Hivi ndivyo alivyomuua bodaboda aliyesoma naye na kumpora pikipiki

Mwanafunzi chuo kikuu amnyonga mwenzake

Muktasari:

  • Tukio hilo lilitokea Oktoba 8, 2019 katika Kijiji cha Msanga Zalala kilichopo Wilaya ya Kisarawe Mkoa wa Pwani na watu watatu –  Isihaka Mohamed, Abuu Mchagua na Nurdin Mohamed – walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuua kwa kukusudia.

Dar es Salaam. “Mimi nikaendelea kumkaba na ule mkanda akakojoa na kukata roho,” hii ni sehemu ya maelezo ya Isihaka Mohamed akikiri kumuua dereva bodaboda, Rashid Said ambaye wakati wa uhai wake, waliwahi kusoma shule moja na mshtakiwa.

Tukio hilo lilitokea Oktoba 8, 2019 katika Kijiji cha Msanga Zalala kilichopo Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani ambapo watu watatu – Isihaka Mohamed, Abuu Mchagua na Nurdin Mohamed – walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kuua kwa kukusudia.

Hata hivyo, katika hukumu aliyoitoa Aprili 15, 2024, Jaji Arnold Kirekiano wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, aliwaachia huru mshtakiwa wa pili na tatu na kumtia hatiani Isihaka, kisha kumhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.

Marehemu Said alikuwa dereva wa pikipiki za abiria katika maeneo ya Chanika wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam, akiishi na baba yake mzazi Saidi Rashid.

Alikuwa na utaratibu wa kurejea nyumbani jioni lakini Oktoba 8, 2019 hakurejea kama ilivyo kawaida na jitihada za kumtafuta siku hiyo hazikuzaa matunda hadi Oktoba 12 mwili wake ulipopatikana vichakani, eneo la Msaranga Zalala.

Uchunguzi wa mwili wake ulibaini sababu za kifo ni kukosa pumzi kulikotokana na kunyongwa.

Upande wa mashtaka ulikuwa unadai kuwa washtakiwa hao watatu ndio waliomkodi na wakiwa njiani walimnyonga hadi kumsababishia kifo.


Ushahidi ulivyokuwa

Upande wa mashtaka ukiongozwa na mawakili wa Serikali, Laura Kimario, Amina Macha na Doris Kawoja uliita mashahidi tisa akiwamo baba mzazi wa marehemu aliyeeleza namna siku ya tukio mwanae hakurudi nyumbani na alivyotoa taarifa kwa kiongozi wa mtaa.

Kiongozi huyo, Hashim Mvungi ndiye aliyemdokeza kuwa mwanae alikuwa amekodiwa na rafiki yake wa zamani ambaye waliosoma wote shule moja ambaye ni mshtakiwa wa kwanza, Isihaka na baadaye polisi walifanikiwa kumkamata mshtakiwa wa tatu, Nurdin.

Alisema baada ya mshtakiwa huyo kukamatwa, Oktoba 12, 2019 aliwaongoza polisi hadi eneo ulipokuwa mwili wa Said na pembeni yake walikuta mkanda uliotumika kumkaba.

Ushahidi wake huo ulioana na wa shahidi wa nane, Juma Mayamba ambaye alisema Oktoba 8, 2019 alikuwa na marehemu Said Chanika Mwisho.

Akasema ilipofika Saa 7:00 mchana, alifika Isihaka na watu wengine wawili ambao hakuwafahamu wakamkodi Said na wakaelekea uelekeo wa Homboza.

Akasema wakati wanamtafuta Said baada ya kutoonekana, walienda hadi Msanga Zalala kulikoelezwa kwamba Isihaka alionekana.

Kwa upande wake shahidi wa tano, Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Leonard yeye aliieleza mahakama namna alivyoongoza timu iliyochukua mwili wa Said kutoka eneo la tukio walikoonyeshwa na mshtakiwa wa tatu.

Shahidi wa tisa ambaye ni askari mgambo, Maulid Mpolya aliyemkamata mshtakiwa Oktoba 15,2019 akiwa Rufiji na mshtakiwa wa pili, Abuu Mchagua baada ya kukamatwa na wananchi wenye hasira wakiwatuhumu kuiba kilo 50 za korosho kijijini hapo.

Walisafirishwa siku hiyohiyo hadi Kisarawe na siku hiyohiyo mshtakiwa wa kwanza aliandikiwa maelezo yake ya onyo na shahidi wa saba, Sajini Dickson mwenye namba F718 ambaye alisema katika maelezo hayo, mshtakiwa alikiri kumuua Said.

Katika utetezi wake, mshtakiwa wa kwanza, Isihaka aliyekamatwa Oktoba 13, 2019 na kupelekwa Kituo cha Polisi Kisarawe, alidai kuwa aliteswa na kulazimishwa kukiri kosa la mauaji ambalo hakuwahi kulitenda na wala alikuwa hamfahamu marehemu.

Mshtakiwa wa pili, alisema alikamatwa Oktoba 13, 2019 eneo la Majumba Sita akituhumiwa kucheza kamari na kupelekwa Kituo cha Polisi Kisarawe lakini hakushiriki katika kumuua Said wala alikuwa hamjui na pia alikuwa hawajui washtakiwa wenzake.

Mshtakiwa wa tatu, Nurdin Mohamed, yeye alijitetea kuwa alikamatwa Oktoba 12, 2019 na wananchi wakimtuhumu kumjeruhi mtu aliyemtaja kuwa ni Said Gesi na kupelekwa Kituo cha Polisi na kukanusha kuhusika na mauaji wala kumkodi Said.

Pia, alikanusha ushahidi wa Jamhuri kuwa Oktoba 12, 2019 aliwaongoza polisi hadi mahali mwili wa marehemu ulipokuwa.

Alidai hakuwahi kuwataja mshtakiwa wa kwanza na wa pili alipokamatwa na kupelekwa Kituo cha Polisi Kisarawe kuhojiwa, ushahidi ambayo unakinzana na maelezo ya kukiri kosa.


Maelezo ya kukiri kosa

Sehemu ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa kwanza, Isihaka inaeleza Oktoba 8,2019 Saa 7:00 mchana akiwa na wenzake, Abuu Mchagua na Nurdin Mohamed, walikodi pikipiki ya rafki yao, Rashid Said kwa nia ya kwenda kunywa pombe Msanga.

“Baada ya kumaliza kunywa pombe, tulipanga tukampore pikipiki Rashid na tulimwambia atupeleke kwenye banda la kuuza pombe barabara ya kuelekea Rufiji. Yeye ndiye alikuwa anaendesha pikipiki,” alieleza mshtakiwa huyo na kuongeza:

“Tulivyofika porini nilimkaba kwa kutumia mkanda huku pikipiki ikiwa kwenye mwendo, ndipo pikipiki ikaanguka na sisi wote tukadondoka na wenzangu wakaja kunisaidia kumshika vizuri. Mimi nikaendelea kumnyonga na ule mkanda, akakojoa na kukata roho.”

“Tukasaidiana kumbeba na kumpeleka porini na tukakata majani na kumfunika kichwani na kiwiliwili chote, tulimpekua na kumfunika kichwani na kuchukua hela aliyokuwa nayo mfukoni Sh5, 000,”anasimulia mshtakiwa katika maelezo yake hayo.


Hukumu ya kunyongwa

Jaji Kirekiano alisema ameupitia kwa umakini ushahidi dhidi ya mshtakiwa wa kwanza hususan maelezo yake ya onyo ya kukiri kosa yakimuunganisha na kosa hilo, lakini kwa mshtakiwa wa pili, amechambua ushahidi wote haoni ukimuunganisha na kosa hilo.

Jaji alisema ni jambo lililopo katika kumbukumbu za mahakama kuwa shahidi wa nane wa Jamhuri, Mayamba alieleza kuwa alimuona mshtakiwa wa kwanza akipanda pikipiki ya marehemu na alielezea namna alivyowafahamu mshtakiwa pamoja na marehemu.

“Hapa hakuna mashaka ya kumfananisha mtu. Ulikuwa ni ushahidi wa shahidi huyu kuwa marehemu alienda uelekeo ambao mwisho wa siku ndipo mahali mwili wake ulipatikana. Muda ambao alionekana akipanda pikipiki vinaunganika,”alisema Jaji.

“Kama nilivyoeleza, mshtakiwa wa tatu alikana kuwepo eneo la tukio huko Msanga Zalala siku hiyo ya tarehe 8.10.2019. Bahati mbaya hakutoa notisi mapema kuwa ataegemea ushahidi wa alibi (kutokuwepo eneo husika) kama sheria inavyotaka.”

“Kwa vile hakuna notisi iliyotolewa, basi inabaki kuwa ni utashi wa mahakama ama kuupa uzito ushahidi wake au la,” alisema Jaji Kirekiano katika hukumu yake hiyo ambayo nakala yake ilipatikana katika mtandao wa mahakama Aprili 17, 2024.

Katika kesi hii, nimezingatia ushahidi wa Jamhuri kuwa mwili wa marehemu uliachwa kwenye vichaka ukioza. Ushahidi huu ulithibitishwa na shahidi wa kwanza na wa tano ambao ndio waliochukua mwili eneo la tukio,” alieleza Jaji Kirekiano.

“Hali ya mwili ilivyokuwa ilithibitishwa pia na daktari aliyeufanyia uchunguzi. Ninachukulia kitendo cha waliomshambulia kuuacha mwili wa marehemu kwenye vichaka kama ilivyoelezwa naichukulia kama nia ovu ya wazi kutenda kosa.”

Jaji Kirekiano alisema kutokana na uchambuzi wake wa ushahidi, anaona mashtaka dhidi ya mshtakiwa wa pili na wa tatu hayakuthibitishwa kwa viwango vinavyokubalika na kuacha mashaka, hivyo anawaona washtakiwa hao hawana hatia ya mauaji.

Hivyo, Jaji alimtia hatiani mshtakiwa wa kwanza kwa kosa la mauaji ya kukusudia kinyume na kifungu cha 196 na 197 cha kanuni ya adhabu sura ya 16, kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022,  hivyo anamhukumu adhabu ya kunyongwa hadi kufa.