Ahukumiwa kunyongwa kwa kuua watu saba

Muktasari:

  • Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma imemuhukumu mkazi wa Mlole, Manispaa ya Kigoma Ujiji, Peter Moris (34), kunyongwa hadi kufa baada ya  kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya watu saba wa familia moja.

Kigoma. Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma imemuhukumu Peter Moris (34), mkazi wa Mlole, Manispaa ya Kigoma Ujiji, kunyongwa hadi kufa baada ya kumtia hatiani kwa kosa la mauaji ya watu saba wa familia moja.

Akisoma hukumu hiyo leo, Februari mosi, 2024 Jaji Agustino Rwizile amesema mshitakiwa huyo alitekeleza mauaji hayo Julai 3, 2022, katika kijiji cha Kiganza, wilayani Kigoma, mkoani Kigoma na kuwaua watu saba  kwa kuwakata  na panga.

Jaji Rwizile amesema mshitakiwa huyo alilwenda nyumbani kwa marehemu Januari Mussa (35), ambaye ni rafiki yake  wakaongea na kupata chakula cha jioni pamoja na mshtakiwa alilala nyumbani hapo.

Amesema mshitakiwa alilala chumba kimoja na ndugu wa Januari aliyejulikana kwa jina la James Joel na ilipofika saa sita usiku aliamka na kwenda chumbani kwa rafiki yake Januari na kumkata mapanga na kumuua.

Jaji amesema baada ya kumkata mapanga rafiki yake alimkata na mke wa rafiki yake, Sara Dunia na kumuua na baadaye wakati anatoka akakutana na mama mzazi wa Januari akitokea chumbani kwake naye akamkata  mapanga na kumuua.

Amesema baada ya hapo mshitakiwa alirudi chumba alichokuwa amelala na James  na kumkata mapanga na kumuua, wakati  anaondoka alikutana na watoto wa rafiki yake na kuwakata mapanga na kuwaua.

Waliouawa katika tukio hilo ni Tilifera Toyi (70), Januari Mussa (35), Joel Mussa (40), Sara Dunia (28) ambaye ni mke wa Januari, Christina Lazaro(9), James Joel (7) na James Januari (4) aliyefariki akiwa njiani kuelekea Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu zaidi.

Jaji amesema maelezo hayo ni kwa mujibu wa maungamo ya mshitakiwa wakati amekamatwa baada ya kutokea kwa tukio hilo, Mahakama imetoa hukumu hiyo kwa kuzingatia maelezo hayo, mashahidi 21 waliotoa ushahidi wao mahakamani hapo pamoja na sampuli za vinasaba vya damu zilizokutwa katika nguo za mshitakiwa.

 “Mahakama imejiridhisha pasipo na shaka, vielelezo na ushahidi uliotolewa pamoja na simu aliyokutwa nayo mshitakiwa baada ya kukamatwa kuwa ni mali ya mmoja wa marehemu, ambayo aliondoka nayo baada ya kutekeleza mauaji.

“Hivyo inafanya Mahakama ijiridhishe kuwa mshitakiwa alitenda kosa la mauaji ya watu saba,” amesema Jaji Rwizile.

Amesema mshitakiwa alifanya kosa kinyume cha kifungu cha sheria namba 196 na 197 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022 na kwamba, mshitakiwa ana haki ya kukata rufaa.

Kesi hiyo namba 46 ya 2022, ilikuwa na jopo la mawakili kutoka upande wa Jamhuri uliongozwa na Enosisye Erasto na wengine ni Edina Makala, Fortunatus Maricha, Flora Lucas huku kwa upande wa wakili wa utetezi uliwakilishwa na wakili Sadiki Akil.