Dk Biteko: Kutokarabati miundombinu ya umeme kwa wakati ni uzembe

Muktasari:

  • Serikali imetaka ukarabati na mabadiliko ya vifaa vinavyotumika kutoa huduma ya umeme, yafanyika haraka mara tu vinapoharibika.

Dar es Salaam. Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko amesema kinachochelewesha ukarabati wa miundombinu ya umeme inapoharibika ni uzembe.

Dk Biteko amesema hayo leo Februari 21, 2024 akiwa ziarani mkoani  Njombe alikoshiriki kuwasha umeme katika Kijiji cha Ikwavila na Shule ya Sekondari ya Wasichana Njombe, ambapo  amesisitiza matengenezo kufanyika haraka.

"Huu ni uzembe. Hili suala la transfoma inaungua halafu inachukua hadi mwezi mmoja kubadilishwa, uzembe huu haukubaliki. Idara ya Manunuzi ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) tumeibadilisha kutokana na sababu hizi.

“Vifaa hivi vinazalishwa kwenye viwanda vya ndani, tunataka watendaji hawa waone shida wanazopata wananchi na kuzitatua, kweli kuna changamoto ya umeme lakini kuna baadhi ya matatizo Tanesco wanaweza kuyamaliza," amesema.

Hata hivyo, ameweka wazi kuwa Serikali isingependa kuona changamoto ya umeme inaendelea, ndiyo maana inatekeleza kwa kasi mradi wa Umeme wa Julius Nyerere (JHNPP).

Amesema kwa sasa mradi huo umefikia asilimia 99 na mtambo mmoja umekamilika utakaoingiza megawati 235 kwenye gridi mwezi huu.

“Mtambo mwingine unatarajiwa kuingiza megawati nyingine 235 Machi mwaka huu,” amesema.

Katika ziara hiyo, mbunge wa Wanging'ombe aliomba laini ya umeme inayojitegemea, kwa kuwa ya sasa inatumiwa na Lupembe na TANWAT hivyo kupunguza kasi ya umeme.

Akijibu ombi hilo, Dk Biteko ameiagiza Tanesco kujenga kituo cha kupoza umeme wilayani humo, ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa huduma hiyo.

Kuhusu usambazaji wa umeme, Dk Biteko amesema vijiji vyote 108 vya wilaya hiyo vina umeme, huku asilimia 56 ya vitongoji tayari vimeshasambaziwa nishati hiyo.

“Kazi inaendelea Sh9 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kusambaza umeme katika wilaya hii,” amesema.

Katika hatua nyingine, Dk Biteko amewataka wananchi watumie uchaguzi wa Serikali za mitaa kuchagua viongozi sahihi, huku akiwaagiza viongozi wa Serikali kujikita katika kutatua kero za wananchi.

Lingine aliloagiza ni kuhakikisha watoto wote wenye umri unaostahili kuanza shule wakaripoti kwa kuwa huduma hiyo inatolewa bila ada.

Maelekezo hayo ya Dk Biteko, yametokana na malalamiko yaliyoibuliwa na Mbunge wa Wanging’ombe, Dk Festo Dugange aliyelalamikia kuungua kwa transfoma 50 hadi 60 kila mwaka, huku matengenezo yakichelewa kufanyika.

Kuharibika kwa transfoma hizo, kulingana na Dk Dugange kunasababishwa na kupigwa na radi ambazo mara nyingi hutokea katika Wilaya ya Wanging’ombe.

Mbunge Dugange, ameshukuru hatua ya wilaya hiyo kupata umeme karibu vijiji vyote.

Awali, akizungumza katika ziara hiyo, mwakilishi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Godfrey Chibulunje amesema Sh70.44 bilioni zimetengwa kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini, huku Wangingo’mbe ikipata Sh9.35 bilioni.