Dk Nchimbi afunguka ukaribu wake na viongozi wa upinzani

Katibu Mkuu CCM, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza wakati wa ufunguzi wa kongamano la kumbukizi ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, uliyofanyika katika Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere Kivukoni, jijini Dar es Salaam leo Aprili 8, 2024. Picha na Sunday George

Muktasari:

  • Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amesema si aibu kwake kuonyesha urafiki wake binafsi na wanasiasa wa vyama vya upinzani.

Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amesema haonei aibu urafiki wake binafsi na sehemu kubwa ya viongozi wa vyama vya upinzani.

 Msingi wa kauli yake hiyo ni kile alichofafanua kuwa huwezi kujivunia utanzania kama huna mapenzi na Watanzania wenzako, hivyo itikadi za vyama haziwezi kukwaza urafiki wake na watu.

Mtendaji mkuu huyo wa CCM ametoa kauli hiyo leo Aprili 8, 2024 wakati akihutubia kongamano la maadhimisho ya kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere (MNMA).

Ameijenga hoja hiyo kwa kurejea kile alichokiita matendo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ambaye enzi za uhai wake aliwapenda Watanzania wote bila kuwabagua.

Kuhusu urafiki na viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani, amesema haoni haya juu ya hilo na kwamba mara nyingi amekuwa akiwasiliana nao kila wanapoonekana wamezungumza vibaya, hasa majukwaani.

"Viongozi wengi wa upinzani ni rafiki zangu binafsi na mara nyingi wakishaongea kwenye mikutano yao kama wameongea kitu kibaya huwa nawatumia ujumbe kuwaeleza ulichozungumza leo kama Watanzania wamekusikia, basi wamehisi umevuta bangi.

"Unakuta ananipigia tunazungumza, tunacheka na mwisho wa siku tunamaliza mazungumzo, ndivyo ambavyo Watanzania tunapaswa tuishi," amesema.

Amesisitiza misingi ya utanzania ni kuwapenda Watanzania wenzako bila kufikiria ubaguzi wa kiitikadi, rangi wala kabila.

Katika hotuba yake hiyo, Dk Nchimbi amesema kwenye uongozi wa sasa ni vema kumteua kiongozi kulingana na kaliba yake.

Ameeleza wapo baadhi ya watu wenye uwezo mkubwa katika kuhamasisha maendeleo, lakini wanapopitiwa na fedha karibu lazima waibe.

"Sasa mtu kama huyu inabidi umpeleke katika eneo ambalo atafanya hiyo kazi ya kuhamasisha maendeleo, ili usiukose ule ufanisi wake lakini asiwe karibu na fedha, kama ni mzuri kwenye kusimamia fedha mpeleke huko," amesema.

Hoja ya ukaribu wa Dk Nchimbi na wanasiasa wa upinzani, iliungwa mkono na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Dk Ayub Rioba aliyesema mwenendo huo ndiyo nyenzo ya uongozi bora.

Amesema ili kuwa kiongozi bora ni vema utoe nafasi ya kusikiliza wengine wakiwemo wanaokupinga.


Akemea wizi

Dk Nchimbi alitumia jukwaa hilo, kueleza uwepo wa sehemu kubwa ya Watanzania ambao aghalabu wanapozungumzia nafasi ya uongozi akili zinawapeleka kwenye kupiga dili.

"Robo tatu ya watu wakiongelea nafasi ya uongozi, akili yao inawapeleka kwenye kupiga dili," amesema.

Amesema akili hizo ni matokeo ya kwenda kinyume na misingi ya Baba wa Taifa juu ya kupenda kazi.

"Mara nyingi asiyependa kazi hupendelea kupata kwa urahisi, ili apate kwa urahisi ataiba na mwizi mara zote yupo tayari kuuwa," amesema.

Amesema msingi wa mambo yote ni kutoandaliwa kwa viongozi kama ilivyokuwa ikifanyika zamani.

Ameeleza Mwalimu Nyerere alitumia nguvu kubwa kuandaa viongozi na hata wakati anakaribia kung'atuka alihangaika kumtafuta mrithi.

"Ndiyo sababu hata alimtafuta Edward Sokoine akamuona anafaa katika wadhifa wa Waziri Mkuu, lakini alimuona hana ‘exposure’ na ikabidi ampeleke nje ya nchi kusoma," amesema.

Amesisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa utaratibu wa kuandaliwa kwa viongozi na kwamba usiishie katika Chuo cha MNMA pekee, bali viwepo na vingine vitakavyoifanya kazi hiyo.

Hata hivyo, amesema ni muhimu kuwepo vyuo vinavyofundisha wananchi kutoka katika vyama vyote na kuwe na namna ambayo kila chama kiwe na mchango.

"Si wajibu wa CCM peke yake, lazima chama kinachotawala na vya upinzani vikae chini kukubaliana muundo wa taasisi ya elimu kwa wanasiasa wake," amesema na kuongeza kila Mtanzania anapaswa kujua kuwa ana wajibu kwa Taifa lake.

Akichangia mada kuhusu amani, umoja, na uwajibikaji katika ujenzi wa taifa, mkufunzi wa Chuo cha Uongozi cha Julius Nyerere, Kanali Joseph Simbakalia amesema chama cha Tanu ndicho kilichojenga misingi yote ya nchi.

Hata hivyo, amesema ili kuwepo na amani kunahitajika umoja kwanza.

"Ni jambo la fahari ulitengenezwa umoja na baadaye ukaja umoja wa Taifa unaotokana na Tanganyika na Zanzibar na kuunda Tanzania," amesema.

Akitoa taarifa ya chuo, mkuu wa chuo hicho, Profesa Shadrack Mwakalila amesema tangu mwaka 1961 ambapo chuo hicho kilianzishwa viongozi 2,000 wamepata mafunzo ya uongozi.

Amesema chuo hicho kilimilikiwa na CCM hadi mwaka 1991 kilipokabidhiwa kwa Serikali na mwaka 2005 kikabadilishwa jina kutoka Chuo cha Kivukoni na kuwa Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere.

"Kwa sasa chuo hiki kina matawi matatu, ikiwemo Kivukoni, Karume, Bugugu Unguja na Pemba katika Wilaya ya Chakechake," amesema.

Amesema kwa sasa chuo hicho kimeongeza masomo ya uongozi, maadili na uzalendo katika mitalaa yote, ili kila mwanafunzi anayehitimu chuoni hapo awe na ujuzi kuhusu masuala hayo.