Jinsi mashirika ya umma yalivyo pasua kichwa

Dodoma. Wakati madudu yakiendelea kutokea kwenye ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ofisi mdhibiti huo imetoa pendekezo la kuongeza fedha, kwa ajili ya huduma za afya ya akili kwenye jamii kutokana na upungufu wa ufanisi  aliouona kwenye wizara mbalimbali.

CAG Charles Kichere amesema hayo akiwasilisha ripoti ya mwaka wa fedha wa 2022/2023 kwa Rais Samia Suluhu Hassan leo Ikulu ya Chamwino, mkoani Dodoma.

Rais Samia akipokea ripoti ya CAG muda huu

Ombi la fedha kwa ajili ya huduma za afya ya akili limejibiwa na Rais Samia aliyesema: “Umeleta ombi jipya,” huku CAG akisema ataiwasilisha ripoti hiyo bungeni kama sheria inavyomtaka.

Ripoti hiyo pia imebainisha kuendelea kupaa kwa deni la Serikali ambalo kwa mwaka wa fedha 2022/2023 lilikuwa Sh82.25 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 15 kutoka Sh71.31 trilioni kwa mwaka wa 2021/2022.

Pia, ripoti hiyo imebainisha mashirika ya umma kuendelea kutengeneza hasara ya hadi mabilioni ya shilingi.

Mbali na hayo, ripoti imelitaja Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na mamlaka za maji kusababisha hasara kwenye miradi ya ujenzi wa barabara, ambapo mamlaka za maji hubomoa barabara kuweka miundombinu yao pale ujenzi unapokuwa umekamilika, huku Tanesco ikishindwa kuondoa nguzo na nyingine zikiwa katikati ya barabara.


Hasara mashirika ya umma

Kichere amesema amebaini mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yamepata hasara.

Baadhi ya mashirika hayo ni Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL) ambayo kwa mwaka 2022/2023, ATCL ilipata hasara ya Sh56.64 bilioni, sawa na ongezeko la asilimia 61 kutoka hasara ya Sh35.24 bilioni iliyoripotiwa mwaka uliotangulia.

“Kampuni imetengeneza hasara hii licha ya kupokea ruzuku ya Sh31.55 bilioni kutoka serikalini na imeonyesha kiasi cha Sh9.71 bilioni, ikiwa ni sehemu ya ruzuku hiyo kama mapato kwa mwaka wa fedha 2022/2023,” amesema.

Kichere amesema Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), kwa mwaka 2022/2023 limepata hasara ya Sh894 milioni, hasara hii imepungua kwa asilimia 94 kulingana na hasara ya Sh19.23 bilioni.

Shirika limetengeneza hasara hii licha ya kupokea ruzuku ya Sh4.55 bilioni kutoka serikalini na limerejesha kiasi cha Sh4.4 bilioni, ikiwa ni ruzuku ya shirika hilo kama mapato yake kwa mwaka 2022/2023.

Amesema Shirika la Reli Tanzania (TRC), nalo limepata hasara ya Sh100.70 bilioni, hasara hii imepungua kwa asilimia 47.32, ikilinganishwa na hasara ya Sh190.01 bilioni ya mwaka uliotangulia.

“Hata hivyo, hasara hiyo imetokea licha ya kupokea ruzuku ya Sh32.81 bilioni kutoka serikalini kwa ajili ya matumizi ya kawaida,” amesema.

Kuhusu kampuni ya uwekezaji ya  TanOil, amesema ilipata hasara ya Sh76.56 bilioni kwa mwaka 2022/2023, ikiwa ni ongezeko la Sh68.72 bilioni, kutoka katika hasara ya Sh7.84 bilioni iliyoripotiwa kwa mwaka uliopita.

“Hasara hii ilisababishwa na mafuta yaliyoagizwa kutoka nje kuzuiwa kwa sababu ya TanOil kushindwa kuwalipa wauzaji na gharama kubwa ya kuhifadhi mafuta ikiwa ni Sh12.9 bilioni, ikilinganishwa na Sh6.1 bilioni ya mwaka jana,” amesema.

Kuhusu Shirika la Posta Tanzania, amesema lilipata hasara ya Sh1.34 bilioni kwa mwaka 2022/2023, ikilinganishwa na faida ya Sh16.21 bilioni kwa mwaka wa fedha uliopita.

“Lakini faida ya mwaka uliopita ilitokana na mauzo ya mali za shirika na siyo biashara. Hasara ya mwaka huu ilichangiwa na kupungua huduma za EMS na gharama za uendeshaji zilizobaki karibu sawa na mwaka uliopita,” amesema.


Afya ya akili

Kichere kwenye ukaguzi wa ufanisi ameitaja Wizara ya Afya kama mfano wa ufanisi mdogo kwenye eneo la afya ya akili, akidai wizara imekuwa ikishughulika na watumiaji wa dawa za kulevya, wazee na wenye mimba za utotoni, huku ikiliacha kundi kubwa kwenye jamii likikosa huduma hiyo.

“Napendekeza kuongeza fedha kwa ajili ya huduma ya afya ya akili, hasa katika ngazi ya jamii, pia kwa ajili ya wataalamu zaidi wa afya ya akili.

Pia, kuboresha miundombinu na vifaa tiba katika vituo vya afya, kuhakikisha huduma za kisaikolojia zinapatikana kwa wakati ili kukidhi mahitaji ya jamii, pia kuanzisha vituo vya utengamano katika mikoa yote ili kuboresha ujuzi, wataalamu na kusaidia wagonjwa kupona,” amesema.

Kichere amesema ukaguzi wa ufanisi ulilenga kutathmini iwapo wizara husika inahakikisha watu wenye matatizo ya akili wanapata huduma bora na kwa wakati.

“Matokeo ya ukaguzi yameonyesha upungufu unaoathiri afya ya akili ya jamii kwa ujumla, ikiwamo utambuzi wa wagonjwa wa afya ya akili kuwa  haufanywi kwa ufanisi katika ngazi ya jamii.

“Utambuzi unaofanywa unalenga zaidi watumiaji wa dawa za kulevya, wazee, walemavu na watoto walio katika mazingira magumu na wale waliopata mimba za utotoni na kupuuza idadi kubwa ya watu wenye matatizo ya akili.

“Hii inasababishwa na ukosefu wa fedha na wataalamu wa ustawi wa jamii katika ngazi ya vijiji na mitaa. Pili, ukosefu mkubwa wa huduma za kisaikolojia katika ngazi ya jamii, huduma hizi hazipatikani kwa wakati kwa watu wenye uhitaji na hazijumuishwi kikamilifu katika mipango, bajeti na sera za afya. Hii inawaathiri sana wagonjwa wa afya ya akili na makundi mengine yenye mahitaji maalumu,” amesema.

Pia, Kichere amesema kuna uhaba mkubwa wa wataalamu, miundombinu, vifaatiba na dawa katika Wizara ya Afya.

“Wizara ya Afya haina mpango wa kuajiri wataalamu wa afya ya akili na kusababisha uhaba wa madaktari wa mfumo wa mishipa ya fahamu na wataalamu wengine,” amesema.

Kichere amesema vituo vingi havipati huduma za utengamo kwa ajili ya kuendeleza ujuzi wa kusaidia wagonjwa kupona ambapo ilibainika kuwa kati ya mikoa 28, ni mikoa mitano ndiyo yenye vituo vya utengamo kwa huduma za afya ya akili. Mikoa hiyo ni Kilimanjaro, Mwanza, Dar es Salaam, Dodoma na Kigoma.


Deni la Serikali

Akizungumzia deni la Serikali, Kichere amesema hadi kufikia Juni 30, 2023, deni la Serikali lilikuwa Sh82.25 trilioni, sawa na ongezeko la asilimia 15 kutoka Sh71.31 kwa mwaka wa 2021/2022.

“Deni hilo linajumuisha deni la ndani la Sh28.92 trilioni na deni la nje la Sh53.32 trilioni. Kipimo cha deni la Serikali kinachotumia pato la taifa kinaonyesha kuwa deni hili ni himilivu, uwiano wa kulipa madeni na mauzo ya nje ni asilimia 12.7, chini kidogo ya kiwango cha ukomo cha asilimia 15. Na uwiano wa madeni na mapato ni asilimia 14.3 chini ya kiwango cha ukomo elekezi cha asilimia 18,” amesema.


Usimamizi mapato ya kodi

Kuhusu ukaguzi wake kwenye Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), amesema kuna makusanyo ya Sh22.58 trilioni kwa mwaka wa 2022/2023, ikiwa ni ongezeko la asilimia nane ikilinganishwa na makusanyo ya Sh20.94 trilioni kwa mwaka 2021/2022.

 “Makusanyo haya yalikuwa chini kwa Sh1.07 trilioni, sawa na asilimia 4.5 ya makadirio,” amesema.

Amesema pamoja na mafanikio hayo, ukaguzi umebaini TRA inakabiliwa na changamoto katika udhibiti wa bidhaa zinazopita nchini kuelekea nchi jirani, kutokana na upungufu wa ving’amuzi vya kielektroniki.

“Upungufu huu unadhoofisha ufanisi katika kuhakikisha mizigo inayoenda nje ya nchi kupitia mipaka yetu.”

Kuhusu ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kodi, Kichere amesema mashirika nane ya umma yalikusanya mapato ya Sh23.27 bilioni nje ya mfumo wa kielektroniki ya mfumo wa malipo ya Serikali kinyume na waraka wa hazina namba 3 mwaka 2017.

Amesema kushindwa kukusanya mapato kupitia mfumo wa kielektroniki, kunaweza kusababisha upotevu wa mapato na kufifisha juhudi za udhibiti na uwazi katika mapato ya Serikali.

“Mapato yasiyokusanywa ya Sh61.15 bilioni na mapato yasiyowasilishwa benki ya Sh6.19 bilioni, ukaguzi umebaini halmashauri hazikukusanya kiasi cha Sh61.15 bilioni kutoka katika vyanzo muhimu na vikubwa, wakati Sh6.19 bilioni zilizokusanywa hazikuwasilishwa benki, hali hii inaathiri uwezo wa mamlaka wa serikali za mitaa kutekeleza miradi ya maendeleo na kutoa huduma bora kwa jamii.

“Mapato ya ndani ambayo hayakutengwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo na uendeshaji wa shughuli za vijiji au mitaa kiasi cha Sh20.23 bilioni. Mamlaka 184 za serikali za mitaa hazikutenga jumla ya Sh20.23 bilioni za mapato ya ndani kwa ajili ya miradi ya maendeleo na shughuli za uendeshaji,’’ amesema.

Hii inajumuisha Sh17.60 bilioni za miradi ya maendeleo na Sh2.63 bilioni zilizotakiwa kutumika kwa uendeshaji wa shughuli za vijiji, mitaa, kilimo, uvuvi, ufugaji na ufadhili wa miundombinu ya barabara kupitia Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura).

Katika hilo, CAG Kichere amependekeza mamlaka ya serikali za mitaa zitekeleze kwa ukamilifu maelekezo ya Serikali kwa kutenga mapato ya ndani kama ilivyohitajika na kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Kutokana na taarifa hiyo, Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na Utetezi wa Vijana la Bridge For Change, Ocheck Msuva, amesema uwazi na uwajibikaji ndio sababu kubwa ya kuendelea kuona ubadhirifu katika fedha za umma nchini.

“Wananchi lazima watambue ili kuleta utendaji thabiti sio jukumu la Rais peke yake kuleta uwajibikaji nchini, uwajibikaji unaanzia kwenye serikali za mitaa kwa watu kushiriki katika vikao ili kujua yanayoendelea kwenye mitaa na maeneo yao,” amesema.


Usimamizi wa matumizi

Kuhusu eneo la usimamizi wa matumizi, Kichere amesema ukaguzi wao ulibaini Bohari ya Dawa (MSD) ilitoa zabuni ya vifaa vya maabara vya upimaji wa Uviko-19 na kubaini kampuni iliyopewa kazi hiyo haikuwa mtengenezaji wa vifaa hivyo kinyume na masharti ya zabuni.

MSD ilinunua vifaa kutoka kwa kampuni hiyo bila ushauri wa kiufundi wa kutosha, baada ya vifaa hivyo kufika wataalamu waligundua havifai kwa mashine za nchini, hata hivyo MSD ililipa fedha zote.

“Mapendekezo ni pamoja na kuchukua hatua dhidi ya wafanyakazi husika kwa kurejesha fedha hizo za umma,” amesema.


Tanesco, mamlaka za maji

Pia, Kichere amesema ukaguzi walioufanya kwenye ujenzi wa barabara, walibaini hasara inayosababishwa na utaratibu duni kati ya taasisi za Serikali kwenye utekelezaji wa miradi.

“Jitihada za Serikali katika ujenzi wa barabara zinakwamishwa sana na utaratibu duni kati ya taasisi za Serikali, hii inasababisha ucheleweshaji upotevu wa fedha na kuathiri ujenzi wa miundombinu muhimu kwa wananchi. Taasisi hizo ni mashirika ya huduma kama vile Tanesco na mamlaka za maji yanaingilia miradi ya barabara inayosimamiwa na Tarura.

“Mfano, huko Arusha Serikali imetumia Sh194.53 milioni katika mradi wa barabara,  lakini ukaharibiwa na kazi za mamlaka ya maji ambayo ilianza tu mara baada ya barabara kukamilika. Mamlaka ya maji sasa inatakiwa kuingia gharama nyingine mpya kurekebisha barabara ambayo wameiharibu wakati wanaweka miundombinu yao,” amesema.

Kuhusu Tanesco, amesema kuna nguzo za umeme ndani ya eneo la barabara zinazojengwa kwa kuwa Tanesco haizingatii maombi ya Tarura ya kuhamisha nguzo za umeme kutoka kwenye maeneo ya barabara.

“Hii inazuia maendeleo ya miradi kadhaa yenye thamani ya jumla ya zaidi ya Sh1 bilioni,” amesema.

Wakati mwingine kuna sehemu unakuta barabara imejengwa, lakini katikati kuna nguzo ya umeme, au kwenye mabega ya barabara kuna nguzo ya umeme.

“Tunalalamika kwamba mifumo yetu haizungumzi kwa maana mifumo ya Tehama lakini pia taasisi zetu nazo pia hazizungumzi. Chanzo cha tatizo ni kukosekana kwa mawasiliano baina ya taasisi na taasisi, hali hiyo inavuruga juhudi za maendeleo na kupoteza pesa za umma,” amesema.


Mita za Tanesco

Kichere amesema ukaguzi wa Tanesco katika kubadilisha mita za umeme, ulibaini mita 100,881 kati ya mita 602,269 zilibadilishwa kabla ya kipindi cha uhai wa matumizi yake kuisha. Mita 13,493 zilibadilishwa ndani ya mwaka mmoja baada ya kufungwa kwake. Mita 94,595 zilikuwa na muda mfupi wa matumizi kati ya mwaka mmoja hadi miaka 15 kinyume na muda unaokubalika wa miaka 20 kwa mujibu wa Tanesco wenyewe.

Amesema kubadilisha mita mapema kunasababisha gharama kubwa kwa shirika.

“Napendekeza Wizara ya Nishati ichunguze sababu za Tanesco kubadili mita mapema, pia wizara ihakikishe vipimo vya ubora wa mita vinafanyika ili kuongeza ufanisi unaotakiwa na kupunguza gharama za uendeshaji za Tanesco,” amesema.