Hivi hapa vipaumbele bajeti ya Wizara ya Nishati

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko akizungumza wakati akiwasilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Nishati na Taasisi zake kwa mwaka 2024/25 leo Jumatano, Aprili 24, 2024. Picha na Merciful Munuo

Muktasari:

  • Kwa kiasi kikubwa vinawiana na vipaumbele vya mwaka wa fedha 2023/24.

Dar es Salaam. Katika mwaka wa fedha 2024/25, utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Nishati utaongozwa na vipaumbele vinavyojikita katika kuendelea kutekeleza miradi ya uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme.

Hayo yamo kwenye hotuba ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk Doto Biteko, alipowasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka 2024/25 bungeni jijini Dodoma leo Aprili 24, 2024

Dk Biteko amesema miongoni mwa yatakayofanyika ni kufikisha gridi ya Taifa katika mikoa iliyosalia, kupeleka nishati vijijini, ikiwemo katika vitongoji; kutekeleza miradi ya kielelezo na kimkakati ya mafuta na gesi asilia ikiwamo wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG).

Pia ujenzi wa bomba la kusafirisha mafuta kutoka Hoima, Uganda hadi Tanga, Tanzania (EACOP).

“Wizara itaendelea kutekeleza na kusimamia shughuli za utafutaji na uendelezaji katika vitalu vya kimkakati na wawekezaji; usambazaji wa gesi asilia viwandani, katika taasisi na majumbani na kuimarisha matumizi ya CNG katika magari,” amesema.

Vipaumbele vingine amesema ni kuendelea kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini, na upatikanaji wa nishati ya mafuta vijijini kupitia uanzishwaji wa vituo vya mafuta katika maeneo hayo.

Dk Biteko amesema pia kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli, na ufanisi katika kushughulikia upatikanaji wa bidhaa hizo.

Dk Biteko ametaja vipaumbele vingine kuwa ni kuimarisha uwekezaji na ushiriki wa aekta binafsi katika shughuli za utafutaji na uendelezaji wa mafuta na gesi asilia, uzalishaji na usambazaji wa umeme.

Pia kuendelea kuimarisha utoaji wa huduma, tija na ufanisi katika uendeshaji wa taasisi na mashirika yaliyo chini ya wizara hiyo.

Mashirika hayo ni Tanesco, TPDC, Ewura, Pura, PBPA pamoja na kampuni tanzu.

“Wizara itaendelea kuimarisha ushiriki wa wazawa katika shughuli za mafuta na gesi asilia na rasilimali watu ya wizara na taasisi zake na upatikanaji wa vitendea kazi muhimu,” amesema.


Vipaumbele 2023/24

Utekelezaji wa majukumu ya wizara hiyo kwa mwaka 2023/24 uliongozwa na vipaumbele vilivyojikita katika kukamilisha miradi ya uzalishaji na usafirishaji wa umeme.

Kwa mujibu wa Dk Biteko, pia vilijikita katika kuendelea kuchukua hatua za kuimarisha uzalishaji, usafirishaji na usambazaji wa umeme nchini.

Kuendelea kupeleka umeme vijijini, vitongojini, katika visiwa na maeneo yaliyo mbali na gridi ya Taifa, vituo vya afya na pampu za maji, wachimbaji wadogo wa madini, maeneo ya kilimo na viwanda na katika shule na mahakama za mwanzo vijijini.

Vingine vilikuwa kutekeleza mikakati na programu za kuimarisha matumizi ya nishati safi ya kupikia nchini.

“Vipaumbele vingine vilikuwa ni kuanza maandalizi ya utekelezaji wa mradi wa kuchakata na kusindika gesi asilia kuwa kimiminika (LNG)” amesema.  Mradi wa EACOP pia ulikuwapo, pamoja na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika vitalu vya kimkakati, usambazaji wa gesi asilia viwandani, majumbani na nchi jirani, kuimarisha matumizi ya CNG kwenye magari, na kunadi vitalu vilivyo wazi katika maeneo ya nchi kavu na baharini ili viendelezwe.

Amesema wizara ilielekeza pia nguvu katika kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na uhakika wa upatikanaji wa bidhaa za mafuta ya petroli, kutokana na umuhimu wake katika ukuaji wa shughuli za kiuchumi na kijamii na kuimarisha ufanisi katika kushughulikia bidhaa hizo.