Dk Biteko atangaza mgawo wa umeme kumalizika Tanzania

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

Amesema changamoto iliyopo ni miundombinu ambayo wanaendelea kuiboresha.


Dodoma. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko ametangaza kumalizika kwa mgawo wa umeme nchini baada ya uzalishaji kuongezeka.

Mgawo wa umeme ulianza Septemba 2023 kutokana na upungufu wa uwezo wa uzalishaji wa umeme kutoka kwenye vyanzo mbalimbali.

Septemba 25, 2023 Rais Samia Suluhu Hassan alimpa miezi sita bosi mpya wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Gissima Nyamo-Hanga kuhakikisha umeme unapatikana.

Leo Jumanne Aprili 16, 2024 akizindua wiki ya nishati 2024, kwenye viwanja vya Bunge, Dk Biteko ametangaza kumalizika kwa mgawo nchini Tanzania.

Amesema kulikuwa na mgawo wa umeme nchini, lakini sasa haupo kwa sababu kuna umeme wa kutosha.

“Hivi ninavyoongea tuna umeme wa kutosha na tuna mitambo tumeiacha ‘standby’ tunasubiri mtambo wowote ukikorofisha tuuwashe. Kwa mfano Kinyerezi megawati 150 zile hatujauwasha leo kwa sababu umeme tunao wa kutosha,” amesema.

Amesema changamoto iliyopo asa ni miundombinu ambayo wanaendelea kuiboresha kwenye maeneo kadhaa.
Dk Biteko amelipongeza Tanesco kwa kazi waliyoifanya siku ambayo mtambo wa Kidatu ulipata shida.

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko (kulia) akiwa na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu

Amesema walipata tatizo katika mitambo ya kuzalishia umeme Kidatu ambako valvu moja ilizidiwa maji katikati ya Sikukuu ya Pasaka, saa nane usiku, hivyo maji kujaa ndani ya chumba.

Amesema alipompigia simu mtu anayeshughulika na miradi ya kuzalisha umeme kwa njia ya maji na kumuuliza wanahitaji siku ngapi kurejesha umeme, alimjibu wakijitahidi sana ni siku tatu.

“Nilikuwa katika Pasaka nguvu za kuendelea kusherehekea kufufuka kwa Yesu zikaisha. Mimi nikawaambia wote twende site,” amesema.

Amesema kazi hiyo waliifanya kuanzia saa nane usiku na ilipofika saa tisa alasiri walikuwa wamemaliza.

Amesema pia nguzo nyingi zimeanguka wakati wa mvua, lakini hata maeneo yasiyoweza kufikika kwa urahisi wamekuwa wakibeba nguzo kwa toroli za kukokotwa na punda, ili mradi zifike kwenye maeneo husika.

Dk Biteko amesema katika kikao cha wabunge wa CCM wameshamweka kitimoto mara kadhaa wakimweleza wao hawataki stori, ila wanataka umeme.

Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu amesema watafanya kazi pamoja na Serikali kuhakikisha mipango inatimia na kuwapatia fedha wanazozitaka kwa sababu wanaamini zinarudi na kufanya kazi kwa wananchi.

Amempongeza Rais Samia kuwa aliwaahidi masuala ya umeme na sasa wanauona.

“Magrupu ya kulalamika ya umeme sasa hivi hayana wachangiaji kwa sababu umeme upo tofauti na mwaka uliopita, au miezi mitatu iliyopita magrupu hayo yalikuwa yakimaliza data mpaka Sh20,000 kwa siku,” amesema.

Amesema changamoto ndogo-ndogo zipo, lakini zinafanyiwa kazi.

Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Kilumbe Ng’enda ameomba Serikali kusimamia uagizaji wa gesi kwa kuwa hivi sasa kila kampuni inajiagizia kivyake.

“Lazima tuwe na mamlaka inayosimamia uagizaji wa gesi kwa pamoja, ili tupate kwa bei nafuu na ubora unaostahili,” amesema.
Mwakilishi wa Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC), Francis Ndulane amesema kamati hiyo ingependa mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP) ukamilike kwa haraka.

Amesema mradi huo unagharimu Sh6.5 trilioni na utekelezaji wa wake umefikia asilimia 97.43 na malipo yaliyofanyika ni Sh5.97 trilioni sawa na asilimia 91.

“Utaongeza hamasa na kuvutia wawekezaji, hivyo ni rai ya kamati kuhakikisha mradi huu unakamilika ndani ya muda uliopangwa, ili kuwezesha mradi kupata tija na thamani ya kifedha zilizowekezwa,” amesema.

Amesema katika mikoa ya Lindi na Mtwara kumekuwa na changamoto ya miundombinu ya umeme na kwamba hilo ni tatizo kubwa hasa wakati huu mvua zinapoendelea kunyesha.
Ameomba kuwekwa nguzo za zege katika mabonde yanayotiririsha maji.