Dk Makakala: Sikupanga kuwa askari

Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI), Dk Anna Makakala  akizungumza katika Jukwaa la nne la The Citizen Rising Woman lililofanyika Machi 8, 2024 katika ukumbi wa Super Dome Masaki jijini Dar es Salaam leo.

Muktasari:

  • Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI), Dk Anna Makakala amesema ndoto yake ilikuwa ni udaktari na hakuwa amepanga kuwa askari.

Dar es Salaam. Kamishna Jenerali wa Uhamiaji nchini (CGI), Dk Anna Makakala amesema hakuwa amepanga kuwa askari lakini aliamua kutumia fursa iliyokuja mbele yake.

Dk Makakala ametoa kauli hiyo leo Machi 8, 2024 katika jukwaa la nne la The Citizen Rising Woman lililofanyika leo Machi 8, 2024 huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi.

Amesema awali ndoto zake ilikuwa ni udaktari na alikuwa akipenda somo la baiolojia lakini alibadilisha gia angani.

Akiwa ni mzaliwa wa Musoma ambaye wazazi wake wanatoka Ruvuma, alisoma Dar es Salaam katika shule ya Msingi Mbuyuni kabla ya kujiunga shule ya sekondari wasichana Jangwani.

“Nilipoenda kidato cha tano na sita nilibadilisha mfumo, baadaye nilienda kusoma Chuo Kikuu cha Mzumbe na katika kutafuta kazi ile ndoto yangu niliibadilisha kutokana na fursa iliyokuwa mbele yangu,” amesema Dk Makakala.

Amesema baadaye nafasi za kazi zilitangazwa lakini hakutaka kuomba lakini siku ya mwisho alipeleka maombi na alikubaliwa kujiunga na jeshi.

“Lakini wote tunakuwa na marafiki wenye mtazamo tofauti kwa sababu zamani nikiwa mdogo watu mnapenda kusuka nywele hadi mgongoni, mnavaa hivi lakini nimeenda chuoni tunanyoa upara halafu mnavaa buti la jeje, sasa unaangalia yale maisha umeyabadilisha kabisa kwamba ulikuwa hivi unaenda kuwa kitu kingine,” amesema Dk Makakala.

Amesema hilo halikumsumbua na badala yake alibadilisha maisha na kujiunga na jeshi kitu ambacho hakukitegemea kwenye maisha.

“Sikutegemea kama siku moja nitakuwa askari. Kitu ambacho naweza kuwaasa wasichana katika maisha wasiangalie ile mipango ya kuwa nani lakini ikashindikana kutokana na mazingira au fursa zilizopo,” amesema Dk Makakala.

Ametumia nafasi hiyo kuwaasa wasichana kutumia chochote kinachotokea mbele yao huku wakijitahidi kupata mafunzo au elimu ambayo yatawawezesha kufanya jambo hilo.

“Nawahamasisha wengi pia kwa sababu ulinzi na usalama si suala la wanaume peke yake ni suala la watu wote na kitu cha kujivunia Tanzania, Amiri Jeshi Mkuu ni mwanamke na mnaona nchi iko imara na tuko salama na yeye ndiyo anatuhamasisha na tunamshukuru kwa kuendelea kutumiani kuendelea kumsaidia kazi ili na wengine chini yetu wajue kuwa wanawake tunaweza,” amesema Dk Makakala.