Je, wenza walioachana wanaweza kuwa marafiki

Muktasari:

Baadhi ya watu katika jamii wanaoachana baada ya ndoa au uhusiano kuvunjika huishia kununiana na kujenga uadui kutokana na kile kilichowatenganisha.

Baadhi ya watu katika jamii wanaoachana baada ya ndoa au uhusiano kuvunjika huishia kununiana na kujenga uadui kutokana na kile kilichowatenganisha.

Hilo huwa linaonekana hata kwa wale waliobahatika kuzaa, kwa kuwa wengine huwazuia wazazi, hasa wa kiume kuwaona watoto wao.

Mbali na changamoto hizo, wataalamu wa saikolojia na uhusiano wanasema upo uwezekano wa waliowahi kuwa wapenzi au kwenye ndoa, kujenga urafiki lakini inategemea na mazingira yanayowafanya kuwa katika hali hiyo.

“Tafiti zinaonyesha kuwa, kuna sababu tofauti za kuwa rafiki na mwenza uliyeachana naye, ikiwamo kama mna watoto, mnafanya kazi ofisi moja au mpo katika mzunguko mmoja utakaowafanya mkutane mara kwa mara,” anasema mshauri wa uhusiano, Dickson Lehmiller.

Anasema katika mazingira hayo waliokuwa katika uhusiano wanaweza kuamua kubaki marafiki.

“Wapo pia ambao tofauti na uhusiano wa kimapenzi huwa wanafurahi kuwa pamoja na kila mmoja anatamani kuwa kwenye maisha ya mwenzake,” anasema Lehmiller.

Hata hivyo, alitoa angalizo kuwa kwenye urafiki huo kuna hatari ya kumlinganisha mwenza wa sasa na mwenza wa zamani, jambo linaloweza kuhatarisha uhusiano.

“Mmemalizana lakini mkaendelea kuwa marafiki, inaweza kuwa kwa nia njema kabisa, lakini kuna uwezekano ikaleta shida kwenye uhusiano wako mpya endapo utakuwa unamlinganisha rafiki yako na mwenza wako wa sasa.

“Shida nyingine inaweza kutokea kama mtakuwa mmeachana na kuamua kuwa marafiki wakati mmoja bado ana hisia kwa mwenzie ambaye tayari ameshapata mwingine. Kwa kifupi kama unaona upo katika hali hii ni vyema ukajiepusha na urafiki huu.”


Ndoa ya Jeniffer, Affleck

Kauli hiyo ya Lehmiller imekuja wakati mastaa Jeniffer Lopez na Ben Affleck huko Marekani wakifunga ndoa baada ya kuachana miaka iliyopita.

Ndoa hiyo imekuwa gumzo kutokana na penzi kati ya wawili hawa lilivyopitia milima na mabonde na hata kufikia hatua ya kila mmoja kuendelea na maisha yake na hatimaye kurudi baada ya miaka 18.

Kabla ya Ben kurudi kwenye maisha ya Jennifer alikuwepo Alex Rodriguez na Marc Antony na upande wa pili alikuwepo Jennifer Garner na Ana de Armas, ila sasa kuna Jennifer Lopez na Ben Affleck.

Wawili hawa walikutana kwa mara ya kwanza mwaka 2001 wakati wakicheza filamu ya Gigli, na wakaingia kwenye uhusiano mwaka 2002, kabla ya kuweka hadharani mwaka 2003, hili lilifanyika baada ya ndoa kati ya Jennifer na Cris Judd kumalizika rasmi mwaka huo huo.

Penzi kati ya Jennifer na Ben lilikolea na hatimaye wakapiga hatua moja katika kurasimisha, wakaingia rasmi kwenye uchumba na hapo ndipo walipopachikwa jina la Bennifer, watu wakakaa wakisubiria kufungwa kwa ndoa yao mwaka 2003 kama ambavyo ilipangwa.

Hata hivyo, Septemba 2003, ikiwa ni siku chache kabla ya tarehe tarajiwa ya harusi wawili hawa wakatangaza kusogeza mbele ndoa hiyo na mambo yakaenda kombo zaidi kufikia Januari 2004 wakatangaza rasmi kuachana na kila mmoja kuendelea na maisha yake.

Jennifer ndiye aliyekuwa wa kwanza kuanza maisha mapya kwa kuwa Juni 2004 alifunga ndoa na Marc Antony na kupata watoto pacha. Ndoa hii ilidumu kwa miaka 10 na kufika ukomo wake mwaka 2014.

Ben naye akaingia kwenye uhusiano na Jennifer Garner uliowapeleka kwenye ndoa mwaka 2005 na kupata watoto watatu. Kama ilivyo kwa mwenza wake ndoa hii nayo ilidumu kwa miaka 13 kabla ya kuvunjika rasmi mwaka 2018.

Baada ya hapo Jennifer akatua kwenye penzi la Rodriguez ambalo liliwapeleka pia kwenye uchumba, wakavalishana pete, uhusiano huu haukufichwa, mambo yalikuwa hadharani. Wengi waliamini kinachosubiriwa ni wawili hao kufunga ndoa, mambo hayakuwa hivyo.

Aprili 15, 2021 Jennifer alitangaza kusitisha uchumba wake na Rodgriguez uliodumu kwa miaka minne, akieleza kuwa ameshindwa kumuamini mwanamume huyo kwa kile kilichodaiwa kuwa aligundua amemsaliti kwa kuwa na mwanamke mwingine.

Siku chache baada ya uamuzi huo akaanza kuonekana na Ben, ukaribu wao ukazidi kuimarika, ikawa ni kawaida kwao kusafiri wakiwa wawili.

Jambo hili lilianza kuibua uvumi kwamba wawili hao wamerudiana, kabla ya uhusiano wao kuanza kuwekwa hadharani Julai mwaka jana.

Aprili mwaka huu Ben alimchumbia kwa mara ya pili Jennifer, safari hii uchumba wao haukuachwa upoe hadi ulipowapeleka kwenye ndoa iliyofungwa Julai 17. Ndoa hiyo ilihusisha watu wachache na ilikuwa ya siri kabla ya maharusi wenyewe kuanza kuachia picha na video za harusi yao.

Kilichotokea kwa wawili hawa huenda kikatoa somo kwa watu waliochana au wanaofikiria kuachana wakatoleana maneno machafu na kujiapiza kuwa haiwezekani tena.

Upo usemi wa Kiingereza unaosema ‘Never say never’, ndio unaweza kuwa sahihi kwa muunganiko huu wa mara ya pili kati ya Jenifer na Ben.

Wanandoa hawa wameacha somo kwamba hakuna sababu ya kuwa na uadui baada ya uhusiano kuvunjika na kufikia hatua ya kuachana kwa kuwa yajayo yanaweza kuwa mazuri zaidi.

Mshauri wa uhusiano

Akizungumzia hilo, mshauri wa uhusiano, Deo Sukambi anasema upo uwezekano wa watu kuwa wanapendana lakini mazingira yasiwaruhusu kuwa pamoja kama ilivyowatokea mastaa hawa na kila mmoja akawa na maisha yake kabla ya kuamua kusikiliza kwa makini mioyo yao.

“Kuna wakati watu wanaweza kuwa wanapendana, lakini wanashindwa kuonyeshana huo upendo kwa sababu ya hali ya uchumi, vipaumbele au mazingira ya watu wanaomzunguka na hii kwa kiasi fulani inawezekana ndicho kilichotokea kwa hawa.

“Lakini pamoja na kupitia hayo, inaonyesha hawakuwahi kuwa maadui, hapa tunajifunza kwamba upo uwezekano wa uhusiano ulioshindwa kufanikiwa wakati uliopita unaweza kufanikiwa wakati mwingine.

“Hiki kitu kinawatokea watu wengi na tatizo ni kwamba huwa wanahisi kwa kuwa uhusia umevunjika basi upendo umekwisha.”

Sukambi anasema upendo huwa hauishi kirahisi, pale inapotokea mazingira ya kuruhusu ujidhihirishe ndipo uhusiano unaweza kurejea.