Jela maisha kwa kulawiti, kubaka mtoto wa miaka minane

Muktasari:

  • Mshtakiwa alitenda makosa hayo Mei 16, 2023 eneo la Mbagala Kuu.

Dar es Salaam. Mahakama ya Wilaya ya Temeke, imemhukumu kifungo cha maisha jela, baba wa kambo Ramadhan Ngauda (40) baada ya kupatikana na hatia ya kumlawiti mwanafunzi wa darasa pili mwenye umri wa miaka minane.

Pia, mahakama hiyo imemhukumu kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mtoto huyo wa kike.

Ngaudaa, ambaye ni mlinzi na mkazi wa Mikocheni, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, anadaiwa kufanya kitendo hicho wakati mama mzazi wa binti huyo ameenda kuangalia tamthilia ya Ottoman kwa jirani.

Hukumu hiyo imetolewa leo Desemba 6, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Ajiza Millanzi.

“Kwa kuzingatia ushahidi alioutoa mtoto mwenyewe mahakamani, pamoja na mashahidi wengine akiwemo kaka yake mwenye umri wa miaka 14, mahakama hii imeridhika pasina na shaka kuwa ulitenda makosa hayo na hivyo inakuhukumu kifungo cha maisha jela kwa kosa la kulawiti na kifungo cha miaka 30 kwa kosa la kubaka na hii iwe fundisho kwa watu wengine wenye tabia kama hii,” amesema Hakimu Millanzi.

Katika kesi hiyo, Ngauda alishtakiwa kwa kumwingilia kinyume cha maumbile mwanafunzi huyo umri wa miaka 8, kinyume cha kifungu cha 154 (1) (a) cha Sheria ya Kanuni za Adhabu (Penal Code).

Pia mshtakiwa huyo anadaiwa kumbaka binti huyo kinyume na kifungu cha 130 (1), (2) (e) na kifungu cha 131 cha Sheria ya kanuni ya adhabu.

Mlinzi huyo anadaiwa kutenda kosa hilo Mei 16, 2023, eneo la Mbagala Kuu.

Inadaiwa siku ya tukio, saa 4 usiku mtoto huyo alikuwa amelala chumbani na kwamba mlindi huyo ambaye ni babake wa kambo, alimfuata na kumbaka na kisha kumlawiti.

Hata hivyo, wakati kitendo hicho kinafanyika kaka wa binti huyo mwenye umri wa miaka 14, alishuhudia tukio hilo na kutoka nje na kwenda kumpigia simu mama yake, bila mafanikio.

Baada ya kuona hivyo, kaka wa binti huyo aliwagongea mlango majirani na kuwaeleza kuwa baba huyo anambaka mdogo wake.

Majirani baada ya kupewa taarifa hiyo, walienda nyumbani kwa Ngauda na kumkuta mtoto huyo akiwa amechafuka sehemu zake za siri na vipimo vya daktari vimeonyesha kuwa alikuwa ameingiliwa.

Endelea kufuatilia mitandao ya kijamii ya Mwananchi