Jumuiya ya Ismailia yapongezwa kwa kuisadia jamii

Muktasari:

  • Jamii ya Kiislamu ya Waismailia wa Shia kwa kushirikiana na Taasisi za Mtandao wa Maendeleo ya Aga Khan (AKDN) zimepongezwa kwa kuzindua mpango wa huduma kwa jamii unaolenga kusaidia shule na masoko Tanzania.

Unguja. Jamii ya Kiislamu ya Waismailia wa Shia kwa kushirikiana na Taasisi za Mtandao wa Maendeleo ya Aga Khan (AKDN) zimepongezwa kwa kuzindua mpango wa huduma kwa jamii unaolenga kusaidia shule na masoko Tanzania.

Mpango huo unaojulikana kama Ismaili CIVIC Tanzania, umezinduliwa leo Septemba 26 nchi nzima, ambapo visiwani Zanzibar kwa wafanyakazi wa Jumuiya hiyo wamejitolea kufanya usafi wa mazingira katika shule ya awali ya Serikali ya Zam Zam iliyopo Mtoni Mazrui mjini Unguja.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwakilishi wa Jimbo la Mtoni, Hussein Makungu Ismail ambaye alikuwa mgeni rasmi, amepongeza jitihada hizo zinazofanywa na jumuiya hiyo akisema ni mfano wa kuigwa.

“Hili ni jambo la kuigwa na taaisisi zingine, nimeelezwa kwamba kuna shghukli mbalimbali zinaendela katika majiji mengine, lakini kusaidia shule hii hili limetupa faraja kubwa maana kama mazingira sio mazuri hata watoto hawewezi kufaulu visuri,” alisema.

Amesema histori ya shule hiyo ni kubwa na lengo ni kuona inaendelea kutoa wanafunzi wengi, “Wengi wamesoma hapa, lakini kwa mazingira iliyokuwa nayo sasa, kwakweli hayakuwa mazuri, sisi tunawapongeza sana.”

Ametumia fursa hiyo kuwataka wengine waige mfano wa jumuiya hiyo lakini pia kusaidia katika maeneo mengine yenye uhitaji maana changamoto zipo nyingi katika maeneo tofauti.

Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Aga Khan Taifa, Alnoor Jinah amesema shule hiyo ya awali ilianzishwa na Taasisa ya Aga khan kabla ya kukabidhiwa serikalini.

Amesema lengo ni kuunga jitihada za Serikali kuhakikisha mazingira yanakuwa bora zaidi ambapo wafanyakazi hao wataendelea kufanya hivyo kwa kujitolea kwa kipindi cha miezi mitatu hadi sita.

 Amesema mbali na usafi wa mazingira shughuli zingine zilizofanywa ni pamoja na kupanda miti, ukarabati na utoaji wa vifaa katika majiji matano ya Dodoma, Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya na Zanzibar yenyewe.

Naye Faki Haji Makame mwenyekiti wa kamati ya shule hiyo, amesema inakabiliwa na changamoto kadhaa ikiwemo ukosefu wa vyumba vya kutosha huku akishukuru ujio wa jumuiya hiyo kujitolea kufanya usafi na kuwawekea mazingira mazuri ya kusomea wanafunzi.

“Tuna darasa moja, lakini tungehitaji mawili, kwahiyo kuna msongamano mkubwa wa wanafunzi, pia kuna uharibifu wa mazingira licha ya kuwa na uzio wa ukuta lakini ni mfupi hivyo jamii inaozunguka hapa wanapanda na kufanya uhalifu ndani,” alisema

Mkuu wa mtandao wa kujitolea wa Ismailia, Shenaz Firoz Hussein amesema vijana mbalimbali wamekusanyika wakiwa mstari wa mbele kuongoza shghuli hiyo kwa ajili ya ustawi wa jamii inayowazunguka hapa nchini.