Hizi hapa athari za saa 36 za kimbunga Hidaya

Muktasari:

  • Mvua ya milimita 316 iliyonyesha Kilwa kwa saa 36 ni sawa na mvua ya miaka mitatu kwa Mei (yaani Mei 2024, Mei 2025 na Mei 2026)

Dodoma. Mvua zilizonyesha kwa takribani saa 36 zikiambatana na upepo mkali kutokana na kimbunga Hidaya zimesababisha vifo vya watu watano na majeruhi saba, huku kaya 7,027 zenye watu 18,862 zikiathiriwa.

Mbali ya hayo, nyumba 2,098 zimeathirika kati ya hizo, 678 zimebomoka kabisa, 877 zimeharibika kiasi, na 543 zimezingirwa na maji.

Hayo yameelezwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa jijini Dodoma wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa hapo bungeni leo Mei 9, 2024 alipowasilisha taarifa kuhusu kimbunga Hidaya kilichotokea pwani ya Bahari ya Hindi Mei 3.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza bungeni jijini Dodoma leo Mei 9, 2024, alipokuwa akitoa taarifa kuhusu athari zilizosababishwa na kimbunga Hidaya. Picha na Edwin Mjwahuzi

Amesema kimbunga Hidaya kilisababisha mvua kubwa na upepo mkali katika Mkoa wa Pwani kwenye wilaya za Rufiji, Mafia na Kibiti, Mkoa wa Lindi (Wilaya ya Kilwa), Mkoa wa Mtwara (Halmashauri ya Mtwara Vijijini na Manispaa ya Mtwara-Mikindani), na Mkoa wa Morogoro (Halmashauri ya Ifakara na maeneo mengine).

Amesema miundombinu ya barabara na madaraja ilisombwa na maji, nguzo za umeme kuanguka, huku maeneo ya kutolea huduma, yakiwamo majengo ya taasisi za umma kama vile shule na vituo vya huduma za afya yameathirika.

Kimbunga Hidaya pia kilisababisha baadhi ya shughuli za kiuchumi kama vile uvuvi, kilimo na biashara kusimama.

“Vilevile, kimbunga Hidaya kimesababisha uharibifu wa chakula na madhara ya kisaikolojia,” amesema.

Majaliwa amesema kutokana na kimbunga hicho, Mei maeneo ya Kilwa na Mtwara yalirekodi kiwango kikubwa cha mvua.

“Kwa kawaida, wastani wa mvua kwa kituo cha Kilwa ni milimita 96.6 na kituo cha Mtwara ni milimita 54. Hata hivyo, kuanzia Mei 3 hadi 4, 2024, jumla ya milimita 316 za mvua zilipimwa katika kituo cha Kilwa, sawa na asilimia 327 ya kiwango cha mwezi,” amesema.

Kwa upande wa Mtwara, amesema milimita 99 zilipimwa katika muda huo ambazo ni sawa na asilimia 183 ya kiwango cha Mei.

“Kwa hali ya kawaida, mvua ya milimita 316 iliyonyesha Kilwa kwa saa 36 tu, ni sawa na mvua ya miaka mitatu kwa Mei (yaani Mei 2024, Mei 2025 na Mei 2026). Hiki ni kiwango kikubwa sana, ndiyo maana kumekuwa na madhara makubwa ya uharibifu wa miundombinu,” amesema.

Kuhusu nguvu ya upepo ulioambatana na kimbunga Hidaya, amesema katika nyakati tofauti ilifikia kilomita 140 kwa saa, kasi ambayo ni kubwa sana.

“Wakati kinafika Mafia, taarifa ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilionyesha upepo ulikuwa na kasi ya kilomita 110 kwa saa na mvua kubwa ambayo imeleta athari zilizoripotiwa,” amesema.


Athari wilayani Mafia

Wilayani Mafia, kimbunga kimeathiri kata saba za Kilindoni, Miburani, Kiegeani, Jibondo, Ndagoni, Baleni na Kirogwe.

Miongoni mwa madhara hayo ni uharibifu wa mali na miundombinu, ikiwemo ya makazi ya watu, shule, ya afya ikiwemo hospitali ya wilaya iliyozingirwa na maji,   masoko na taasisi nyingine za umma na binafsi.

“Vilevile, barabara zimechimbika na kuangukiwa na miti mikubwa, nguzo za umeme zimekatika na kuanguka, na kukosekana kwa huduma ya maji kutokana na kukosekana kwa umeme,” amesema.

Majaliwa amesema mmomonyoko wa udongo umetokea katika bandari iliyopo wilayani Mafia.

Amesema hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuwapatia hifadhi waathirika, huku Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) likifanya marekebisho ya nguzo zilizoanguka na huduma ya umeme imerejea kwa baadhi ya maeneo.


Wilaya ya Rufiji

Wilayani Rufiji vijiji sita vya Ngarambe Mashariki, Ngarambe Magharibi, Chumbi A, Chumbi B, Nyamwage, na Mbwara vimeathirika kutokana na mvua kubwa na upepo mkali.

Waziri mkuu amesema katika Kata ya Chumbi, Kijiji cha Chumbi A nyumba moja imeanguka na katika kijiji cha Chumbi B ambacho kipo jirani na kambi ya waathirika wa mafuriko, nyumba 10 zimejaa maji.

Katani Mbwara, miundombinu ya barabara ya kutoka Nyamwage kwenda Tawi, na Nyamwage kwenda Mbwara imeharibika.

“Katika Kijiji cha Mbwara, nyumba 37 zimepata athari ya kuta kuanguka na kuezuliwa mapaa,” amesema.


Wilaya ya Kibiti

Majaliwa amesema wilayani Kibiti vijiji 10 vilivyopo kwenye kata sita vimepata athari kiasi.

Amevitaja vijiji vilivyoathirika kuwa ni Mchinga, Twasalie, Kiasi, Ruma, Pombwe, Jaja, Kiechuru, Maparoni, Hanga na Mbwera Magharibi.

“Madhara yaliyotokea katika vijiji hivyo ni pamoja na kuathirika kwa miundombinu ya makazi, soko na kuanguka kwa minazi,” amesema.

Kutokana na madhara yaliyojitokeza Rufiji na Kibiti amesema wametoa huduma ya afya ya akili, msaada wa kisaikolojia na kijamii kwa waathirika 1,941 (Kibiti 1,501 na 440 wa Rufiji), kuwaunganisha waathirika 24 (Rufiji 12 na 12 Kibiti) walio kambini na huduma za matibabu.

Amesema idadi ya waathirika waliofikiwa na huduma hadi sasa ni 912 (Kibiti 472 na 440 Rufiji). Pia wametoa elimu ya usafi, ulinzi na usalama kwa mtoto kwa waathirika 1,023 (Kibiti 583 na 440 Rufiji).

Amesema wanaendelea kupokea misaada kwa waathirika akieleza wameshapokea ya malazi na chakula, yakiwamo magodoro 2,126.


Wilaya ya Kilwa

Majaliwa amesema wilayani Kilwa vijiji 13 katika kata 11 vimeathiriwa na mvua na upepo mkali, huku madhara mbalimbali yakitokea vikiwamo vifo vya watu watano.

Amesema kaya 178 zenye watu 941 zimezingirwa na maji, shule moja imezingirwa na maji, barabara kuu ya Lindi kuelekea Dar es Salaam imekatika kipande cha Somanga chenye urefu wa mita 200, kukwama kwa magari takribani 126 yakiwamo mabasi ya abiria, malori na magari binafsi.

Majaliwa amesema inakadiriwa takribani watu 2,534 walikwama.

“Kwa sasa baadhi ya abiria na magari wamerudi njia ya Lindi mjini, wengine wamesafiri kupitia njia ya Songea kuelekea Dar es Salaam, wengine kurudi Dar es Salaam kutokea Somanga,” amesema.

Amesema taasisi za umma, binafsi na makazi ya wananchi yalizingirwa na maji, ikiwemo kituo cha Songasi ambako watu 31 walizingirwa na maji katika mtambo wa kuchakata gesi.

Majaliwa amesema wilayani Kilwa watu 4,080 wameokolewa katika maeneo mbalimbali, pia kumefanyika kazi ya kurejesha hali ya miundombinu ya barabara kuu ya Lindi – Dar es Salaam.

“Tanroads (Wakala wa Barabara Tanzania) wapo eneo la tukio wanaendelea na kazi, juhudi zinafanyika za urejeshaji wa daraja la Somanga - Mtama ili magari yaliyokwama yaendelee na safari,” amesema.

Majaliwa amesema wameanzisha makazi ya muda kwenye shule za msingi za Mchakama, Ruhatwe na Ndende, ambako waathirika wamepatiwa chakula.

Manispaa ya Mtwara

Majaliwa amesema katika Manispaa ya Mtwara, vijiji sita kwenye kata sita vimeathiriwa na mvua na upepo mkali.

Amesema madhara yaliyotokea yanajumuisha nyumba 18 kubomoka na kusababisha watu kukosa makazi.

Katika Wilaya ya Mtwara, amesema kijiji cha Msimbati kilichopo Kata ya Msimbati kimeathiriwa na mvua na upepo mkali na kusababisha nyumba 21 kubomoka na nyingine 38 zimezingirwa, hivyo watu 42 kukosa makazi.

Amesema wananchi waliokosa makazi katika Manispaa ya Mtwara na Wilaya ya Mtwara Vijijini wameendelea kuunganishwa na ndugu na jamaa kwa ajili ya hifadhi ya muda. 


Halmashauri ya Mji Ifakara

Majaliwa amesema katika Halmashauri ya Mji wa Ifakara, kata nne za Viwanja 60, Mbasa, Kibaoni na Katindiuka zimeathirika kwa kiasi kikubwa kutokana na athari za mvua, zilizosababisha mafuriko baada Mto Lumemo kujaa na kumwaga maji kwenye makazi ya watu.

“Athari zilizotokea ni nyumba 43 kubomoka,  512 kuzingirwa na maji na kuharibiwa kwa miundombinu ya barabara zinazounganisha wilaya na wilaya, barabara za vijiji na mitaa, na miundombinu ya Reli ya Tazara,” amesema.

Amesema miundombinu ya barabara na makaravati hususani katika Tarafa ya Ifakara yalijaa maji hivyo kutopitika.

“Ekari 23,501 za mazao mbalimbali yakiwamo mahindi, mpunga na mengine mchanganyiko zimeharibiwa, pia mifugo imeathirika,” amesema.


Msisitizo wa Serikali

Waziri Mkuu Majaliwa amerejea msisitizo alioutoa bungeni Alhamisi Aprili 25, 2024 kuwa kamati za maafa za wilaya na mikoa ziendelee kuchukua hatua stahiki, ikiwemo kutoa tahadhari kwa wananchi na kuwasaidia kwa wakati pindi maafa yanapojitokeza.

“Leo nasisitiza, sambamba na kamati hizo, wizara zote za kisekta zinazohusika na usimamizi wa maafa ziendelee kushirikiana na kamati hizo za ngazi ya mikoa na wilaya ili kuharakisha suala la kurejesha hali,” amesema.