Dk Mpango ataka AGRF kuleta suluhisho la chakula

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango.

Muktasari:

  • Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amefungua Jukwaa la Mifumo ya Chakula akitaja wajumbe kuja na suluhisisho la usalama wa chakula nchini.

Dar es Salaam. Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango amewataka wajumbe wanaohudhuria Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF), kuja na suluhisho la upatikanaji wa chakula barani Afrika.

Ameyasema hayo leo Septemba 5 alipokuwa akifungua mkutano huo jijini hapa wenye wajumbe zaidi 5,000 kutoka zaidi ya nchi 70 duniani.

"Mkutano huu wenye kauli mbiu ya ‘Rejesha, Zalisha, Tekeleza: Suluhisho la Afrika la Maboresho ya Mifumo ya Chakula,’ ni juhudi za pamoja kutatua na kutafsiri maneno hayo kuwa hatua muhimu kupata maboresho ya mifumo ya chakula," amesema.

Akieleza mikakati ya Serikali katika kutafuta suluhisho la mifumo ya chakula, Dk Mpango amesema imeongeza bajeti ya Wizara ya kilimo kwa zaidi ya asilimia 70 ndani ya miaka miwili iliyopita.

“Kwanza kilimo kitambulike kama injini ya ukuaji shirikishi na mhimili wa uchumi. Kinaajiri silimia 65 ya Watanzania na kinachangia asilimia 27 katika pato la Taifa kikikuwa kwa asilimia 5 kwa mwaka.

"Kilimo kinachangia asilimia 30 ya bidhaa zinazouzwa nje na kutoa asilimia 65 ya bidhaa za viwandani,” amesema.

Kuhusu uongezwaji wa bajeti, Dk Mpango amesema, “Uongezwaji huo umelenga kukuza uzalishaji kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030, kutoka kiwango cha asilimia 5.4. Pia mkakati huo unalenga kukuza kukuza huduma za ugani, uwekezaji na kuhamasisha vijana kushiriki katika kilimo biashara.”

Pia ametaja suala la sera akisema Serikali imeendelea kuboresha sera za kukuza uzalishaji wa kilimo.

“Hapa Tanzania tumeanzisha mfumo wa hali ya chini na wa muda mrefu wa kugharamia kilimo kwa sekta binafsi ikiwamo kuanzisha mpango katika Benki Kuu unaowezesha benki kukopa kwa ajili ya kukopesha wakulima katika riba ya chini ya asilimia 10.

Amesema pia Serikali imeweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi ikiwa pmoja na mbinu za kilimo kwa kuangalia afya ya udongo, matumizi ya pembejeo chache kama kemikali na mbolea.

“Tumeongeza pia uwekezaji wa utafiti wa kilimo na elimu. Hii ni pamoja na kufanya kazi kwa karibu na vyuo vikuu, taasisi za utafiti, ili kukuza mbinu za kilimo, dawa za kuua wadudu, mbegu na kuhamasisha kilimo biashara na kuhamasisha vijana kushiriki,” amesema.

Ili kukabiliana na janga la njaa, alisema bara la Afrika linapaswa kukumbatia mbinu za kisayansi zikiwemo za kienyeji kuzalisha chakula, kuepuka kunyonya wakulima na kuimarisha mnyororo wa bidhaa za chakula.

“Amani na utulivu ni mambo muhimu kufanikisha mifumo ya chakula," amesema.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais, Waziri wa Kilimo, Husein Bashe asema Bara la Afrika ni changa, lina asilimia 67 ya ardhi ambayo bado haijatumika, akishauri Waafrika kuungana katika matumizi ya rasilimali.

“Usalama wa chakula utakuwepo ikiwa viongozi wa Afrika watafanya wajibu wao kwa kuungana badala ya kushindana katika matumizi ya rasilimali zilizopo,” amesema.