Alichosema Rais Samia baada ya kupokea ripoti ya kikosi kazi

Muktasari:

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema amepokea mapendekezo ya kikosi kazi cha kuratibu na kuchakata maoni ya wadau wa demokrasia, akisema Serikali inakwenda kuyafanyia kazi, “lakini mapendekezo yao si amri kwa Serikali.”



Dar es Salaam. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema amepokea mapendekezo ya kikosi kazi cha kuratibu na kuchakata maoni ya wadau wa demokrasia, akisema Serikali inakwenda kuyafanyia kazi, “lakini mapendekezo yao si amri kwa Serikali.”

“Itabidi ndani ya Serikali tujipange vikosi kadhaa, wale watunga sheria, kuangalia mambo ya siasa na Katiba. Inabidi tujipange vikosi kadhaa ndani ya Serikali na pengine tuje tuwaombe tena baadhi yenu kuingia katika vikosi hivyo ili tuyafanyie kazi mlioyaleta.

“Kuna ambayo ni mepesi tunaweza kuyafanyia kazi haraka, lakini kuna yale ambayo lazima tukae na kuangalia sheria zilizopo zina mapungufu wapi? Na tunayabadilisha vipi kutokana na maoni yenu,” amesema Rais Samia.

Rais Samia ameeleza hayo leo Ijumaa, Oktoba 21, 2022 Ikulu jijini Dar es Salaam wakati akipokea mapendekezo ya ripoti ya kikosi cha kuratibu na kuchakata maoni ya wadau wa demokrasia kutoka kwa mwenyekiti Profesa Rwekaza Mukandala.

“Nimesikiliza vizuri uwasilishwaji uliofanywa na Profesa Mukandala na nimesikiliza vifungu vyote alivyovisema.Vingine nilikuwa nasema ilo kweli? Lakini ni maoni ya kikosi kazi,” amesema.

Hata hivyo, Rais Samia amesema sio jambo la kukabidhiwa papo uanze kulifanyia kazi, lakini kikosi kazi kimependekeza mambo mazuri yanayotakiwa kuzingatiwa na kuyafanyia kazi katika utendaji wa Serikali.

Aidha, amesema kikosi kazi hicho kimemaliza kazi yake.