Baba abaka mtoto alipoachiwa ampakate

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, George Kyando

Muktasari:

Majirani wamesema baada ya kufanya unyama huo, alimpeleka kwa mama mwenye nyumba na kumtelekeza.

Shinyanga. Mwanaume mwenye umri wa miaka 26 mkazi wa kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga anashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kwa tuhuma za kumbaka mtoto wake wa kambo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 11.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, George Kyando amesema tukio hilo limetokea Jana Aprili 8, 2022 majira ya saa nane na nusu mchana huko katika kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga.

“Ni kweli Mwanaume huyu tunamshikilia kwa tuhuma za kumbaka mtoto wake wa kambo mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi 11. Anatuhumiwa kufanya kosa hili jana baada ya mke wake kumwachia mtoto huyo na kwenda dukani," amesema Kamanda Kyando.

“Imesemekana Mtuhumiwa baada ya kufanya kitendo hicho alimpeleka mtoto kwa mama mwenye nyumba na kumwambia anatoka damu kwa kujikata kisu, pia amemuoa huyo mama akiwa tayari ana mtoto huyo,” ameongeza Kamanda Kyando.

Baadhi ya majirani wanaoishi katika eneo hilo wamesema kuwa mtuhumiwa huyo baada ya kutenda unyama huo na mtoto kuendelea kulia, alimpeleka kwa mama mwenye nyumba kisha kumwambia kuwa mtoto huyo anatokwa damu kwa sababu amejikata kisu.