Dk Nchimbi ampiga tafu Tulia Mbeya Mjini

Muktasari:

  • Ziara ya wajumbe wa sekretarieti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakiongozwa na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Emmanuel Nchimbi wameendelea mkoani Mbeya.

Mbeya. Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Emmanuel Nchimbi amewaambia Wana-CCM mkoani Mbeya wanatakia kulinda heshima ya Taifa wa kuhakikisha wanamshikilia mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson ambaye ni Spika wa Bunge.

Katibu mkuu huyo, ametoa kauli hiyo leo Jumatano, Aprili 17, 2024 wakati akizungumza na mabalozi wa mashina wa CCM, viongozi wa Serikali, wazee, machifu na vingozi wa dini pamoja na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Dk Nchimbi amesema wananchi wa Mbeya wameipa sifa Taifa kwa mwakilishi wao kushika nafasi ya Rais wa Mabunge ya Dunia (IPU).

"WanaCCM wa Mbeya mmetupa sifa kubwa kama Taifa, baada ya kumchagua Dk Tulia amekuwa Spika wa Bunge na sasa ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani, mnaweza msijue uzito wa nafasi hiyo, lakini mjue heshima mlionayo duniani ni kubwa kuliko mnavyofikiri.

"Kwa hiyo ni hiari yenu mnataka kuendelea na heshima hiyo au mmechoka kuheshimika? Maana kuna watu wengine wanajisikia tu hamu ya kupoteza heshima.

Ametolea mfano kuna mtu anaamka tu asubuhi anajisikia hamu ya kupoteza heshima kwa kupita na kutukana kila mahali ili kupoteza heshima, hivyo ni hiari yao kama wanataka hivyo.

"Kama mnataka kupoteza heshima potezeni, lakini kama mnajua heshima yenu kubwa duniani na mna wajibu wa kuilinda mbarikiwe sana," amesema Dk Nchimbi.

Awali, akimkaribisha Dk Nchimbi kuzungumza na viongozi hao wa CCM, Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Amos Makalla amesema Serikali imedhamiria kufanya upanuzi wa ujenzi wa barabara kwa njia nne ya Nsalaga hadi Ifisi yenye urefu wa kilomita 29 kwa kiwango cha lami.

"Ujenzi huu ni mkakati wa kupunguza msomgamano wa magari, mchakato huo unaofadhiliwa na Serikali utagharimu Sh138.7 bilioni

"Dhamira ya Serikali ni kujenga barabara hiyo inayoanzia Igawa - Songwe - Tunduma yenye urefu wa kilomita 218 ili kuunganisha mikoa ya Njombe, Mbeya, Songwe na nchi jirani za Zambia, Malawi na Congo

Makalla amesema mkoa huo umepiga maendeleo akiwashangaa wanaobeza kuwa hakuna kilichofanyika,wakati Serikali imefanya kazi kubwa.

"Unakuta mtu anasema mbeya hakuna maendeleo, wakati yapo hivi sasa usafiri wa anga ni muda wote hapa lakini wengine nakuta wanajifanya hawaoni wakati wanatumia usafiri huo," amesema.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Mbeya, Patrick Mwanulenge amewataka makada wenye nia ya kuwania nafasia mbalimbali kama wana mambo wanataka kuyafanya basi wayatekeleze sasa sio kusubiri wakati wa uchaguzi.

"Kama unataka kufanya kitu kifanye sasa sio wakati wa uchaguzi ili tuyaone hayo maendeleo,siyo ukifika wakati wa uchaguzi unatuletea khanga na fulana hakutakuwa na nafasi hapa," amesema Mwanulenge.