Ajali ya bajaji, Coaster yaua mama na mtoto

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP,  Abdi Isango akizungumza na waandishi wa habari.

Muktasari:

  •  Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Abdi Isango amesema kwa sasa jeshi hilo linamsaka dereva wa bajaji

Mbeya. Mwanamke mmoja na mtoto wake ambao hawajafahamika majina wamefariki dunia baada ya ajali ya bajaji waliyokuwa wamepanda kugongana na basi aina ya Toyota Coaster Mtaa wa Maghorofani jijini Mbeya.

Ajali hiyo ilitokea jana jioni, Mei 7, 2024  huku bajaji ikiwa imebeba watatu waliokuwa wanatokea hospitali ya mkoa.

Imedaiwa kuwa, dereva wa bajaji hiyo aliyekuwa anajaribu kulipita lori bila tahadhari, aligongana na coaster hiyo.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, SACP Abdi Isango amesema kwa sasa jeshi hilo linamsaka dereva huyo.

Amesema katika ajali hiyo pia watu wawili wamejeruhiwa na wamelazwa Hospitali ya Mkoa Mbeya wanaendelea na matibabu.

“Coaster ilikuwa ikielekea Tunduma ilikuwa upande sahihi, yule dereva wa bajaji akawa analipita lori lililokuwa mbele yake bila tahadhari, ndiyo akasababisha ajali hiyo iliyochukua uhai wa mama na mtoto wake na kujeruhi watu wengine wawili,” amesema kamanda huyo.

Hata hivyo, amesema bado marehemu wote hawajafahamika majina yao japo mama anakadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 25 na 30 na mtoto anakadiriwa kuwa na miaka kati ya miwili na mitatu.

“Tunaendelea kumtafuta dereva na chombo chake tunakishikilia,” amesema Kamanda Isango.

Kamanda huyo amesema Jeshi la Polisi litaendelea kuchukua hatua kwa madereva wote wanaokiuka sheria za barabarani ikiwamo kuwasitishia leseni kwa kipindi cha miezi sita.

“Kama ilivyo majukumu ya Jeshi la Polisi, hatutasita kuchukua hatua kwa madereva wanaokiuka sheria,” amesema kamanda huyo.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Halima Daud amesema akiwa katika shughuli zake za kuhudumia chakula, alishuhudia dereva bajaji akijaribu kulipita moja ya gari lililokuwa mbele yake akiwa katika mwendo kasi, ndipo akaivaa Coaster.

"Nadhani kwenye bajaji walikuwa zaidi ya watu wanne kwa kuwa ruti ya hospitali ya mkoa, madereva huwa wanajaza, ila sikwenda kushuhuhudia ni wangapi wamefariki,” amesimulia Halima.

Frank Gasper,  muosha magari katika mtaa huo amesema: "Dereva bajaji hakuangalia wakati analipita gari kubwa lililokuwa mbele yake, ghafla akakutana uso kwa uso na Coaster ikawaswaga wote lakini dereva aliiacha bajaji kushoto kwake akafanikiwa kutoka na kukimbia,” amesema Frank.

Ofisa Habari wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Mbeya, Agrey Mwaijande amesema wamepokea miili ya watu wawili mama na mtoto wake na majeruhi wawili waliotokana na ajali hiyo.

Hata hivyo, amesema majeruhi mmoja tayari ameruhusiwa kutoka hospitali baada ya hali yake kuendelea vizuri na mwingine amehamishiwa Hospitali ya Kanda Mbeya kwa matibabu zaidi.

"Ni kweli ajali hiyo ilitokea na hapa hospitali tulipokea miili ya marehemu wawili," amesema Mwaijande.