Fahamu jinsi ya kujilinda na saratani ya shingo ya kizazi

Muktasari:

  • Saratani ya shingo ya kizazi inatajwa kuwa ni saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi duniani.

Saratani ya shingo ya kizazi inatajwa kuwa ni saratani inayoongoza kwa kusababisha vifo vya wanawake wengi duniani.

Inakadiriwa asilimia 85 ya vifo hivyo hutokea katika nchi zinazoendelea. Kwa Tanzania, wastani wa wanawake 6,241 huugua saratani hiyo kila mwaka na 4,355 kati yao hufa, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2010.

Ripoti hiyo ilibainisha saratani ya shingo ya kizazi ndiyo ya kwanza kwa wanawake Tanzania na saratani namba moja kwa wanawake walio kati ya umri wa miaka 15 hadi 44.

Akizungumza na jarida la afya la Mwananchi, Daktari bingwa wa magonjwa ya saratani kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Dk Nanzoke Mvungi anasema mara nyingi saratani hiyo ikiwa inaanza haionyeshi dalili yoyote, hivyo mgonjwa hawezi kuchukua hatua kukabiliana nayo wakati huo.

Dk Mvungi anasema saratani hiyo na ya matiti zinakua kwa kasi nchini ikilinganishwa na miaka ya nyuma, kwani kwa takwimu za sasa za ORCI zinaonyesha saratani inayoongoza kwa wanawake ni ya shingo ya kizazi kwa uwepo wa wagonjwa asilimia 33, ikifuatiwa na saratani ya matiti ambayo ni asilimia 12 kwa nchi nzima. “Kwa takwimu hizi inadhihirisha kuwa tatizo ni kubwa nchini, hivyo tunapaswa kulivalia njuga, kwani wanawake wote wapo hatarini endapo wataanza kushiriki ngono isiyo salama katika umri mdogo,” anasema.

Vihatarishi vya saratani

Anasema ufanyaji wa ngono na wanaume wengi kwa wasichana wenye umri mdogo ni moja ya vihatarishi vya saratani ya shingo ya kizazi.

“Hapa tunaamini kupitia ngono isiyo salama itakuwa imebeba wadudu wa virusi vya HPV ambao wanaelezwa kuwa na mchango mkubwa wa mabadiliko wa vimelea vilivyopo kwenye mlango wa kizazi wa mwanamke, hasa akiwa katika umri mdogo wa miaka tisa hadi 15,” anasema.

Anasema virusi hiyo vikifanikiwa kuingia katika mlango huo wa kizazi vinafanya mabadiliko hayo kwa muda wa miaka 10 hadi 20 na ndipo mtu hubainika kupata saratani hiyo.

“Wakati naanza kazi kama miaka 10 iliyopita saratani hizi za shingo ya kizazi zilikuwa zikionekana kwa wanawake wenye umri wa miaka 60, lakini miaka ya karibuni tunaona wagonjwa hata wakiwa na miaka 28.

“Hivyo kuna haja ya kutoa elimu kwa watoto wa kike kujitunza, kutoanza ngono mapema wakiwa na umri mdogo, hii inatokea zaidi vijijini, kwani kuna watoto wanaolewa wakiwa na umri mdogo na kuanza ngono mapema, hivyo kumuweka kwenye hatari ya kupata saratani,” anasema.

Viashiria vingine vya saratani hiyo ni uvutaji sigara, unywaji wa pombe kupita kiasi, kutokufanya mazoezi, kuwa na magonjwa ya zinaa pamoja na ulaji wa vyakula vyenye wanga zaidi.

“Ndio maana tunashauri watu kula mlo kamili, ili kujikinga na hatari ya kupata saratani ya shingo ya kizazi,” anasema.

Daktari bingwa mbobezi wa magonjwa ya wanawake na uzazi kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Dk Matilda Ngarina anasema kutokana na watu kukosa uelewa husababisha kupokea wagonjwa wakiwa katika hatua mbaya ya ugonjwa huo.

“Steji ambayo wagonjwa hao huja tunachoweza kuwasaidia ni kuwapa mionzi au chemotherap, lakini watu wangekuwa na uelewa wa haraka wa kuja kufanya vipimo mapema huu ugonjwa ungepungua kwa sababu ukigundulika mapema unatibika na unapona,” anasema Ngarina.


Dalili zake

Dk. Ngarina, ambaye pia ni Rais wa madaktari bingwa wa magonjwa ya wanawake Afrika Mashariki anasema moja ya dalili ni kutokwa na damu kwa utaratibu usioeleweka.

“Tunaelewa wanawake tunapata damu za mwezi na mzunguko unaeleweka, sasa pale unapoona damu zinaanza kutoka ovyo ovyo au inatoka wakati wa kujamiiana hiyo ni dalili ya kwanza mbaya,” anasema Dk Ngarina.

Anasema dalili nyingine ya saratani hiyo ni kutokwa na maji yanayonuka ukeni (kama mtu amejikojelea).

“Hizo dalili mbili kubwa ambazo unatakiwa kuzifuatilia, ukiziona unatakiwa kwenda kituo cha afya kupima, ili kuanza matibabu kama utabainika kuwa na saratani hiyo,” anasema.

Anasema kwa wanawake waliofikia ukomo wa hedhi, wakianza kuona tena damu watambue hiyo pia ni moja ya dalili ya hatari ya saratani ya shingo ya kizazi.

“Kwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, nusu ya wanawake waliolazwa kwenye wodi za magonjwa ya kike wana saratani ya shingo ya kizazi na Ocean Road nusu ya waliokuja kupata mionzi kwa ajili ya matibabu ni kinamama wenye saratani ya shingo ya kizazi,” anasema.

Dk. Ngarina anasema kutokana na hali hiyo, ni wazi sasa saratani hiyo inaongoza kwa kudhuru wanawake wengi Tanzania.

Hata hivyo, anasema moja ya changamoto iliyopo katika kuwatibu watu waliopata saratani hiyo ni kuogopa mionzi, hivyo wengi wao hukimbia hospitali na kwenda kutafuta dawa za miti shamba.

“Watu wengi wanaokuja hospitali wanaogopa mionzi na dawa za kansa, hivyo huishia kufa kwa kutumia dawa za miti shamba na kutotibiwa kwa wakati,” anasema.

Anashauri kinachopaswa kufanyika ni kuongeza uelewa kwa jamii ambayo itaona mtaji wao wa maisha upo katika afya, hivyo kujenga tabia ya kupima mara kwa mara.

Anasisitiza watoto wa kike wenye umri kuanzia miaka 11 kabla hawajaanza kushiriki ngono wapatiwe chanjo, kwa kuwa kirusi kinachoeneza saratani ya shingo ya kizazi kinaweza kudhibitiwa na chanjo inayotolewa na Serikali kupitia ORCI.

“Chanjo kuhusiana na HPV tulianza kutoa Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro kwa wanafunzi wote waliokuwa shule za msingi, ni matumaini yangu jambo hilo litakuwa endelevu, tukifanikiwa kuwachanja watoto wetu kwa kiasi kikubwa tutatokomeza ugonjwa huu,” anasema.


Massana watoa elimu

Mkurugenzi wa Tiba Hospitali ya Massana, Dk Robert Josiah anasema wanatoa elimu kuhusu saratani hiyo baada ya kubaini kuwepo kwa wanawake wengi wanaosumbuliwa na ugonjwa huo, huku wengi wao wakishindwa kupata tiba kwa kukosa elimu sahihi.

“Wanawake wanatakiwa kwenda vituo vya afya mara kwa mara kufanya uchunguzi wa awali, kwani ikigundulika mapema saratani hii inatibika,” anasema.