Jiji Arusha matatani mishahara ya mtumishi

Wilbroad Rawile aliyeacha kazi ya daktari msaidizi wa binadamu.

Muktasari:

  • Licha ya mtumishi kuacha kazi anadaiwa mishahara ya miezi 18 inayofikia zaidi ya Sh14.92 milioni inayodaiwa kulipwa kwa Halmashauri Arusha pasipo yeye kujua

Dar es Salaam. Halmashauri ya Jiji la Arusha inadaiwa kutumia mishahara ya watumishi walioacha kazi au kufariki, akiwamo Wilbroad Rawile aliyeacha kazi mwaka 2013.

Imedaiwa Rawile ambaye ni daktari msaidizi wa binadamu na aliyeacha kazi katika halmashauri hiyo Mei 2013 na kuajiriwa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), aliendelea kulipwa mishahara ambayo hata hivyo haikuingizwa kwenye akaunti yake kwa miezi 18 inayofikia zaidi ya Sh14.92 milioni.

Rawile ambaye tangu Novemba 2, 2022 aliporejeshwa Wizara ya Afya akitakiwa kufanya kazi Hospitali ya Mount Meru, ameshindwa kulipwa mishahara hadi sasa, baada ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kumjulisha kuwa namba yake ya mshahara (cheki namba) aliyokuwa akiitumia ina deni la Sh14.92 milioni.

Kupitia barua ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ya Agosti 2023 yenye kumbukumbu Na. CFA.228/237/01P/63 na ambayo ofisi hiyo imeithibitisha, Rawile ametakiwa kushirikiana na mwajiri wake wa awali, (Halmashauri ya jiji Arusha) kueleza Sh14.92 milioni ziko wapi, ili aingiziwe mishahara ya ajira mpya.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Juma Hamsini alipoulizwa kwa simu, alisema mtumishi huyo alishafukuzwa kazi.

“Sina la kujibu, ila mtumishi huyo alishafukuzwa kazi, mbona hakwambii kama alishafukuzwa?” amehoji.

Alipoulizwa ushahidi wa mtumishi huyo kufukuzwa kazi, Hamsini alijibu: “Wewe andika chochote unachojua, mimi 2013 nilikuwa Wizara ya Sayansi na Teknolojia, wala sikuwepo Arusha.”

Hata hivyo, majibu ya Hamsini yanatofautiana na ya Katibu wa Tume ya Utumishi, Mathew Kirama aliyekiri kufahamu malalamiko ya Rawile.

Alipozungumza na Mwananchi, Kirama amesema wameshapokea malalamiko ya Rawile, lakini wanasubiri majibu ya mwajiri wake wa zamani ambaye ni Halmashauri ya Jiji la Arusha.

“Fedha ya Serikali iliyolipwa kama mshahara ikionekana haikukatiwa risiti na kurejeshwa serikalini kwa kawaida huwa inadaiwa. Sasa kama mwajiri aliitumia, anatakiwa airejeshe, kama ni mtumishi aliitumia anatakiwa airejeshe,” amesema na kuongeza:

“Ndiyo maana katika hili ngoma au mchezo uko kati ya daktari (Rawile) na mwajiri wake ambaye ni Halmashauri ya Jiji la Arusha. Wao ndio wanatakiwa wajibu hoja ya Katibu Mkuu Utumishi ili aruhusu huyu mtumishi aendelee kutumia cheque number yake,” amesema.

Amesisitiza Jiji la Arusha ndilo linatakiwa kutoa maelezo hayo.

“Hiyo wanayoeleza sijui alikuwepo mkurugenzi nani au nani, mimi leo niko hapa niliyoyakuta sijui 2000 na ngapi, yapo hapa nayashughulikia kama mtendaji niliyepo leo, siwezi kusema ilikuwa kwa katibu nani. Serikali ni continuous (endelevu) na jambo likija unali-handle kama linavyotakiwa,” amesema.

Hata hivyo, amemtaka mtumishi huyo kuwasiliana na Tume hiyo ili kujua shauri lake limefikia wapi.

“Kuna taarifa tayari tumeshazipata na suala lake linaendelea kufanyiwa kazi, kama atahitaji kujua hali halisi mahali lilipofikia awasiliane na mimi au msaidizi,” amesema.

Rawile baada ya kurudishwa Wizara ya Afya alitakiwa kurejea kwenye cheki namba aliyokuwa akitumia awali ndipo ilipobainika mishahara ya miezi 18 ilikuwa ikilipwa lakini haiingizwi kwenye akaunti yake.

Ilikuwaje?

Rawile ambaye ni daktari wa binadamu (MD), aliajiriwa na Halmashauri ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro Novemba mosi, 2009 akiwa na cheo cha daktari msaidizi daraja la II, kisha akahamishiwa Jiji la Arusha Julai 2, 2012.

Hata hivyo, ilipofika Mei 2013 alifanya usaili na kupata nafasi NHIF alikofanya kazi katika mikoa ya Dar es Salaam, Kagera Kilimanjaro na Arusha hadi Novemba 1, 2022, alipohamishwa Wizara ya Afya na kurudishwa mkoani Arusha alikopangiwa kufanya kazi katika hospitali ya Mount Meru.

Hapo ndipo mambo yalipoanza kuwa magumu, kwani Ofisi ya Rais Utumishi na Utawala Bora ilishindwa kuingiza taarifa zake kwenye mfumo wa Taarifa za Kiutumishi na Mishahara (HCMIS) baada ya kubainika ana cheki namba na ilipochunguzwa ikakutwa na deni la Sh14.92 milioni.

Fedha hizo zinatakiwa kurejeshwa Hazina na kukatiwa risiti ya kielektroniki (ERV) itakayopelekwa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

“Mpaka sasa imepita miezi 15 sina mshahara. Ilipofika Mei 2023 niliwasiliana na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, akanijibu nisimame kazi hadi suala langu litakapotatuliwa,” amesema.

Rawile amesema alipoacha kazi Jiji la Arusha mwaka 2013 alifuata utaratibu ikiwa ni pamoja na kumjulisha mwajiri kwa barua na alipoenda NHIF, hakutumia tena cheki namba ya awali.

“Nilipoajiriwa NHIF, nikamwandikia barua mwajiri wangu na kuacha ule mshahara mmoja kama inavyokuwa,” amesema.

“Nilipopeleka barua kwa mkurugenzi akaipeleka kwa Ofisa Utumishi ambaye aliniambia nipeleke barua ya wito (appointment letter) huko ulikopata. Nikampa nakala, akasema ataipekeka kwa Katibu Mkuu wa Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kujua wewe si mtumishi wa Jiji la Arusha,” amesema.

Hata hivyo, Rawile amesema kumbe mshahara uliendelea kulipwa kwa miezi 18.

Kwa mujibu wa barua ya Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ambayo Mwananchi imeiona, katika kipindi ambacho hayupo kazini, aliandikiwa barua zenye kumbukumbu Na.MD/PF 203/6 ya Mei 20, 2013 na Na. 203/7 ya Juni 11, 2013 zilizomtaka kutoa maelezo ya kutokuwepo kazini, lakini hazikujibiwa ndipo mshahara ukasitishwa.

Rawile amesema alianza kufuatilia Sh14.92 milioni zinazodaiwa kulipwa, kujua zimepelekwa wapi.

“Nikaja kwa Mkurugenzi wa Jiji, nikamweleza suala langu, yeye akaniambia kwanza mimi sikuwepo, lakini alinitaka nipeleke taarifa ya benki (jina linahifadhiwa kwa sasa) ya kipindi ambacho inadaiwa hela ilikuwa inakuja kutoka Hazina na haijulikani inakwenda wapi, ikaonekana sikuingizwa mishahara hiyo,” amesema.

Amesema mkurugenzi huyo alimkabidhi kwa ofisa utumishi mkuu ambaye naye alimpeleka kitengo cha mishahara.

“Kule wakasema ili tupate taarifa, lazima tupate kitabu ambacho watu hawakuingiziwa mishahara yao. Ilibainika fedha hizo zilipelekwa Deposit Account,” amedai.

Amedai walipofuatilia kwenye akaunti hiyo, fedha hizo hazikuwepo.

“Nikamwambia mkurugenzi, kwa kuwa fedha hizo hazipo, basi waniandikie barua nipeleke Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, ili wafungue akaunti yangu nilipwe mshahara wangu. Mpaka leo nimefuatilia ni mwaka mzima na miezi mitatu sijapewa,” amesema na kuongeza:

“Kila nikimfuata mkurugenzi anasema suala langu lina utata na kwamba endapo watanilipa watafanyiwa ukaguzi maalumu. Mara waseme suala langu ni gumu haliwezi kutatuliwa,” amesema.

Amesema amefuatilia suala lake katika taasisi za Serikali ikiwamo Taasisi Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Arusha.

“Wamesema wanafuatilia na walishawahoji Halmashauri ya Jiji kuhusu fedha hizo,” amesema.

Kamanda wa Takukuru mkoani Arusha, Zawadi Ngailo alipoulizwa amesema uchunguzi wao ni siri, hawezi kuutoa hadharani.

“Kama limeshaletwa kwetu, sitakiwi kulizungumzia na kama yeye ameleta taarifa kwenu kama chombo cha habari, ni busara mmwelekeze aje ili tuongee naye,” amesema.