Aina za futari unazoweza kuandaa kwa dakika 30
Dar es Salaam. Katika kipindi hiki cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kuna changamoto ya muda kwa wafanyakazi hususani wanawake.
Changamoto ya muda inatokana na kuwapo kwa muda maalumu wa kufuturu (kula) na chakula maalumu (futari).
Kutokana na changamoto hiyo leo ninakuletea futari mbili ambazo unaweza kuziandaa kwa muda mfupi.
Futari hizo ni pamoja na ndizi mbivu na viazi mbatata.
Futari ya ndizi mbivu
Mahitaji
Ndizi mbivu sita
Nazi pakiti moja
Sukari kiasi
Hiliki ya kutosha
Jinsi ya kutayarisha
Menya ndizi kisha toa moyo wa kati kati, zikate kate kulingana na unavyotaka, zipange ndani ya sufuria.
Weka maji kiasi kulingana na wingi na ugumu wa ndizi, zichemke kidogo zikikaribia kuiva na kabla maji hayajakauka kabisa weka tui la nazi, mimina hiliki na sukari ziache zichemke hadi tui libaki kidogo, zitakuwa tayari kwa kuliwa.
Futari ya viazi mbatata
Mahitaji
Viazi mbatata kulingana na ukubwa wa familia ua watakaokula.
Nyanya
Vitunguu
Pili pili hoho
Karoti
Mafuta ya kupikia
Maji safi
Chumvi
Pili pili mtama
Maandalizi
Menya viazi, unaweza kuvikata au kuviacha vizima kulingana na unavyopenda.
Vioshe vizuri kwa maji safi.
Tayarisha nyanya, vitunguu, hoho na karoti
Bandika sufuria ya kupikia jikoni, weka mafuta ya uto, yakichemka weka vitunguu maji, vikiiva kiasi weka vitunguu saumu, kisha acha viive hadi viwe na rangi ya hudhurungi (brown).
Weka viazi mbatata kwenye mchanganyiko wa vitunguu koroga kwa muda na uviache kwa muda wa dakika 10 hadi 15 hadi vikaukie mafuta kisha weka nyanya hakikisha ukiweka nyanya moto uwe wa kutosha ili ziive.
Funika kwa dakika tano, geuza kisha weka hoho na karoti kwa pamoja kisha funika, hapa unaweza kupunguza moto baada ya dakika mbili au tatu geuza na hakikisha vimechanganyika na vimebaki na mchuzi mzito kisha viipue tayari kwa kuliwa.