Kama una dalili hizi, unanyemelewa na tatizo la akili

Muktasari:

  • Kama unakosa usingizi, umeongezeka uzito ghafla au unashindwa kufanya vitu kwa usahihi na una shida ya nguvu za kiume basi chukua hatua, kwa kuwa hizo ni dalili za tatizo la akili.

Dar es Salaam. Kama unakosa usingizi, umeongezeka uzito ghafla au unashindwa kufanya vitu kwa usahihi na una shida ya nguvu za kiume basi chukua hatua, kwa kuwa hizo ni dalili za tatizo la akili.

 Ndivyo anavyosema mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Chris Mauki akisema, kumekuwa na utamaduni wa kuwaona watu wenye changamoto ya afya ya akili kama vichaa au watu wanaostahili kwenda hospitali ya Taifa ya Afya ya Ali ya Mirembe mkoani Dodoma.

Dk Mauki ameyasema hayo leo Oktoba 7, 2023 Dar es Salaam katika kilele cha Waajiri Bonanza lililoandaliwa na Chama Cha Waajiri nchini (ATE) likiwa na Kauli mbiu kuimarisha afya ya akili Ili kuongeza tija mahala pa kazi.

Amesema changamoto ya akili ni janga duniani ambapo katika kila sekunde 40 watu watatu wanapoteza maisha kutokana na tatizo hilo.

Mbali na dalili hizo za awali, kukosa usingizi vizuri kunakosababisha wengine kuchukua hatua za kunywa kilevi na kukosa hamu ya tendo la ndoa kwa wanawake na wanaume nayo ni dalili mojawapo.

Dalili nyingine ni kuongezeka uzito wa ghafla wakati vyakula havijabadilika, hasira   za mara Kwa mara, magonjwa ya vidonda vya tumboni,ngozi, ini na hataagonjwa ya  moyo.

Akizungumza katika bonanza hilo, Dk Mauki ambaye pia ni mtaalam wa saikolojia amesema wengi wamekuwa wakitafsiri vibaya tatizo la afya ya akili kuwa ni wale wanaopelekwa hospitali ya Mirembe.

"Wengi wamekuwa wakipitia changamoto mbalimbali kazini na hata nyumbani...pale unapojiona hauko sawa ni vyema kufahamu ndipo changamoto ya Afya ya akili huanzia,"amesema.

Dk Mauki ameshauri Jamii kuwasaidia watu wenye matatizo hayo na kuepukana na unyanyapaa kwani ni sumu.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Chris Mauki akizungumza katika kilele cha bonanza la waajiri, lililoandaliwa na Chama cha Waajiri Tanzania. Picha na Michael Matemanga

Kwa upande mwingine, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Saad Mtambule amesema kwa kipindi cha miezi saba tangu ateuliwe kushika nafasi hiyo watu sita wamejiua.

Matukio ya kujiua aliyoitaja Mtambule ni yaliyochangiwa na watu kujinyonga na wengine kujirusha ghorofani akitolea mfano tukio lililotokea Kijitonyama Dar es Salaam.

"Tuna tatizo la afya ya akili kwa watu wetu na madhara yake sio madogo yanaondoa uhai,jambo hili la afya ya akili mahala pa kazi ni hatua nzuri ukiwa na watu wenye matatizo ya akili kazi haziendi," amesema.

Katika kukabiliana na changamoto hiyo, amesema tayari wameanza kuhimiza watu kujishughulisha na michezo akieleza tayari wilaya hiyo imekwisha kujenga Uwanja wa michezo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA)Khadija Mwenda amesema vichocheo vya changamoto ya afya akili mahala pa kazi ni masuala ya kibayolojia na Kisaikolojia.

Mwenda amesema ongezeko la magonjwa kwenye jamii limekuwa kubwa akitolea mfano katika kampeni waliyoiendesha hivi karibuni walibaini kati ya watu 300,050 walipima afya watu 100,624 wakibainika kuwa na shinikizo la juu damu,kiharusi na kisukari.

Magonjwa hayo ndiyo Mwenda ameyataja kuyatafuna fedha za waajiri wengi nchini.

Naye Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) Hery Mkunda akizungumza kwenye bonanza hilo amewaomba wadau kuweka mikakati eneo la kazi ili kudhibiti changamoto hiyo na kutengenezà mazingira wezeshi kwa wenye changamoto ya afya ya akili kuifanya kazi kwa uweledi.