Baba matatani akituhumiwa kumlawiti mtoto wake wa miaka tisa

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama.

Muktasari:

  • Ukatili wa baba huyo ulibainika baada ya majirani na jamii inayozunguka familia hiyo kuona mabadiliko na mienendo ya mtoto huyo, ambayo iliashiria kufanyiwa ukatili huo.

Morogoro. Mkazi wa eneo la Kola A mkoani hapa  Stanley Mbena (39), anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kumlawiti mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka tisa.

Akizungumzia tukio hilo leo Mei 9, 2024, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema tukio hilo limetokea Mei 3, 2024 maeneo ya Kola A, kata ya Kilakala, manispaa ya Morogoro.

Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa huyo amekuwa akiishi na watoto wake watatu baada ya kuachana na mkewe akiwemo huyo aliyemlawiti.

“Huyu mtuhumiwa alishaachana na mke wake na aliamua kubaki na watoto wake na kuishi nao na hapo ndipo alipopata nafasi ya kumlawiti mmoja wa watoto hao (jina limehifadhiwa),” amesema kamanda Mkama.

Amesema ukatili huo ulibainika baada ya majirani na jamii inayozunguka familia hiyo kuona mabadiliko na mienendo ya mtoto huyo ambayo iliashiria kufanyiwa ukatili huo.

Kamanda huyo amesema baada ya jamii kubaini ukatili huo walienda kutoa taarifa kwa maofisa wa polisi dawati la jinsia na watoto Mkoa wa Morogoro ambao walichua hatua za kuchunguza na kumkamata mtuhumiwa huyo.

“Baada ya tukio hilo, sisi polisi kwa kushirikiana na wenzetu wa ustawi wa jamii tuliamua kuwahoji na kwenda kuwapima wale watoto wengine kujua usalama wao, baada ya vipimo tulibaini walikuwa salama,” amesema Kamanda Mkama.

Katika tukio jingine la ukatili, Jeshi la Polisi linamshikilia Alex Chilongola (34), mkazi wa Kigurunyembe, Manispaa ya Morogoro kwa tuhuma za kumbaka binti yake mwenye umri wa miaka 12 ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya Msingi Kigurunyembe.

Kamanda Mkama amesema mtuhumiwa ametenda ukatili huo Mei 2, 2024 huko Kilakala na kwa sasa polisi wanaendelea na uchunguzi ili kumfukisha mahakamani.

Wakati huohuo, Iddy Mwanzo (23) anashikiliwa na jeshi la polisi kwa tuhuma za kumbaka mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Kauzeni (jina limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 16. Mtuhumiwa huyo ametenda ukatili huo Mei 4, 2024.