Chama cha PTI kupinga matokeo ya ubunge

Chama cha Pakistan Tehreek-e-Insaf (PTI) cha Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan, Imran Khan kimesema  Aprili 26, mwaka huu kitafanya mkutano wa kupinga matokeo ya uchaguzi mdogo uliofanyika Jumapili iliyopita.
 
Wakizungumza na waandishi wa habari katibu mkuu wa PTI,  Omar Ayub, mwenyekiti wa chama hicho, Barrister Gohar Ali Khan pamoja na  mkuu wa Baraza la Sunni Ittehad (SIC) Hamid Raza, wamesema kura ziliibwa bila kificho.
 
Jumapili iliyopita ulifanyika uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo manne ambapo watu wa kada mbalimbali wakiwemo wanaharakati walipinga chaguzi hizo kwa madai kuwa mitandao ya simu ilizimwa na matokeo yalichelewa kutangazwa.
 
Uchaguzi huo mdogo ulikuwa wa kwanza tangu nchi hiyo kufanya uchaguzi wake mkuu Februari 8, mwaka huu.
 
"Tutatoa wito wa maandamano Ijumaa hii katika majimbo yote manne. Maandamano mengine yatafuata maeneo ya Faisalabad, Karachi na miji mingine siku za hivi karibuni,’’ amesema Ayub akibainisha kwamba uchaguzi huo hauwezi kuitwa wa wazi na fedha za walipakodi zimepotea bure.
 
Ayoub amedai msimamizi wa uchaguzi eneo la Bajaur aliandika barua kwa baadhi ya maofisa wakiwataka kutengeneza mwanya wa kuwabana wapiga kura.
 
"Ninatoa wito kwa wakuu wa mashirika yote ya kijasusi yanayofanya kazi nchini Pakistan kuchunguza tuhuma zinazotolewa dhidi ya mashirika yao kuhusika kuharibu uchaguzi na kuomba radhi kwa Taifa kwa kuingilia uchaguzi na mahakama," amesisitiza Ayoub.
 
Gohar amedai yeye pamoja na kiongozi wa upinzani katika Bunge la Kitaifa walifanya ziara za kushtukiza katika vituo tofauti vya kupigia kura eneo la Punjab na walishuhudia wizi wa kura.
 
"Tulitoa taarifa kwa yote tuliyoyaona lakini baraza la wapiga kura bado halijaamka kutoka kwenye usingizi mzito," amesema Gohar.