DC Sumaye ahimiza kuenzi fikra za waasisi wa Muungano

Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Zephania Sumaye akizungumza wakati wa dua maalumu ya kuliombea Taifa katika ukumbi wa manispaa ya Moshi, mkoani Kilimanjaro. Picha na Janeth Joseph

Muktasari:

  • Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 26, 1964 kutokana na kihistoria baina ya nchi hizo katika nyanja mbalimbali kama vile udugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na uhusiano wa karibu kisiasa.

Moshi. Wakati Taifa likiadhimisha miaka 60 ya Muungano Aprili 26, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, Zephania Sumaye amewataka wananchi wa wilaya hiyo kuendelea kudumisha amani na utulivu wilayani humo ili fikra na falsafa za waasisi wa Taifa hili zinaendelea kudumu hadi vizazi vijavyo.

Tanganyika na Zanzibar ziliungana Aprili 26, 1964 kutokana na kihistoria baina nchi hizo mbili katika nyanja mbalimbali kama vile udugu wa damu, biashara, utamaduni, lugha na uhusiano wa karibu kisiasa, hususani baina ya vyama vya Tanu na ASP.

Akizungumza wakati wa dua maalumu ya kuliombea Taifa, iliyofanyika leo, Aprili 23 mjini Moshi, Zephania amewaomba viongozi wa dini wilayani humo kuendelea kuliombea Taifa akidai maombi yana nguvu ya kuliimarisha Taifa.

“Muungano wetu umeweza kudumu na kuwa imara kwa sababu ya mambo mengi ambayo yameweza kuchangia kuimarika kwake, ikiwa ni pamoja na historia yetu nzuri, undugu wetu, fikra na falsafa imara za viongozi wetu waasisi wa Taifa hili,” amesema.

Amesema amani iliyopo imekuwa ni ngao ya kudumisha Muungano na kwamba yapo mataifa yaliyoungana na hayakuweza kuchukua muda mrefu kama ilivyo kwa Taifa hili.

“Wapo wengi waliojitajidi kuungana kama sisi wakashindwa lakini wapo waliofanikiwa lakini wakakaa muda mfupi lakini sisi tumeweza kuishi kwa miaka 60, ni jambo la kumshukuru Mungu,” amesema.

Zephania amesema  Muungano wa Tanganyika na Zanzibar umekuwa na manufaa ambayo yamepanua wigo wa masuala ya ajira, uchumi, biashara, pamoja na tunu katika Taifa, ambayo yamechangia sana kuimarisha  Muungano.

“Muungano wetu huu ulionekana muhimu miaka 60 iliyopita, tumerithishwa, wengine tulikuwa hatujazaliwa, tumebakiza kazi moja ya kuhakikisha kwamba tunaulinda na kuutunza na kuurithisha kwa vizazi vingine,” amesema.

Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Moshi, Faraji Swai naye amewataka viongozi wa dini kuendelea kuliombea Taifa hili ili kuliepusha na majanga yanayoweza kuleta madhara kwa nchi.

“Yapo mambo yanayotokea, mvua  za kuzidi kipimo na mengine mengi, turudi kwa Muumba wetu ili mambo yetu yaende vizuri na kuleta mafanikio, lakini pia viongozi wetu wa dini tunaomba waliombee Taifa letu,” amesema Swai.

Kadhi wa Mkoa wa Kilimanjaro, Hussein Chifupa ambaye amemwakilisha Sheikh wa Mkoa, amesema Watanzania wana wajibu wa kumshukuru Mungu kwa kutimiza miaka 60 ya Muungano na kuwataka Watanzania kuendelea kutendeana mema.

“Miongoni mwa faida zinazopatikana katika kutendeana mema ni muunganiko ambao tunao katika nchi hii. Tuna wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu, miaka 60 sio michache lakini unaposhukuru Mungu anakuzidishia zaidi, hivyo tuendelee kupendana ili amani na upendo uliopo uzidi kututawala,” amesema.