Gardner wa Clouds kuagwa kesho Dar, kuzikwa Jumanne Rombo

Muktasari:

  • Kesho Aprili 22, 2024 mwili wa Gardner utaagwa kwenye viwanja vya Leaders Club vilivyopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Dar es Salaam. Mwili wa aliyekuwa mtangazaji wa kituo cha redio cha Clouds FM, Gardner Habash utaagwa kesho jijini Dar es Salaam na kuzikwa Jumanne Aprili 23, 2024 mkoani Kilimanjaro.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Kampuni ya Clouds Media Group, mwili huo atazikwa kijijini kwao Kikelelwa, kata ya Tarakea, wilayani Rombo, mkoani Kilimanjaro.

Gardner amefariki dunia jana Aprili 20, 2024 saa 11 alfajiri katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKIC) jijini Dar es Salaam alipokuwa anapatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa ratiba hiyo, leo Aprili 21, 2024 mwili wa Gardner utapelekwa nyumbani kwake Kijitonyama saa 12.00 jioni ambako kutakuwa na ibada ya faraja kwa familia.

Kesho Aprili 22, 2024 saa mbili asubuhi mwili utapelekwa katika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mbezi kwa ajili ya ibada.

Baadaye ya ibada mwili huo utapelekwa kwenye viwanja vya Leaders Club vilivyopo Kinondoni kwa ajili ya umma kutapata nafasi ya kushiriki kutoa heshima za mwisho.

Shughuli hiyo inatarajiwa kukamilika saa nane mchana itakapoanza safari ya kwenda Rombo mkoani Kilimanjaro.

Gardner ambaye ni baba mzazi wa msanii wa Bongofleva, Malkia Karen, hadi anaugua alikuwa anatangaza kipindi cha Jahazi akiwa na wenzake wawili, Musa Hussein na George Bantu.

Gardner ni mtangazaji wa pili kufariki dunia akiwa anakitumikia kipindi cha Jahazi, baada ya Ephraim Kibonde, aliyefariki dunia Aprili 2021 akiwa anatibiwa katika Hospitali ya Bugando, mkoani Mwanza.

Gardner alianza utangazaji wa redio akiwa Clouds FM, kisha aliondoka na kujiunga na Times FM alikotangaza kipindi cha Masikani.

Safari yake ya utangazaji iliendelea alipohamia E FM na kuanzisha kipindi cha Ubaoni, kabla ya kurejea Clouds FM mwaka 2016.

Ukiacha utangazaji, Gardner amewahi kuwa meneja wa mwanamuziki Lady Jaydee ambaye pia alikuwa mke wake.

Ndoa ya wawili hao ilidumu kwa takribani miaka 10 kabla ya kutalikiana.