Bugando yaboresha mfumo wa kidijitali kusaidia wagonjwa

Muktasari:

  • Katika kurahisisha huduma za matibabu kwa kutumia mifumo ya kisasa, Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa ya Bugando (BMC) mfumo wa kidijitali utakaosaidia kutunza taarifa za mgonjwa na kuwasiliana na hospitali nyingine nchini.

Dar es Salaam. Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa ya Bugando (BMC) imeendelea kujikita katika utoaji huduma za kisasa baada ya kufunga mfumo wa kidijitali utakaosaidia kutunza taarifa za mgonjwa na kusomana na mifumo ya hospitali nyingine nchini.

Mfumo huo, utasaidia kuondoa mkakanyiko wa taarifa za wagonjwa wanaotibiwa kwenye hospitali hiyo inayohudumia wagonjwa kati ya 1,000 hadi 1,500 kwa siku ambapo mgonjwa akitaka kwenda hospitali nyingine taarifa zitakuwa zilezile hivyo kurahisisha utoaji huduma kwa madaktari.

Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya Bugando, Dk Fabian Massaga alieleza hayo leo Alhamisi, Januari 11, 2024 katika halfa ya kuingia mkataba na taasisi inayotengeneza mifumo hiyo, (GPITG), amesema siku za nyuma walishatumia mfumo huo lakini kwa sasa umeboreshwa zaidi.

"Mfumo wao tulianza kuutumia kwa siku nyingi umekuwa na mafanikio na leo tunasaini nao tena mkataba mpya kwa ajili ya kuendeleza na kufanya nao kazi katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa Watanzania," amesema Dk Massaga nakuongeza

"Mfumo huu kama taasisi yetu inanufaika katika kurahisisha kwenye shughuli za utendaji kazi za kila siku,kama mnavyojua ni hospitali kubwa inayohudumia wagonjwa wengi lazima mifumo yake iendane na watu tunaohudumia" amesema Massaga

Naye Mkurugenzi wa taasisi ya GPITG, Adelard Kiliba ameushuru uongozi wa hospitali hiyo huku akisema kutumia mfumo huo kunawarahisishia watoa huduma kutekeleza majukumu yao kwa wakati.

"Mfumo unawezesha kusomana na mifumo ya hospitali nyingine taarifa ya mgonjwa anayetibiwa hapa Bugando  hata akienda kwenye hospitali nyingine taarifa inakuwa ileile,"amesema

Kwa maelezo ya Kiliba kampuni hiyo ya kizawa ilianza  kujishughulisha na kazi hiyo tangu mwaka 2010 na wanafanya kazi na hospitali za Serikali na binafsi ikiwemo  Bugando waliyofunga mifumo hiyo.

"Tunashukuru uongozi wa Bugando kwa kutuamini tena, kuingia mkataba mwingine kama muendelezo wa kuwapatia huduma ya mifumo ya kieletroniki kwa kuhuisha kuja kwenye hali ya ukisasa zaidi uliotengenezwa kwa kuzingatia vigezo vyote  vya Serikali na vigezo vya bima ya afya na zingine.," amesema Kiliba

Hospitali ya Bugando inatoa huduma za rufaa za kibingwa kwa wagonjwa inategemewa na mikoa ya Kanda ya Ziwa ikiwemo Mwanza, Mara, Simiyu, Geita, Kagera, Shinyanga, Tabora na Kigoma.