Ashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kumbaka mama yake hadi kumuua

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani

Muktasari:

  • Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonjani amekiri kutokea kwa tukio hilo na kumtaja mtuhumiwa huyo kuwa ni  Mathias Elias.

Katavi. Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi linamshikilia Mathias Elias (30) kwa tuhuma za kumbaka hadi kumuua mama yake mzazi akidhani ni mpenzi wake.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani amebainisha hayo leo Ijumaa Mei 10, 2024 kwenye mkutano wa kusikiliza kero za wananchi uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Uhuru.

Amesema tukio hilo limetokea hivi karibuni ambapo mtuhumiwa alitumia mbinu ya kumuita marehemu mama yake atoke, huku akiambatana na wenzake wakiwa wamelewa na ndipo walipomfanyia kitendo hicho.

“Baada ya mama yake kutoka nje, mtuhumiwa na wenzake wakaanza kumbaka hadi kusababisha kifo chake,” amesema.

Kamanda Ngonyani amesema kufuatia tukio hilo,  wanamshikilia mtuhumiwa ili alisaidie Jeshi la Polisi kuwataja wenzake alioshirikiana nao katika tukio hilo la ubakaji na kusababisha kifo.

Amesema matukio ya ukatili yanafanywa na vijana waliojiingiza  kwenye matumizi ya dawa za kulevya, ulevi wa kupindukia kitendo ambacho kinaumiza wazazi wanaowategemea.

“Mimi Kamanda wa Polisi nimekuja hadharani kuwasikiliza kero zenu hususani zinazohusu usalama katika Mkoa wa Katavi,” amesema.

Amesema kuna vijana wanazurura mitaani, hawataki kufanya kazi, wanajiingiza kwenye vitendo vya kuvuta bangi na matumizi ya vilevi kupindukia, umefika wakati wa wananchi kutoa taarifa ili kuwadhibiti wasilete madhara.

Mkazi wa Manispaa ya Mpanda, Sylivestae Joseph ameshukuru hatua hiyo ya Kamanda wa Polisi kusikiliza kero za wananchi na kuweka mikakati ya kudhibiti ili kupunguza uhalifu.

“Bado hatujui taratibu za Jeshi la Polisi za kufanya kazi, kuna baadhi wanafanya kazi wakiwa wamelewa pombe, jambo linalowafanya wananchi wasiwe na imani na utendaji wao wa kazi,” amesema.

Naye Amina Abdallah amesema kwa sasa matukio ya uhalifu yamepungua kutokana na uwepo wa polisi jamii na ulinzi shirikishi kwenye mitaa yao.

Amesema licha ya kuwepo kwa ulinzi shirikishi, wanaomba Jeshi la Polisi kuwapatia mafunzo ili wasitumie nguvu kubwa na kuleta madhara kwa jamii, pindi wanapobaini waliotenda uhalifu au kuvunja sheria.