ATCL: Hakuna kiongozi anayesafiri bure

Muktasari:

  • Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limesema viongozi wanaotumia ndege zake kwa safari za nje ya nchi, wanazikodi hawapewi bure.

Dar es Salaam. Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limesema hakuna kiongozi wa Serikali aliyewahi kutumia ndege za shirika hilo kwenda ama ndani au nje ya nchi bila kulipia.

Limesema safari zote za viongozi zinazoshuhudiwa wakitumia ndege za shirika hilo, huwa wanazikodi na kulipia gharama kama ilivyo kwa wateja wengine.

Hayo yanaibuka kipindi ambacho, kumekuwepo na ukosoaji wa matumizi ya ndege hizo kwa viongozi wa Serikali na wastaafu.

Malalamiko dhidi ya matumizi hayo, yamekwenda mbali zaidi hadi kuhusishwa na sababu za kuahirishwa na kucheleweshwa kwa safari za ndege za shirika hilo.

“Safari zinaahirishwa ratiba hazieleweki kwa sababu ndege wanapewa viongozi wanaenda nazo nje bure, badala ya kuziacha zifanye biashara,” amesema Denis Don mkazi wa Dar es Salaam.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo, Oktoba 4, 2023 Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Mhandisi Ladislaus Matindi amesema kila inapoonekana ndege ya shirika hilo imetumika na kiongozi kwa safari ama za ndani au nje ya nchi, sio kwamba amepewa bure, bali anaikodi na kulipia gharama.

Kulingana na Mhandisi Matindi, tangu alipoteuliwa kushika nafasi hiyo ndani ya ATCL hakuwahi kutokea kiongozi aliyesafiri kwa ndege hizo bure, wote wanalipia ama kwa kukodi au kama abiria.

“Watu wanafirikiri viongozi wanachukua ndege bure, hajawahi kutokea kiongozi aliyesafiri bure na haitatokea kwa sababu wamenipa shirika ili nizalishe, nipo tayari kuweka rehani nafasi yangu kama kuna kiongozi aliwahi kusafiri bure,” amesema.

Ameusisitiza ufafanuzi huo kwa kile alichoeleza, Ofisi ya Rais ndiye mteja mkubwa wa kukodi ndege hizo, Kadhalika ndiye mlipaji mzuri, ingawa wapo wengine pia.

“Huwa tunatoa muda wa kulipia, ukifika mimi mwenyewe nafunga safari nakwenda namwambia kwamba kuna deni kiasi fulani na linalipwa, haikuwahi kutokea haijalipiwa,” amesema.

Hata hivyo, amesema upo utaratibu iwapo kiongozi atataka kukodi ndege, ikiwemo kutoa taarifa mapema ili kujua ratiba na kwamba imewahi kutokea mara kadhaa wamekosa.

“Mbona imewahi kutokea mara kadhaa viongozi wanataka kukodi ndege tunawaambia kwa wiki hii ratiba imebana na hakuna aliyewahi kubisha au kulazimisha akodishiwe huwa wanaelewa,” amesema.


Kuchelewa, kuahirishwa safari

Kuhusu kuchelewa na kuahirishwa kwa safari za ndege hizo, Mhandisi Matindi amesema zipo sababu za ndani na nje ya uwezo wa shirika hilo, zinazofanya safari kuahirishwa.

Amezitaja sababu zilizo nje ya uwezo wa ATCL ni kama hali ya viwanja, hali ya hewa, uwepo wa ndege maalum zinazopita katika anga na maelekezo ya waongoza ndege.

Kwa upande wa zile zilizopo ndani ya uwezo wa shirika hilo, Matindi amesema ni hitilafu ya ndege, lakini inashindikana kutatuliwa kutokana na kutokuwepo mbadala.

"Inapotokea ndege imeharibika au inahitilafu, lazima muwe na ndege mbadala, lakini uwezo huo bado hatujaupata kwa sasa,” amesema.

Kulingana na uwezo wa sasa, Mhandisi Matindi amesema kinachofanyika ni kusubiri itengenezwe iliyopo na itaruhusiwa kuruka iwapo watajiridhisha na usalama wake.

Lakini, ameeleza kwa kadri Serikali inavyoliongezea uwezo shirika hilo, ndivyo litakavyopunguza changamoto hizo.

“Tunapaswa kuwa na ndege nyingi zaidi ili kudhibiti changamoto kama hizi, tunashukuru Serikali inatuwezesha, hii ni hatua nzuri, imetuongezea ndege, japo haitoshi kumaliza tatizo lakini inavyoendelea kufanya hivyo utafika wakati tutakuwa vema,” amesema.

Amesisitiza, “bado shirika linajengwa, hatuwezi kusema sisi tupo kama wengine walioendelea, lakini Serikali inazidi kutuongezea uwezo.”