Atuhumiwa kuua mfanyakazi kwa moto

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela

Muktasari:

“Banda na ndugu yake aliyejitambulisha kwa jina la Festo Richard juzi walifika katika Kituo cha Polisi Oysterbay ili kutoa taarifa za kujeruhiwa kwa kupigwa na kuchomwa moto na

POLISI Mkoa wa Kinondoni wanamshikilia mwanamke (jina tunalo) kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mlinzi wake aliyejulikana kwa jina la Isaac Banda baada ya kumchoma moto hadi kufa.

Mwanamke huyo, ambaye ni Mtanzania mfanyabiashara anayeishi New York, Marekani anadaiwa kufanya uhalifu huo baada ya kurudi nchini Januari 22 na kugundua upotevu wa mali zake zenye thamani ya Dola za Marekani 50,000 karibu Sh80 milioni za Tanzania katika nyumba yake iliyopo Upanga.

Habari zilizopatikana jana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Charles Kenyela zinasema kuwa awali Banda ambaye anadaiwa kuwa ni raia wa Malawi alifika katika Kituo cha Polisi cha Oysterbay na ndugu yake Festo Richard kutoa habari za kujeruhiwa na mwanamke huyo na akapatiwa fomu ya PF 3 kwa ajili ya matibabu.


“Banda na ndugu yake aliyejitambulisha kwa jina la Festo Richard juzi walifika katika Kituo cha Polisi Oysterbay ili kutoa taarifa za kujeruhiwa kwa kupigwa na kuchomwa moto na jalada la kujeruhi lilifunguliwa.


Majeruhi huyo alikwenda kutibiwa katika Hospitali ya Mwananyamala.
Kenyela alisema baada ya kufikishwa hospitalini hapo hali ya Banda iliendelea kuwa mbaya na kuhamishiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili(MNH), lakini alipoteza maisha muda mfupi baada ya kufika hospitalini hapo.


Kenyela alisema maelezo ya awali yanaeleza kuwa Banda, ambaye alikuwa ameajiriwa kama mtunza nyumba na mlinzi wa nyumba ya mwanamke huyo akiwa kazini kwake Block 41, Kinondoni alishambuliwa na tajiri yake akiwa na watu wengine ambao bado hawajafahamika.


Banda alipigwa huku akiwa amefungwa kamba miguuni na mikononi na kisha kuchomwa moto.


“Saa 11 alfajiri, Januari 22, mlinzi huyo alifanikiwa kujiokoa na kukimbilia nyumbani kwa Festo akiwa na majeraha makubwa ya moto yaliyosababisha kifo chake,”alisema Kenyela.
Alisema hata hivyo haijafahamika mlinzi huyo aliwezaje kufika nyumbani kwa ndugu yake akiwa katika hali hiyo.


Kenyela alisema wakiwa katika upelelezi wa tukio hilo, Februari 2, mtuhumiwa alifika Kituo cha Polisi cha Oysterbay na kutoa taarifa za wizi wa mali zake lakini kabla hajamaliza mchakato huo walipewa taarifa za kifo cha mlinzi huyo kutoka Hospitali ya Muhimbili na yeye kugundulika kuwa ni mhusika hivyo kuwekwa ndani kwa tuhuma hizo.