Chadema waanza maandamano Kilimanjaro

New Content Item (1)


Muktasari:

  •  Maandamano hayo ambayo mbele yanaongozwa na vijana wa pikipiki maarufu bodaboda, wananchi walianza kujitokeza eneo la Mailisita saa 2:30 asubuhi

Moshi. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeanza maandamano mkoani Kilimanjaro huku viongozi na wananchi wakijitokeza.

Maandamano hayo yameanzia njia za Mailisita, Mbwaruki Getifonga, wote watakutana mjini Moshi na kuelekea Viwanja vya Mashujaa kutakapofanyika mkutano wa hadhara.

Ruti ya kuanzia Mailisita wilayani Hai, ilitarajiwa kuongozwa na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe maandamano yameanza saa 6:33 mchana kuelekea mjini Moshi na mpaka yanaanza Mbowe alikuwa hajafika.

 Akitangaza kuanza maandamano hayo, Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Michael Kilawila amesema Mbowe amepata dharura na ataungana nao mbele.

Katika njia ya Mailisita wengine walioshiriki ni  Mwenyekiti wa Jimbo la Moshi Mjini, Raymond Mboya na vijana wa matarumbeta ambao wameonekana kunogesha shamra shamra za maandamano hayo.

Maandamano hayo ambayo mbele yanaongozwa na vijana wa pikipiki maarufu bodaboda, wananchi walianza kujitokeza eneo la Mailisita saa 2:30 asubuhi na kuendelea kujikusanya wakimsubiri Mbowe hadi ilipofika saa 6:31 mchana.

Njia ya Geti Fonga itakayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Taifa, Benson Kigaila  wanatarajiwa kuwepo pia viongozi mbalimbali huku ruti ya Mbwaruki ikiongozwa na Grace Kiwelu ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema Taifa pamoja na  viongozi wengine.