Jacob na Malisa wafikishwa kortini Kisutu

New Content Item (1)
New Content Item (1)

Muktasari:

  • Wadaiwa kuchapisha taarifa za uongo, jambo ambalo ni kunyume na Sheria ya Makosa ya Kimtandao.

Dar es Salaam. Meya wa zamani wa Ubungo, Boniface Jacob na mwanaharakati Godlisten Malisa,  wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka matatu ya kuchapisha taarifa za uongo kinyume na sheria.

Washtakiwa hao wamefikishwa Mahakamani hapo Leo, Jumatatu Mei 5, 2024 na kusomewa mashtaka yao na wakili wa Serikali,  Neema Moshi akishirikiana na Happy Mwakanyamale, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo.

Wakili Moshi amesema wawili hao wameshatakiwa chini ya kifungu cha 16 cha sheria ya Makosa ya Kimtandao namba 14 ya mwaka 2015.

Akiwasomea mashtaka yao, Moshi amedai kuwa washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 11805/2024.

Aprili 27 Jacob na Malisa,  waliachiwa kwa dhamana na Jeshi la Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es salaam baada ya kushikiliwa kwa siku tatu kwa tuhuma za uchochezi.

Tuhuma za uchochezi zinazowakabili wawili hao ni kuchapisha taarifa kwenye mitandao ya kijamii kuwa Jeshi la Polisi linaua raia wakihusisha kifo cha Robert Mushi, maarufu babu G.

Tuhuma hizo zilikanushwa na Jeshi la Polisi na kudai taarifa hizo zinachochea chuki kati ya jamii dhidi ya taasisi hiyo na kwamba Mushi alifariki dunia kutokana na ajali ya barabarani. mwili wake tayari umezikwa Alhamisi nyumbani kwako, Shirimatunda huko Moshi Mjini, mkoani Kilimanjaro.

Kufuatia taarifa hizo Jeshi la Polisi liliwaita wawili hao kuwahoji na Aprili 25, 2024 wakaripoti kituo cha Polisi Oysterbay lakini Mkuu wa upelelezi mkoa wa Kipolisi Kinondoni akawapeleka Ofisi za Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, baada ya kuripoti walishikiliwa kwa ajili ya mahojiano mpaka walipoachiliwa.

Wakizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya kuachiwa, wawili hao walisema hawataacha kutetea haki za raia.

Endelea kufuatilia zaidi