Auawa kwa kukatwa shingo na mpangaji mwenzake

Mtaa yalipotokea mauaji hayo.

Muktasari:

 Shaban Athuman, mkazi wa Mtaa wa Majengo Mapya, Manispaa ya Moshi, amefariki dunia, baada ya kukatwa na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa ni panga na mpangaji mwenzake.

Moshi. Kijana mmoja, Shaban Athuman amefariki dunia baada ya kukatwa shingo na kitu chenye ncha kali kinachodhaniwa kuwa ni panga na mpangaji mwenzake, huku chanzo cha tukio hilo kikidaiwa kuwa ni ugomvi wa simu.

Tukio hilo limetokea leo, April 24, 2024 katika Mtaa wa Majengo Mapya, Manispaa ya Moshi, katika nyumba ambayo wawili hao walikuwa wakiishi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na kusema uchunguzi bado unaendelea na utakapokamilika, hatua nyingine za kisheria zitafuata.

Wakizungumzia tukio hilo, baadhi ya majirani wamedai kuwa vijana hao walikuwa na ugomvi kuhusu simu, ambapo mtuhumiwa alidai Shabani (marehemu) amemwibia simu ndogo, jambo ambalo linatajwa huenda likawa chanzo cha tukio hilo. 

Mwenyekiti wa mtaa huo, Beatrice Kimambo amesema kijana huyo ameuawa Aprili 24, 2024 asubuhi kwa kukatwa shingo na kusababisha kifo chake papo hapo,  huku mtuhumiwa akikimbia kusikojulikana.

“Saa 12:20 asubuhi nilipigiwa simu na balozi wangu, akanieleza jirani kwake kuna tukio la mauaji limetokea. Nilifika eneo la tukio nikawapigia polisi kata, wakafika na polisi wengine wakachukua mwili na taarifa nilizozipata ni kwamba tukio hili si la kwanza, kugombana kuhusu simu ni mara ya pili,” amesema Kimambo.

Mmoja wa wapangaji wa nyumba hiyo, aliyejitambulisha kwa jina moja la Said, amesema wawili hao walikuwa wakigombana kuhusu simu, lakini chanzo kikubwa cha ugomvi huo hadi kufikia kumkata na kumuua mwenzake hakijafahamika. 

“Asubuhi nilisikia kelele huko nje, marehemu akigombana na mwenzake, tukatoka na huyu mtuhumiwa alikuwa na panga, tukawasuluhisha ikaisha kila mmoja akarudi kwenye chumba chake.

“Lakini kumbe waliendelea kubishana wakiwa ndani, sasa huyu marehemu akatoka akawa yuko hapa nje na mwenzake akatoka na panga ile bishanabishana akamkata shingoni, sisi kutoka tukakuta ameshakatwa na tulipotaka kumkamata akachukua pikipiki akakimbia,” amesema.

Ibrahimu Muhamed ambaye ni mwenye nyumba, amesema: “Ninamfahamu kama mpangaji wangu, ni mfanyakazi, anakoboa mpunga na hili tukio limetokea asubuhi na nimeamshwa nikaambiwa kuna watoto wameuana huko na sijajua chanzo ni nini.”

Naye polisi jamii wa kata ya Pasua, Hassan Yusuph ametoa wito kwa wenye nyumba kuhakikisha wanawafahamu watu wanaowapangisha kwenye nyumba zao ili kuwa rahisi kusaidia pindi wanapopata shida.

“Natoa wito kwa wenye nyumba, kila mwenye nyumba sheria inamtaka apangishe mtu anayejulikana anatoka wapi na anatoka kwa nani ili linapotokea tatizo, mwenyewe aweze kusaidiwa. Lakini pia niwatake vijana waepuke kujichukulia sheria mkononi na jamii isione matukio maovu kama haya ni kawaida,” amesema Yusuph.