Hivi ndivyo mtoto wa mwezi mmoja alivyouawa

Muktasari:

  • Shahidi huyo wa pili wa upande wa Jamhuri, Casmiry Lubango ambaye ni daktari kutoka kituo cha afya Masumbwe, ameiambia Mahakama kuwa mwili wa mtoto huyo ulikutwa kwenye shimo la maji ukiwa unatoa harufu na tayari ulikuwa umevimba.

Geita. Shahidi wa pili wa Jamhuri katika kesi ya mauaji ya kukusudia ya mtoto mchanga mwenye umri wa mwezi mmoja anayedaiwa kuuawa na baba yake, ameeleza namna mtoto huyo, Anna Shemasi alivyouawa kwa kunyongwa au kubanwa pumzi.

Kesi hiyo ya jinai namba 53/2022 dhidi ya Shemas Juma, imeanza kusikilizwa jana Aprili 15, 2023 na itaendelea leo katika Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Geita, mbele ya Jaji Mfawidhi wa mahakama hiyo, Kelvi Mhina.

Shemasi anadaiwa kuua kwa makusudi mtoto huyo, Oktoba 19, 2021 huko Masumbwe wilayani Mbogwe mkoani Geita, kinyume na kifungu 196 na 197 cha Kanuni ya Adhabu sura ya 16 kama kilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.

Katika ushahidi wake, shahidi huyo, Casmiry Lubango ambaye ni daktari wa kituo cha afya Masumbwe aliyeufanyia uchunguzi mwili wa marehemu, ameieleza Mahakama kuwa mtoto huyo alikufa kwa kukosa hewa  kutokana na kunyongwa au kubanwa pumzi.

Akiongozwa na mwendesha mashtaka ambaye ni wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashitaka (NPS), Godfrey Aodupoy, shahidi huyo ameeleza kuwa mwili wa mtoto huyo ulikutwa kwenye shimo la maji ukiwa unatoa harufu na tayari ulikuwa umevimba.

“Mwili ulikutwa kwenye shimo lililojaa maji ukiwa umeshaharibika, unatoa harufu na ulikuwa umevimba, lakini haukuwa na jeraha na viungo vyote vilikuwepo.  Baada ya kumfanyia uchunguzi mwili ulipelekwa mochwari kutokana na kukosa ndugu na baada ya siku 14 ulizikwa”, amesema shahidi huyo.

Pia ameiomba Mahakama kupokea ripoti ya uchunguzi wa mwili kama kielelezo, ombi ambalo halikupingwa na upande wa utetezi na Mahakama hiyo imeipokea taarifa hiyo na kuwa  kielelezo namba moja kwa upande wa mashtaka.


Awali, shahidi wa kwanza wa upande wa mashtaka, Gaudencia Aloyce (57), mkazi wa mtaa wa Lugito wilayani Mbogwe mkoani Geita ameeleza Mahakama kuwa alipata taarifa za kifo cha mtoto huyo mchanga Oktoba 19, 2021.

Ameeleza kuwa siku hiyo, saa 2 asubuhi wakati akitoka kwenye jumuiya, alifuatwa na mtu aitwaye Anna akamueleza kuwa kuna mtoto kwenye shimo la maji lililopo karibu na ofisi za Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Hivyo, amesema kuwa alitoa taarifa kituo cha Polisi Masumbwe na askari Polisi walifika na kuuchukua mwili huo wakiongozana na daktari.

Akiongozwa na wakili Kabula Benjamini, shahidi wa tatu,  Monika Kisusia ameieleza Mahakama kuwa Agosti 2021 wakiwa nyumbani, aliitwa na Shemas Juma na kumuomba amsindikize mkewe hospitali akidai alikuwa anaumwa uchungu.

Ameeleza kuwa baada ya kufika kituo cha afya Masumbwe, mke wa Shemas aitwae Kulwa alishindwa kujifungua kwa njia ya kawaida, akafanyiwa upasuaji na kupata mtoto wa kike, lakini kidonda kilibaki kikitoa usaha na baada ya wiki moja alirudi nyumbani.

Bila kutaja tarehe amedai siku moja mtoto alikuwa akilia sana usiku, ndipo Shemas (baba wa mtoto) alidai anampeleka hospitali kwa kuwa kitovu kinatoa usaha na kwamba baadaye alirudi akidai mtoto amepelekwa Bugando kwa kutumia gari la wagonjwa.

“Kwa kuwa yule mtoto alikuwa mdogo sana tulimuuliza amemwacha vipi wakati ananyonya, naye akadai kuwa mama yake mzazi ameenda naye na kesho yake asubuhi alimchukua mkewe akidai wanaenda kumfuata mtoto hospitalini lakini hawakurudi tena”, ameeleza shahidi huyo.

Ameongeza kuwa baada ya siku kadhaa kupita, mshtakiwa alirudi kuchukua vyombo vyake, akawaeleza kuwa wamehamia wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga.

Hata hivyo, amedai kuwa Desemba 7, 2022, Kulwa James, mke wa Shemas na mama wa mtoto huyo alimpigia simu kumsalimia na alipomuuliza hali ya mtoto alimweleza kuwa hana mtoto na kwamba hajawahi kumuona, kwani aliambiwa amefariki.

Kesi hiyo iliendeshwa kwa njia ya mtandao, huku mshtakiwa  akiwa katika  gereza la Butimba jijini Mwanza, anakoshikiliwa mahabusu, kwa kuwa shtaka la mauaji linalomkabili halina dhamana kwa mujibu wa sheria.