Bashungwa aapa kutoondoka Lindi, kisa barabara

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa (aliyenyoosha mkono). akizungumza jambo na watendaji wa Serikali. Picha na Bahati Mwatesa

Muktasari:

Waziri wa Ujenzi Innocent Bashungwa, amesema kuwa hatoondoka wilayani Kilwa hadi pale maagizo aliyoyatoa ya saa 72 yakamilike.

Kilwa. Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema hatoondoka mkoani Lindi, hadi pale agizo lake la kujengwa kwa barabara iliyokatika kujengwa ndani ya saa 72 litakapokamilika.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumatatu Mei 6, 2024 alipotembelea eneo la Mto Matandu, Waziri Bashungwa amesema atajitahidi kufika maeneo yote yaliyopata madhara hata ikiwa kwa boti.

“Kwa namna yoyote ile, nitajitahidi kuyafikia maeneo yote korofi, hata ikiwa kwa boti, siwezi kuondoka hapa hadi maagizo niliyoyatoa ya saa 72 yatimie,” amesema Waziri Bashungwa.

Waziri Bashungwa ametoa maagizo kwa ofisi ya  mtendaji mkuu wa Wakala wa Barabara nchini (Tanroads),  kuhakikisha wanaongeza magari ya kubebea mawe ili kuharakisha ujenzi huo.

“Namuagiza mtendaji mkuu wa Tanroads kuhakikisha anaongeza magari ya kubebea mawe, ikiwezekana barabara ya Nangurukuru iwe malori tupu,” amesema Waziri Bashungwa.

Mkandarasi anayejenga daraja la Mto Matandu, Mhandisi Joseph Peneza ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Makapu Constructors, amesema amepokea maagizo ya Waziri Bashungwa na kuahidi kuongeza magari 20 ya kubebea mawe.

“Maagizo ya Waziri nimeyachukua na nitaongeza magari 20, kwani kwa sasa hapa tuna magari 30 na hayo 20 tukiongeza yatakuwa 50,” amesema Mhandisi Peneza.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilwa, Mohamed Nyundo amesema hadi sasa jumla ya kaya 830 zimeokolewa na wapo sehemu salama ambapo kaya hizo ni katika maeneo sita yaliyoathiriwa na mvua kubwa iliyoambatana na Kimbunga Hidaya.

DC Nyundo ametaja maeneo yaliyoathiriwa na mvua kuwa ni pamoja na eneo la Mbaga, Matandu, Somanga Mtama, Mikereng'ende, Lingaula na Masaninga.

“Hadi sasa kaya 830 zimeokolewa, vifo bado ni vilevile viwili, na wale ambao bado watu wetu wa majeshi mbalimbali wakiwemo askari wa zimamoto, jeshi la akiba na waokoji wengine wamekwenda kuokoa watu ambao wapo maeneo mengine na kuwaleta sehemu salama,” amesema DC.

Fatuma Selemani ambae ni msafiri aliyekuwa anatoka Msangamkuu mkoani Mtwara kuelekea Dar es Salaam, ameiomba Serikali kuweka jitihada za makusudi ili waweze kuondoka majumbani kwao ambapo amesema tangu juzi wamekosa maeneo ya kulala, hivyo wanalala kwenye hoteli.

“Mimi nilikuwa natoka nyumbani kwa bibi yangu mkoani Mtwara, naelekea kwa mama yangu Dar es Salam, hadi sasa sijajua tutaondoka lini licha ya jitihada za Serikali wanazozifanya lakini bado hali ni ngumu,” amesema Fatuma.