80 waokolewa, wawili wafariki kwa mafuriko yaliyoambatana na kimbunga Hidaya

Daraja la Matandu likiwa limesombwa na maji na kukatisha  mawasiliano ya ya barabara kati ya mikoa ya kusini na Pwani. Picha  na Bahati Mwatesa

Muktasari:

  • Mbali na vifo hivyo, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limesema limefanikiwa kuwaokoa watu 80 ambapo 49 walikutwa mashambani na 31 walikutwa katika kituo cha gesi asilia cha Somanga.

Lindi. Kufuatia kuwepo kwa athari za mvua zitokanazo na kimbunga Hidaya, watu wawili wamefariki dunia.

Mmoja kati ya waliofariki dunia alikutwa na mauti  wakati akijaribu kuokoa pikipiki yake isisombwe na maji.

Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Lindi, Joseph Mwasabeja amethibitisha kutoa kwa matukio hayo.

Amefafanua kuwa watu wawili walifariki  dunia huku mmoja kati yao alikutwa na mauti baada ya kuzidiwa na maji alipokuwa akiokoa pikipiki yake isisombwe.

Amesema wamewaokoa watu 80 ambapo 49 walikutwa mashambani na 31 walikutwa katika kituo cha gesi asilia cha Somanga.

 “Unajua eneo hili la Matandu jana lilikuwa linapitika bila shida lakini leo zaidi ya mita 80 zimeliwa na maji zimekatika ambapo kwa Somanga imekatika mara mbili yaani hapo tayari ni shida,” amesema.

Amesema kwa sasa wanazungumza na wenye mabasi ili kuhakikisha wanawarudisha abiria walipowatoa kwa kuwa hakuna uwezekano wa kuendelea na safari, na pia tunawaasa wananchi kufuatilia taarifa za Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA).

Kamanda huyo amesema kama wangezingatia maagizo ya awali wangeweza kusaidia kupunguza madhara ya kimbunga Hidaya ambayo yalitolewa mapema, amesisitiza kwamba taarifa hizi ni za kweli.

Amesema jeshi hilo lilianza uokoaji saa 4 asubuhi baada ya Shule ya Sekondari Kilwa kuzingirwa na maji, hivyo kulazimika kufanya uokoaji kwa wanafunzi.

Hata hivyo, amesema walishindwa kuokoa basi la King Yasin linalofanya safari zake Mtwara - Dar es Salaam lilikuwepo ambapo walishindwa kuliokoa kutokana na wingi wa maji.

“Tulienda eneo la Masaninga ili kwenda kuokoa gari ya King Yasin lakini kutokana na wingi wa maji tulishindwa kuliokoa tuliendelea kukagua maeneo mengine ambapo Kilwa masoko tulikuta maji yamejaa eneo limekuwa kama beseni,” amesema Mwasabeja. 

Naye Mwenyekiti wa kitongoji cha Okote kilichopo Kilwa Kivinje, Abdalla Mboya amesema saa 6 usiku, taarifa ilitolewa juu ya maji kuzingira makazi ya watu ambapo jitihada zilifanyika ili   kuwaokoa.

“Nikiwa nimelala, saa 6 usiku, nilipokea taarifa kuwa hapa Kitandu darajani kuwa wakulima wakiwa mashambani wamezingirwa na maji ambapo tulifanya mawasiliano lakini hatukufanikiwa hadi saa 11 alfajiri, ndio tukaenda kuwaokoa ambapo tumeokoa watu 50 na bado ambao hatujapata taarifa zao.

“Kuna kitongoji kinaitwa Mkenda, kuna watu 10 wako juu ya miti wanasubiri uokozi ambapo tunawafuatilia lakini tulipata taarifa ya kifo cha mtu mmoja ambaye alikwenda kuokoa pikipiki yake na akashindwa, amepoteza maisha,” amesema.

Kwa upande wake, Salum Mohamed, mkazi wa Matandu amesema maji yamezingira makazi yao na hakuna pa kutokea ndiyo maana boti zinapita kuangalia usalama wao.

“Unajua kule mbele kuna karavati limekatika na hata ukimaliza daraja hili, mbele maji yalikuwa yanapita juu ya barabara, hali si nzuri baada ya maji kuanza kujaa, saa 7  usiku tulianza kuamshana lakini hatukuweza kwenda popote kwa kuwa tayari tulikuwa tumezingirwa na maji.

“Kwa eneo hili la Matandu, hakuna asiyejua kuwa linajaa maji hasa wanaoishi mabondeni na haya maji ni mara ya pili, lakini sasa yameongezeka kwa kiasi kikubwa  kuna maeneo hayakupata maji, watu walirudi licha ya tahadhari waliyopewa juu ya kimbunga Hidaya,” amesema Mohamed.