Chifu Mkwawa II aomba kujengewa ofisi Iringa

Chifu Adam Mkwawa II akizungumza kwenye ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Taifa, Ali Hapi. Picha na Tumaini Msowoya

Muktasari:

  • Utawala wa Adam Sapi Mkwawa II unabaki kuwa miongoni mwa tawala chache za kikabila zilizobaki Tanzania baada ya uhuru, mwaka 1961.

Iringa. Chifu wa kabila la Wahehe, Adam Mkwawa II ameomba kujengewa ofisi ya kichifu ili iwe rahisi kwa makundi mbalimbali wanaotaka kujua historia ya  kabila hilo kukutana naye.

Iringa ni kati ya mikoa inayoheshimu nafasi za kichifu tangu wakati wa Mkwawa ambaye alifahamika pia kama Mkwavinyika Munyigumba Mwamuyinga aliyefariki Julai 19, 1898 kwa kujipiga risasi, akigoma kukamatwa na Wajerumani.

Utawala wa Adam Sapi Mkwawa II unabaki kuwa miongoni mwa tawala chache za kikabila zilizobaki Tanzania baada ya uhuru.

Kijana huyo alitawazwa kuwa chifu akiwa na umri wa miaka 13 baada ya baba yake, Abdul Sapi Mkwawa kufariki akiwa, huku  Rais mstaafu, Jakaya Kikwete akishuhudia kuapishwa kwake.

Akizungumza katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Mkwawa (Muce) wakati wa ziara ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Wazazi Taifa, Ali Hapi leo Mei 5, 2024, Chifu Mkwawa II amesema tangu zamani machifu walikuwa wakifanya kazi za jamii na Serikali, jambo ambalo na yeye anaomba litokee.

Amesema naye ni miongoni mwa watu muhimu kwenye jamii wanaoweza kuisaidia kuhusu masuala mbalimbali ikiwamo kuwakumbusha historia ya kichifu na namna wazee wa zamani walivyotunza maadili kwenye jamii zao.

“Babu yangu Adam Sapi Mkwawa alikuwa Spika wa Bunge, alifanya kazi nzuri na jamii na aliweza kuwakumbusha watu wapi walipotoka, walipo na wanakokwenda. Jamii inakumbana na changamoto nyingi kwa sababu imesahau ilikotoka, ombi langu ni kujengewa ofisi hapa mjini,” amesema Chifu Mkwawa II.

Amebainisha kuwa kuna uhusiano mkubwa baina ya mmomonyoko wa maadili kwenye jamii na masuala ya kihistoria.

“Kama vijana watafundishwa masuala ya historia, tunaweza kurudisha maadili ambayo kwa sasa hakuna. Fikiria hadi mtu anabaka mtoto maana yake hana anachojua kuhusu maadili. Nipo tayari kusaidia, naomba kupata ofisi,” amesema.

“Niwaombe vijana wenzangu kwenye jamii, tusiwaache wazee wetu, tukae nao watufundishe maadili na namna wao walivyokuwa. Haya maisha tunayoishi sasa yatakuja kutugharimu baadaye tusiposikiliza wazee,” amesema.

Chifu Mkwawa II amelelewa na wazee wa kimila mkoani Iringa na mara zote anapotokea kwenye jamii, huwa amevaa mavazi meupe maarufu kwa jina la mgolole.

Hapi amesema amelipokea ombi hilo na atashirikiana na viongozi wengine wakiwemo wa Serikali kulifanyia kazi.