamii na za kitaaluma katika jitihada na kampeni ya kuelimisha jamii kupata ufahamu sahihi juu ya kifafa.

"Kampeni hii yenye kauli mbiu ‘Elimika juu ya kifafa, tokomeza unyanyapaa, pata tiba sahihi’ itatusaidia kutokomeza unyanyapaa ili kupata tiba sahihi kwa watu waishio na ugonjwa huo," amesema.