Abiria wavutiwa ‘ruti’ mpya ATCL kwenda Dubai

Muktasari:

  • Waeleza manufaa watakayopata baada ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) kupitia ndege mpya ya Boeing B737 Max 9 kuzindua safari mpya za kwenda moja kwa moja Dubai.

Dar es Salaam. Abiria wa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), wamesema kupungua gharama na kutumia muda mfupi ni moja ya manufaa watakayopata, baada ya kuzinduliwa safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Dubai.

ATCL imezindua leo Jumapili Machi 31, 2024 safari hizo mpya zitakazofanyika mara nne kwa wiki---Jumapili, Jumatatu, Jumatano na Ijumaa.

Wakizungumza wakati wa uzinduzi, abiria wameeleza walikuwa wakipata changamoto ya kufika Dubai.

"Nafurahi kwa sababu ni mara yangu ya kwanza kwenda na ndege hii moja kwa moja hadi Dubai. Gharama tunalipa Dola 399 za Marekani (takribani Sh1 milioni)," amesema Bizoza Pacifique, raia wa Burundi.

Amesema awali ili ufike Dubai ilimlazimu mtu kuunganisha safari na gharama ilikuwa kati ya Dola 700 na 800 (Sh1.8 milioni hadi Sh2 milioni).

"Mimi ni raia wa Burundi, nimetoka Burundi kuja kupanda ndege Dar es Salaam baada ya kuona gharama ni nzuri na unapata usafiri wa moja kwa moja," amesema Pacifique.

Mtendaji Mkuu wa  (ATCL), Ladislaus Matindi (kushoto) akizungumza na mmoja wa abiria.

Abiria mwingine, Ridhiwani Othaman amesema: "Nafanya biashara mtandaoni, nimekuwa nikisafiri mara kwa mara kwenda mataifa mbalimbali na nimewahi kufika Dubai, lakini furaha yangu ni kuona Air Tanzania inatupeleka moja kwa moja hadi Dubai."

Amesema faida ya kuwa na safari ya moja kwa moja kutoka Tanzania hadi Dubai ni kutumia muda mfupi unaokadiriwa kuwa saa tano.

"Hatuna wasiwasi wa kupoteza muda tena, naishi Dar es Salaam hata nikiwa na safari najua muda, hata shughuli ninazofanya zinakuwa katika ratiba," amesema.

Akizungumzia safari hizo Mtendaji Mkuu wa ATCL, Ladislaus Matindi amesema ni jitihada za kuendelea kupanua mtandao wa safari.

"Leo tunafuraha kama Air Tanzania na abiria wetu tunaongeza kituo kipya katika mtandao wetu wa safari za kwenda hadi Dubai, kwani ni sehemu muhimu katika mahusiano ya kibiashara kati ya nchi yetu na Falme za Kiarabu.

Amesema wanaanza safari leo na ndege mpya ya Boeing B 737 Max 9 iliyopokewa nchini Machi 26, 2024.

“Tutafanya safari nne siku ya Jumapili, ya pili Jumatatu, ya tatu Jumatano na ya nne Ijumaa. Tumezipanga kwa aina ya pekee," amesema Matindi.

Amesema wamepanga safari hizo kwa kuzingatia mahitaji, ili abiria wafurahie huduma na kuona soko lao linaendelea kukuua vizuri.

"Tumeweka ndege mpya kabisa itakayotoa ushindani na kuwa na huduma nzuri si kwa safari tu, bali hata huduma kwa abiria," amesema Matindi.

Kuhusu mizigo, Matindi amesema: "Daraja la biashara mizigo mitatu itaruhusiwa ya kilo 30 kila mzigo na tunawakaribisha kuungana nasi katika njia mpya kwenda Dubai."