Elimu bila malipo bado kitendawili

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tamisemi, Angellah Kairuki.

Dar es Salaam. Wakati fedha zinazotengwa kwa ajili ya kugharimia elimu bila ada kwa shule za msingi na sekondari zikiongezeka kila mwaka, asilimia 68.4 pekee ya fedha ndiyo ilitolewa kati ya kiasi kilichopangwa mwaka 2022/23.

Kwa mujibu wa hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) ya mwaka 2023/24 iliyowasilishwa wiki iliyopita na Angellah Kairuki ambaye ni Waziri, mwaka 2022/23 Tamisemi iliidhinishiwa Sh346.49 bilioni kwa ajili programu hiyo, lakini hadi Februari, mwaka huu ni Sh235.75 bilioni ndiyo zilizopokewa.

Hata hivyo, Waziri Kairuki alifafanua kuwa utekelezaji wa bajeti hufanywa kwa miezi 12, kati ya Juni mwaka unaotangulia na Juni mwaka unaofuatia, hivyo ni ngumu kusema fedha hazikupelekwa kiwango hicho kwa kutumia kiasi kilichowasilishwa hadi Februari.

“Ukisema Februari mwaka unakuwa haujakamilika, kuna miezi mingine inabakia, utekelezaji wa bajeti unakuwa unaendelea hadi Juni, nikushauri tafuta bajeti ya mwaka mzima halafu tuzungumze,” alisema Kairuki.

Kwa mujibu wa hotuba za bajeti za Tamisemi za miaka tofauti, Sh57.7 bilioni zimeongezwa katika ugharamiaji wa elimu bila malipo kati ya mwaka 2019/20 hadi mwaka 2022/23 kutoka Sh288.7 bilioni hadi Sh346.49 bilioni, mtawaliwa.

Ongezeko hilo la fedha linaendana na kasi ya udahili wa wanafunzi katika shule za umma na ujenzi wa shule mpya unaofanywa kila mwaka.

Jambo hilo limewafanya wadau wa elimu kupaza sauti wakitaka fedha itolewe kama ilivyopangwa ili kuboresha elimu na kuepuka athari zinazoweza kupatikana, ikiwamo wanafunzi kufanya vibaya katika masomo.

Utekelezaji wa sera ya elimu bila malipo mwaka 2016 unahusisha ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia, kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa taaluma shuleni kwa kutoa posho ya madaraka kwa wakuu wa shule za msingi, sekondari na maofisa elimu kata.

Akizungumzia suala hilo, Mtafiti wa masuala la Elimu, Muhanyi Nkoronko alisema licha ya fedha kutolewa, ukadiriaji wake hauakisi mahitaji ya sasa kwa kuwa viwango vinavyotolewa vilikadiriwa zaidi ya miaka mitatu nyuma.

“Haviakisi (viwango) mahitaji na upandaji wa gharama za maisha kwa sasa, shule nyingi zinatekeleza mahitaji yake kwa kusuasua,” alisema Nkoronko.

Alisema utoaji wa fedha usioendana na mahitaji halisi unawafanya viongozi wa shule kupata wakati mgumu kiutendaji, hasa wakati wa mtihani. Mhadhiri wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu cha Dar es Salaam (Duce), Luka Mkonongwa alisema ikiwa nchi inataka matokeo mazuri katika elimu ipo haja ya kuitekeleza bajeti kama ilivyo bila kuipunguza.

“Kwa sababu hata inayopitishwa si kwamba inakidhi mahitaji yote, hapana, inahitajika zaidi ya hapo, sasa hata kidogo kilichotengwa kwa ajili ya masuala ya msingi hakiletwi, maana yake hatupo serious na tuwe tayari kupokea matokeo yoyote,” alisema Mkonongwa.

Alisema bajeti ndiyo inayotoa dira ya maendeleo ya sekta na utekelezaji wa mipango mbalimbali ya sekta hivyo fedha isipotolewa kulingana na bajeti iliyoombwa mipango mingi inakwama.

Ochola Wayoga, ambaye ni Mratibu wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) alisema umefika wakati elimu inatakiwa kuwa kigezo cha kumpigia kura mgombea kwa kile alichokieleza kuwa kama hali itaendelea kuwa hivi kwa miaka mitano ijayo nchi itakuwa kwenye hali mbaya.

“Rasilimali zilizotakiwa kutumika katika ruzuku hazitumiki ipasavyo, ukiangalia ripoti ya CAG (Mdhibiti mkuu na Mkaguzi wa hesabu za Serikali) kuna takribani Sh2 trilioni zimetumika vibaya, ukipeleka hii fedha katika elimu hutasikia mtoto amekosa dawati, ninakuhakikishia ikitumika vizuri hii fedha asilimia 70 ya changamoto tunazokutana nazo sijui walimu, vyoo haitakuwepo,” alisema Wayoga.

Alisema kama nchi bado haijaamua kupambana na maendeleo ya nchi, hususan katika elimu, huku akieleza kuwa hata sekta ya kipaumbele bado haijawekwa bayana.


Hali ya utoaji wa fedha

Kwa mujibu wa hotuba mbalimbali za Tamisemi, kumekuwa na uelekezaji wa viwango tofauti vya fedha kati ya mwaka na mwaka.

Kwa mfano, katika bajeti ya mwaka 2019/20 Serikali ilipanga kutoa Sh288.7 bilioni katika kutekeleza mpango wa elimu bila malipo.

Lakini hadi Februari 2020, Serikali ilitumia Sh169.67 bilioni kwa ajili ya kutekeleza mpango huo. Kati ya fedha hizo Sh81.68 bilioni zilitumika shule za msingi na Sh 87.99 bilioni kwa sekondari.

Bajeti hiyo pia ilieleza kuwa, kufuatia ongezeko la wanafunzi linaloshuhudiwa, fedha iliyotengwa katika programu hiyo iliongezwa kwa Sh9.6 bilioni katika mwaka wa fedha 2020/21. Hiyo ikiwa na maana kuwa kwa sasa zilitengwa Sh298.13 bilioni kati ya fedha hizo, Sh137.63 bilioni zilielekezwa msingi na Sh160.49 bilioni zilienda sekondari.

Hata hivyo, katika bajeti ya mwaka 2021/2022, ilielezwa kuwa kati ya Julai, 2020 hadi Februari 2021, Serikali ilitoa Sh166.44 bilioni pekee kwa ajili ya kutekeleza mpango huo. Kati ya fedha hizo, Sh80.51 zilielekezwa elimu msingi na Sh85.93 sekondari.


ACT Wazalendo

Wakati utoaji ruzuku ukiwa wa kusuasua, Chama cha ACT-Wazalendo kiliitaka Serikali kuongeza kiwango cha ruzuku kwa shule za msingi na sekondari hadi Sh25,000 na Sh58,000, mtawaliwa ili kuboresha viwango vya ubora wa elimu inayotolewa.

Msemaji wa sekta ya Tamisemi na Maendeleo Vijijini wa ACT, Kulthumu Mchuchuli alisema hayo wakati akichambua hotuba ya bajeti ya Tamisemi iliyowasilishwa bungeni Aprili 14, 2023.