Jela miaka saba kwa kumwambukiza mtoto virusi vya Ukimwi

Msirari Muhere (60) akiwa amejifunika kuficha sura yake wakati akitoka mahakamani akiwa chini ya ulinzi muda mfupi baada ya kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka saba kwa kosa la kumuambukiza kwa makusudi virusi vya ugonjwa wa Ukimwi mtoto wake wa kambo. Picha na Beldina Nyakeke.

Muktasari:

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara imema adhabu ya kifungo cha miaka saba jela, Msirari Muhere (60) mkazi wa Wilaya ya Tarime baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumwambukiza makusudi virusi vya ugonjwa wa Ukimwi mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka sita.

Musoma. Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mara imema adhabu ya kifungo cha miaka saba jela, Msirari Muhere (60) mkazi wa Wilaya ya Tarime baada ya kumtia hatiani kwa kosa la kumwambukiza makusudi virusi vya ugonjwa wa Ukimwi mtoto wake wa kambo mwenye umri wa miaka sita.

Hukumu hiyo imetolewa leo Mei 31, 2023 na Hakimu Mkazi Mkuu Mwenye Mamlaka ya Ziada ya Kusikiliza Mashauri ya Mahakama Kuu, Timoth Swai baada ya kuridhika bila shaka yoyote na ushahidi wa upande wa mashtaka kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo.

Uamuzi huo umetokana na rufaa iliyokatwa na upande wa Jamhuri katika shauri la jinai namba 7/2023 ilifunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Tarime Juni, 2021 na kuamuliwa Novemba, 2022 kwa mshtakiwa kutiwa hatiani na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miaka mitano jela au faini ya Sh200, 000.

Upande wa Jamhuri katika rufaa hiyo uliwakilishwa na Mawakili wa Serikali, Felix Mshama na Joyce Matimbwi.

Kutokana na kutoridhika na hukumu hiyo mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Tarime, upande wa Jamhuri ulikata rufaa ambayo leo imeamuliwa kwa mshtakiwa kuadhibiwa kwenda jela miaka sita bila faini.

‘’Kwa mujibu wa Sheria ya kuzuia maambukizi ya Ukimwa namba 28 ya mwaka 2008, mtu yeyote anayetiwa hatiani kwa kosa la kueneza makusudi virusi vya Ukimwi anatakiwa kupewa adhabu ya kifungo jela cha kati ya miaka mitano hadi 10; hakuna chaguo la faini," amesema Hakimu Swai

Mtoto alivyoambukizwa VVU

Akisoma maelezo ya kosa katika shauri la awali, Hakimu Swai amesema mshtakiwa anadaiwa kuoa mke wa pili mwaka 2018 ambaye alimkuta akiwa tayari amezaa watoto watatu ambao aliwachukua na kuishi nao pamoja na mama yao.

Amesema baadaye wanandoa hao waligombana na kutengana huku watoto wakibaki kwa baba yao wa kambo.

Hakimu Swai amesema baada ya mashauriano, wana ndoa hao walimaliza tofauti zao na kurudiana lakini baada ya muda mfupi, mama aligundua kwamba mume wake amemwambukiza mtoto wake virusi vya Ukimwi makusudi.

"Ushahidi uliowasilishwa mahakamani unaonyesha kuwa mshtakiwa Muhere alitumia sindano kuvuta damu kutoka kwa mtoto wa mke  wake mkubwa aliyeathirika kwa virusi vya Ukimwi na kumdunga mtoto wa mke wake wa pili walihitilafiana na kutengana kabla ya kumaliza tofauti zao na kurudiana,’’ amesema Hakimu Swai

Amesema uchunguzi wa kitabibu umegundua kuwa mshtakiwa Muhere na mke wake mkubwa ni waathirika wa virusi vya Ukimwi na mmoja wa watoto wao pia alizaliwa akiwa ameambukizwa virusi hivyo.

Jumla ya mashahidi sita waliitwa mbele ya Mahakama akiwemo mama na watoto wake ambao bila kuacha shaka yoyote, waliihibitishia Mahakama jinsi mshtakiwa alivyotenda kosa hilo.