DIT kufungua viwanda viwili 2022

Muktasari:

Taasisi ya Teknolojia Dar es Salam (DIT) inatarajia kufungua rasmi viwanda viwili, kikiwemo cha uchakataji wa bidhaa za ngozi.

Dar es Salaam. Taasisi ya Teknolojia Dar es Salam (DIT) inatarajia kufungua rasmi viwanda viwili, kikiwemo cha uchakataji wa bidhaa za ngozi.

 Viwanda hivyo vitapunguza gharama za uagizaji wa bidhaa kutoka nje na kuongeza ajira kwa wananchi, ikiwemo wahitimu wa vyuo vya ufundi.

Mwenyekiti wa Baraza la DIT, Dk Richard Masika amebainisha hayo leo Alhamisi Julai 29, 2022 baada ya Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda, kutembelea kiwanda cha utengenezaji wa vipuri.

Amesema taasisi hiyo imekuwa ikitoa mafunzo kwa nadharia na baadae kwa vitendo kadri teknolojia inavyokuwa.

Amesema Taasisi hiyo imedhamiria kuingia kwenye hatua ya tatu ya uzalishaji, ili kuongeza ajira ikiwemo kwa wanaokusanya bidhaa hizo na kuzichakata.

"Hatua nyingine ni kwa wake wanozalisha vipuri hivi, mashine za uzalishaji tunatengeneza hapa na uzalishaji tunafanyia hapahapa," amesema Dk Masika.

"Lengo letu ni mwanafunzi anapotoka hapa na kwenda kiwandani kwa muajiri wake, aweze kutimiza majukumu yake kwa ufanisi," amesema.

Naye Waziri wa Elimu Profesa Mkenda amesema, baada ya mafanikio hayo makubwa wataangalia ubora wa bidhaa hizo illi ziweze kuingia sokoni.

"Mambo yanayoweza kuinua uchumi wa nchi yetu ni pamoja na kiwanda hiki baada ya kuzalisha bidhaa za kutosha tunaweza kusambaza maeneo mbalimbali tukishaangalia ubora na kujiridhisha,"ame wesema Profesa Mkenda.

Amebainisha kuwa zipo programu mbalimbali za kufundisha wakufunzi wa ndani nje ya nchi, na Serikali iko tayari kuwajengea uwezo ili kurekebisha ujuzi kwa vyuo.

"Nchi zilizoedelea kote Duniani zilianza kwa kuzalisha vipuri, hapa Tanzania hatuwezi kuanza kuzalisha pikipiki kama hatutaweza kuzalisha vipuri,"amesema Profesa Mkenda.