Hivi kweli Rais anatukanwa polisi mpo kimya?

Wiki iliyopita, tumemsikia Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda akisema wapo watu, wakiwamo mawaziri wanaowalipa watu fedha ili kumtukana Rais Samia Suluhu Hassan mitandaoni, najiuliza hivi kutukana si ni kosa la jinai? Mbona polisi wetu wako kimya?

Kauli ile kama ina ukweli na siyo kutafuta kick (umaarufu), inavivua nguo vyombo vyetu vya usalama kama Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) na Jeshi la Polisi, lakini kama ni ya kutunga, imeleta uchonganishi mkubwa kati ya Rais na mawaziri wake aliowateua.

Kwanza ni lazima niweke wazi kabisa kuwa kuna tofauti kubwa kati ya ukosoaji mzuri wa Rais na kumtukana Rais kwa sababu ukosoaji haujawahi kuwa kosa la jinai hata siku moja katika nchi yetu, bali kumtukana mtu ni kosa la jinai.

Bahati mbaya sana baada ya kuibuka kizazi cha uchawa katika nchi yetu ambacho sijui kinalipeleka wapi taifa letu linalozalisha wasomi wa ngazi mbalimbali milioni 1.2 kila mwaka, wamegeuza ukosoaji ni kosa la jinai na kukosa uzalendo, bali kusifia ni uzalendo.

Ni kutokana na dhana hiyo, hivi sasa wapo wasomi hadi ngazi ya Profesa na wenye shahada ya uzamivu (PhD), wanasiasa, watendaji serikalini na hadi viongozi wa dini wameamua kuwa chawa ili kumpamba Rais ili kujipendekeza kupata mkate wa siku.

Turudi sasa kwenye kauli ya RC Makonda kwamba kuna watu wanalipwa ili kumtukana Rais mitandaoni ambao anawafahamu, wakiwamo mawaziri, kama ina ukweli ama la, au naye ni miongoni mwa wale wanaotumia majukwaa kumpamba Rais ili kupata mkate.

Akiwa katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 40 ya aliyewahi kuwa Waziri mkuu wa Tanzania, Edward Moringe Sokoine yaliyofanyika Aprili 12 huko Monduli mkoani Arusha, RC Makonda alimweleza Rais Samia na Taifa kuwa ana majina ya wanaomtukana.

Nikimnukuu akiongea mbele ya Rais, RC Makonda alisema wapo watu wanatumia fedha kuwaagiza watu kumtukana Rais Samia kwenye mitandao na kuwataka waache mara moja kwa sababu anawafahamu kwa majina na miongoni mwao wapo mawaziri.

RC Makonda alienda mbali na kuahidi kuwataja kwa majina Jumatatu ya Aprili 15 endapo watu hao, wakiwamo mawaziri, wataendelea kutuma watu wa kumtukana Rais Samia ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu wa majeshi yetu ya ulinzi na usalama nchini.

Sasa anatokea RC Makonda, ama kwa kujua ama kutokujua, anautangazia umma wa Watanzania kuwa kuna watu wanalipa watu pesa ili kumtukana Rais wakati kitendo hicho ni kosa la jinai chini ya kifungu cha 89(1)(b) cha kanuni ya adhabu sura ya 16.

Chini ya sheria hiyo iliyofanyiwa marejeo 2022, adhabu ya kosa hilo ni kifungo cha miezi sita jela, lakini RC Makonda anataka kutuaminisha kuwa watu wanaomtukana Rais mitandaoni, tena anaowafahamu kwa majina, wako uraiani wakila bata kwa mrija.

Lakini ukiacha sheria hiyo, tuna kifungu cha 16 cha sheria ya makosa ya kimtandao (Cyber Crime Act) ya mwaka 2015 ambayo pia inakataza matusi mitandaoni na adhabu yake ni faini ya Sh5 milioni au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote viwili.

Sasa RC Makonda anawafahamu wanaomtukana Rais ambalo ni kosa, tunajiuliza hivi ni kweli hajui ni wapi pa kutoa taarifa za kosa hilo? Alishindwa kumnong’oneza Rais kwamba waziri fulani ndiye anakusaliti, anatuma watu mtandaoni kukutukana.

Kwamba RC Makonda alishindwa kuvijulisha vyombo vyetu vya usalama kwa maana ya TISS na Jeshi la Polisi, au hata kumnong’oneza Katibu Mkuu Kiongozi ama Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) au Mkuu wa Majeshi (CDF) kuwa waziri fulani ndiye anamtukana Rais?

Nchi yetu inaongozwa kwa utawala wa sheria ambao kwa lugha ya kawaida kabisa, maana yake hakuna mtu aliye juu, au nje ya mamlaka ya sheria, kuanzia Rais wa nchi, mawaziri mpaka mimi mnyonge, sasa inakuwaje wanaomtukana Rais waachwe tu?

Mimi kwa akili yangu hii ya Kipare, nilitarajia mara baada ya kauli ile, mamlaka zingemwita RC Makonda na kumhoji na alazimishwe sio tu kutaja majina ya hao anaosema wanatuma watu kumtukana Rais, bali atoe na ushahidi, siyo blaa blaa.

Jambo hili si dogo hata kidogo, kwamba lichukuliwe tu kama kauli ya kisiasa, hapana, kwa sababu RC Makonda anachosema Rais amezungukwa na wasaliti kwenye Baraza la Mawaziri aliloliteua yeye mwenyewe, lakini kama hana ushahidi achukuliwe hatua.

Umma unatamani kuwajua hao mawaziri na tuambiwe na ushahidi, maana isije kuwa ni vita ya madaraka kuelekea uchaguzi mkuu 2025 ya watu kuanza kuchafuana, hivyo Rais na vyombo vya usalama visikubali jambo hili likapita hivihivi. Umma unahitaji maelezo.

Mwandishi wa uchambuzi huu anapatikana kwa namba: 0656600900