DC Serera afanikisha urejeshwari wa Sh5 milioni Simanjiro

Muktasari:

  • Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera amesimamia urejeshaji wa Sh5 milioni kwa kijiji cha Ngage, baada ya katibu wa kikundi cha ushirika cha Inywati Moipo kufanyia ubadhirifu fedha hizo.

  

Simanjiro. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, Dk Suleiman Serera amesimamia urejeshaji wa Sh5 milioni kwa kijiji cha Ngage, baada ya katibu wa kikundi cha ushirika cha Inywati Moipo kufanyia ubadhirifu fedha hizo.

Kikundi cha ushirika cha Inywati Moipo cha kijiji cha Ngage kilikuwa na mashine ya kusaga, soko na kutoa mikopo kwa wanawake, kilifilisika na kutakiwa kutoa Sh5 milioni kwa kijiji hicho.

Dk Serera akizungumza kwenye kijiji cha Ngage amesema endapo kiongozi wa kikundi hicho asingerejesha kiasi hicho cha fedha Sh5 milioni angeondoka naye kwa kumchukulia hatua.

“Fedha hizi Sh5 milioni zimesharejeshwa na zinapaswa kuwekwa benki kwenye akaunti ya kijiji cha Ngage kwa ajili ya matumizi ya maendeleo mengine ya wananchi,” amesema Dk Serera.

Amemwagiza ofisa mtendaji wa kijiji hicho kufanikisha uwekwaji wa fedha hizo benki kwenye akaunti ya kijiji kwa lengo la maendeleo kwani mgogoro wa suala hilo umekwisha.

Amesema fedha hizo zilipaswa kurejeshwa kwenye kijiji baada ya ushirika kufilisika na baada ya kupata taarifa za ufujaji wa fedha hizo aliagiza zirejeshwe.

“Baada ya kikundi kufilika na kuuza mali zao ikiwemo na kutoa mikopo walipaswa kutoa fedha hizo Sh5 milioni kwenye kijiji cha Ngage ila huyu kiongozi akakaa nazo," amesema Dk Serera.

Mkuu wa Takukuru wa wilaya ya Simanjiro, Otenyo Michael amesema baada ya kiongozi huyo katibu wa ushirika kukiri kuwa atarajesha fedha hizo walimsamehe hivyo hawatamchukulia hatua.

“Kiongozi wa vikundi hicho cha ushirika angechukuliwa hatua endapo asingerejesha fedha hizo kama alivyoagizwa na mkuu wa Wilaya ila baada ya kuzitoa amesamehewa," amesema Otenyo.