Bajeti ya Uwekezaji yapita, Mpina, Dk Kimei wakwama

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo akizungumza wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma leo Aprili 22, 2024.Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  •  Luhaga Mpina amekosa kuungwa mkono na wabunge kushika Shilingi kwenye mshahara wa waziri, Dk Charles Kimei akielezwa hakufuata utaratibu

Dodoma. Bunge limepitisha bajeti ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, licha ya mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina kutaka kushika Shilingi kwenye mshahara wa waziri, lakini wabunge hawakumuunga mkono.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo leo Aprili 22, 2024 amewasilisha bungeni taarifa ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka 2024/25, Bunge limejadili na limepitisha.

Profesa Mkumbo ameliomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Sh121.32 bilioni kwa mwaka wa fedha 2024/25, akiwa na vipaumbele 16 ikiwemo kuhuisha mpango wa kuboresha mazingira ya biashara (Mkumbi), kuimarisha dira mpya 2050, kufanya mapitio ya sheria mbalimbali zinazohusu ardhi, maandalizi ya sera mpya, kukamilisha uunganishaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) na Mamlaka ya Maeneo ya Uzalishaji wa Mauzo ya Nje (EPZA).

Mpina ametoa hoja kwamba, kuunganisha mashirika 16 na mengine manne kufutwa uamuzi huo umefanyika kwa kukiuka taratibu za kisheria, ilitakiwa suala hilo lipelekwe  bungeni na ndilo liamue.

“Naomba wabunge wenzangu waniunge mkono kuondoka na mshahara wa waziri,” amesema Mpina.

Hata hivyo Spika,  Dk Tulia Ackson amemwambia kwa mujibu wa kanuni hawezi kuondoka na mshahara wa waziri ila anaweza kuondoa Shilingi kwenye mshahara wa waziri.

Mpina ambaye ametoa maelezo kwamba kuna ukiukwaji wa sheria kwa waziri kufuta mashirika bila kupeleka mchakato huo bungeni kwa kuwa mashirika hayo yalianzishwa kwa mujibu wa sheria, pia kunavunja moyo wafanyakazi wa mashirika hayo.

Profesa Mkumbo amejibu hoja akisema tangazo lake lilielekeza wizara zinazohusika na mashirika yanayounganishwa na yale yanayofutwa kuanza mchakato wa kisheria kutekeleza hayo.

Mpina hakuridhika na majibu  ya waziri, aliwaomba wabunge wenzake kumuunga mkono kushika Shilingi kwenye mshahara wa waziri.

Hata hivyo, hakuungwa mkono na mbunge hata mmoja.

Spika amemweleza Mpina hoja yake haikuungwa mkono, hivyo alifunga mjadala.

Mbunge mwingine wa Vunjo, Dk Charels Kimei naye alisimama kutaka kushika Shilingi kwenye mshahara wa waziri.

“Mimi pia nataka kushika Shilingi kwenye mshahara wa waziri, lakini siungi mkono hoja ya Mpina. Hoja yangu ni nyepesi kuliko ya Mpina,” amesema Dk Kimei.

Spika amemweleza Dk Kimei kwamba mezani kwake hakuwa na taarifa yake kwamba ana hoja kwenye kifungu cha matumizi ya kawaida chenye mshahara wa waziri, hivyo hakupewa nafasi ya kueleza hoja yake.

Awali, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Exaud Kigae akifanya majumuisho amejibu hoja ya mbunge wa Viti Maalumu, Mwanaisha Ulenge kuhusu viwanda vingi kufungwa.

Amesema hakuna viwanda vinavyofungwa isipokuwa kinachofanyika ni mchakato wa kuwawezesha wawekezaji wa ndani, badala ya kutoa fursa zaidi kwa wawekezaji wa nje.

Awali, Profesa Mkumbo amesema TIC hadi Machi mwaka huu,  kilisajili miradi mipya 509 sawa na ongezeko la asilimia 112.1. Miradi inatarajia kuwekeza Dola za Marekani milioni 4,490.24 na kutengeneza ajira 229,282.

Amesema kwa miaka minne kuanzia 2020 hadi 2023, TIC ilisajili miradi 1,282 itakayoingiza Dola milioni 15,100 na kuajiri 248,309.

“Miradi ya kongani ya viwanda imesajiliwa ambayo inatarajia kuzalisha ajira za moja kwa moja 130,000 na 700,000 zisizo za moja kwa moja,” amesema Profesa Mkumbo.

Kuhusu vipaumbele, Profesa Mkumbo amesema ni pamoja na kukamilisha maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo kuelekea mwaka 2050 na kukamilisha uandaaji wa sera mpya ya uwekezaji na mkakati wake wa utekelezaji.

Amesema vingine ni kukamilisha uunganishaji wa TIC na (EPZA) na kuanzisha taasisi mpya ya kusimamia masuala ya uwekezaji wa sekta binafsi.

Profesa Mkumbo ameeleza  ofisi yake pia itakamilisha mwongozo wa ujenzi na uendeshaji wa kongani za viwanda nchini, na kufanya tathmini kuhusu uanzishwaji na uendeshaji wa maeneo maalumu ya kiuchumi nchini.

Pia, kufanya mapitio ya sheria zinazohusu masuala ya madini, ardhi, kilimo, utalii na biashara kwa ajili ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini; na kukamilisha kutungwa kwa Sheria ya Uwekezaji wa Umma na kanuni zake.

“Kuanza utekelezaji wa mradi wa kielelezo wa Ukanda Maalumu wa Kiuchumi Bagamoyo (BSEZ) kwa kuzingatia Mpango Kabambe wa mwaka 2024,” amesema.

Vipaumbele vingine ni kuanzisha mashindano ya jinsi sekretarieti za mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinavyovutia uwekezaji na kuweka mazingira bora ya uwekezaji na biashara; na kuhuisha Mpango wa Maboresho wa Mazingira ya Biashara na Uwekezaji utakaoainisha changamoto mpya za uwekezaji na biashara nchini, na namna ya kuzishughulikia changamoto hizo.